Mifepristone: Vidonge vya uavyaji mimba ni salama kiasi gani?

Mifepristone and Misoprostol pills are pictured Wednesday, Oct. 3, 2018, in Skokie, Illinois. (Erin Hooley/Chicago Tribune/Tribune News Service via Getty Images)

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Vidonge vya kutoa mimba vimeruhusiwa nchini Marekani tangu mwaka 2000
  • Author, Natasha Preskey
  • Nafasi, BBC World Service

Kesi inayoendelea Marekani katika mahakama - itaamua iwapo madaktari na wanaharakati wanaopinga uavyaji mimba wanaweza kuzuia upatikanaji wa dawa ya mifepristone kwa sababu za usalama.

Kidonge hicho cha kuavya mimba kimekuwa halali tangu mwaka 2000 nchini Marekani na sheria kuhusu dawa hiyo zimelegezwa hatua kwa hatua tangu 2016.

Mabadiliko ya hivi karibuni ya sheria za Mamlaka ya Chakula na Dawa (FDA), yameruhusu tembe za kuavya mimba kutumwa kwa posta na kuuzwa katika maduka ya dawa bila agizo la daktari.

Majimbo kadhaa yameanzisha marufuku ya utoaji mimba tangu uamuzi wa kihistoria wa Roe v Wade, ambao ulibatilisha haki ya kutoa mimba 2022. Uamuzi katika kesi ya kuavya mimba unatarajiwa kutolewa mwisho wa Juni.

Pia unaweza kusoma

Ni wapi utoaji mimba ni makosa?

Demonstrators hold up signs during a protest in front of the Supreme Court during the "Bans Off Our Mifepristone" action organized by the Woman's March outside of the Supreme Court on March 26, 2024 in Washington DC

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Waandamanaji wanaounga mkono kutoa mimba wakiwa wamekusanyika nje ya Mahakama Kuu huko Marekani

Nchi 21 zina marufuku ya moja kwa moja ya uavyaji mimba, hasa Kusini mwa Ulimwengu, kulingana na data kutoka Kituo cha Haki za Uzazi.

Nchi nyingi zina sheria kali juu ya sababu zinazokubalika za kutoa mimba, na huruhusu tu kuokoa maisha ya mama au katika kesi za ubakaji.

Barani Afrika, nchi nyingi zina sheria zinazozuia utoaji mimba, ingawa nchi chache - ikiwa ni pamoja na Afrika Kusini na Msumbiji – hazina sheria hiyo.

Congo, Senegal, Sierra Leone, Mauritania, Madagascar na Misri zote zina marufuku kamili ya kutoa mimba.

Nchi nyingi za Ulaya huruhusu uavyaji mimba kwa sababu za kiuchumi (kuzingatia hali za kijamii au kiuchumi) au kwa ombi. Nchi zingine zikiwemo Australia na New Zealand pia zinaruhusu utoaji mimba kwa ombi.

Nchini Marekani, hali ni ngumu zaidi. Sheria zinatofautiana kutoka jimbo moja hadi jimbo jingne, tangu haki ya kutoa mimba kubatilishwa mwaka 2022.

Historia ya Mifepristone

Map showing 'Legal status of abortion around the world'

Mifepristone iliidhinishwa kwa mara ya kwanza nchini Ufaransa mwaka 1988 na kulingana na data kutoka shirika la Gyunity, sasa imeidhinishwa kutumika katika nchi 96 - hivi karibuni Argentina, Ecuador, Japan na Niger mwaka jana.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linaorodhesha uavyaji mimba kwa kutumia mifepristone na misoprostol kama sehemu ya miongozo yake ya kupunguza uavyaji mimba usio salama, na linasema dawa hizo zinaweza kutumiwa kwa usalama.

Nchini Marekani, mifepristone imeidhinishwa kwa matumizi hadi wiki 10 za ujauzito, lakini katika nchi nyingine nyingi, hutumiwa kwa utoaji mimba wakati mimba ikiwa katikati.

Je, ni salama?

A woman holds a sign during a demonstration called to commemorate the International Women's Day on 8 March 2024 in Buenos Aires, Argentina

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kidonge hicho kimeruhusiwa katika nchi 96

Misuli kubana na kutokwa damu ukeni hutokea baada ya mtu kutumia mifepristone na kwa kawaida ni ishara kwamba dawa inafanya kazi (ingawa si hakikisho).

Madhara mengine ya kawaida ni pamoja na kichefuchefu, udhaifu, homa, baridi, kutapika, maumivu ya kichwa, kuhara na kizunguzungu.

WHO inasema mifepristone na misoprostol ni salama kwa matumizi na inajumuisha dawa zote mbili kwenye Orodha yake ya Dawa Muhimu.

Lakini wanaharakati wa kupinga uavyaji mimba wanasema dawa ya kutoa mimba, ni hatari na haina ufanisi. Madai yao hayaungwi mkono na mashirika makubwa ya matibabu, kama vile WHO na Jumuiya ya Madaktari ya Marekani.

Kulingana na FDA, kuna vifo vitano kwa watumiaji milioni moja wa mifepristone.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah