Uwezo wake, mafuta na mchoro wa $450m - wadadisi wazungumza juu ya kupanda kwa Mwana Mfalme wa Saudi

.
Maelezo ya picha, Mohammed Bin Salman MBS

Mwezi Januari 2015, Abdullah, mfalme wa Saudi Arabia mwenye umri wa miaka 90, alikuwa akifariki dunia hospitalini. Kaka yake wa kambo, Salman, alikuwa anakaribia kuwa mfalme - na mtoto anayependwa sana na Salman, Mohammed bin Salman, alikuwa akijiandaa kutawala.

Mwana wa mfalme, anayejulikana kwa herufi za mwanzo za jina lake kama MBS na kisha akiwa na umri wa miaka 29, alikuwa na mipango mikubwa kwa ufalme wake, ikiwa ni mipango mikubwa zaidi katika historia yake; lakini alihofia kwamba kuna watu wanaopanga njama ndani ya familia yake ya kifalme ya Saudi ambao hatimaye wangeweza kumpinga. Kwa hiyo usiku wa manane jioni moja mwezi huo, alimwita afisa mkuu wa usalama kwenye ikulu, akiwa ameazimia kupata uaminifu wake.

Afisa huyo, Saad al-Jabri, aliambiwa aache simu yake ya mkononi kwenye meza nje ya ofisi hiyo.

MBS pia naye alifanya vivyo hivyo. Wawili hao sasa walikuwa peke yao. Mtoto wa mfalme aliogopa sana wapelelezi wa ikulu hivi kwamba alitoa soketi nje ya ukuta, hatua iliokata ya pekee iliokua mezani.

Kulingana na Jabri, MBS kisha alisema jinsi ambavyo angetaka kuamsha ufalme wake kutoka kwenye usingizi wake mzito, na kuuruhusu kuchukua nafasi yake ipasavyo kwenye jukwaa la kimataifa.

Kwa kuuza hisa katika kampuni kubwa ya serikali ya uzalishaji wa mafuta Aramco, kampuni yenye faida kubwa zaidi duniani, angeanza kupunguza uchumi wake kutoka kwa utegemezi wake wa mafuta.

Angewekeza mabilioni ya fedha katika uanzishaji wa teknolojia ya Silicon Valley ikijumuisha kampuni ya teksi, Uber. Kisha, kwa kuwapa wanawake wa Saudia uhuru wa kujiunga na wafanyakazi, angeunda nafasi mpya za kazi milioni sita.

Kwa mshangao, Jabri alimuuliza mwanamfalme huyo juu ya ukubwa wa azma yake. Uliwahi kumsikia Alexander The Great , ndilo lililokuwa jibu lake.

MBS alimalizia mazungumzo yake hapo. Mkutano wa usiku wa manane ambao ulipangwa kudumu nusu saa ulifanyika kwa saa tatu.

Jabri alitoka chumbani na kukuta amekosa simu nyingi zilizopigwa katika simu yake kutoka kwa wafanyakazi wenzake wa serikali wakiwa na wasiwasi juu ya kutoweka kwake kwa muda mrefu.

Hadithi ya kupanda kiuwezo kwa mtu ambaye anaiongoza Saudia na ambaye udhibiti wake wa mafuta unaathiri kila mtu , kuanzia jinsi alivyoshinda wengi hadi kuwa mwanamfalme.

Kwa takriban mwaka mmoja sasa, timu yetu ya filamu imekuwa ikizungumza na marafiki na wapinzani wa MBS nchini Saudia , pamoja na majasusi na wanadiplomasia wakuu wa Magharibi.

Serikali ya Saudi ilipewa fursa ya kujibu madai yaliyotolewa katika filamu za BBC na katika makala haya. Walichagua kutofanya hivyo.

Saad al-Jabri alikuwa katika wadhfa wa juu sana katika vyombo vya usalama vya Saudia hali ya kwamba alikuwa na urafiki na wakuu wa CIA na MI6.

Ingawa serikali ya Saudia imemwita Jabri kama afisa wa zamani aliyedharauliwa, yeye pia ndiye mtu aliye na ufahamu zaidi wa Saudi aliyethubutu kuzungumza juu ya jinsi mtoto wa mfalme anavyotawala Saudi Arabia - na mahojiano ambayo ametupatia yanashangaza kwa undani wake.

Kwa kupata ufikiaji wa watu wengi wanaomfahamu mtoto wa mfalme kibinafsi, tunatoa mwanga mpya kuhusu matukio ambayo yamemfanya MBS kujulikana kuwa mbaya - ikiwa ni pamoja na mauaji ya 2018 ya mwandishi wa habari wa Saudi Jamal Khashoggi na kuanzishwa kwa vita vikali nchini Yemen.

Huku baba yake akizidi kudhoofika, MBS mwenye umri wa miaka 38 sasa ndiye msimamizi kamili wa nchi yenye uzawa wa Uislamu na muuzaji mkubwa wa mafuta duniani.

Ameanza kutekeleza mipango mingi ya msingi aliyomueleza Saad al-Jabri - huku pia akishutumiwa kwa ukiukaji wa haki za binadamu ikiwa ni pamoja na kukandamiza uhuru wa kujieleza, kuenea kwa matumizi ya hukumu ya kifo na kufungwa jela kwa wanaharakati wa haki za wanawake.

Mwanzo Mbaya

Mfalme wa kwanza wa Saudi Arabia alizaa angalau wana 42, akiwemo babake MBS, Salman. Taji la ufalme huo limekuwa likirithiwa na wana hawa.

Ni wakati wawili kati yao walipofariki ghafla mwaka 2011 na 2012 ambapo Salman aliinuliwa katika mstari wa urithi.

Mashirika ya kijasusi ya Magharibi yanafanya biashara yao kusoma lugha inayolingana na nani atakuwa mfalme anayefuata. Katika hatua hii, MBS alikuwa mchanga sana na hakujulikani na hata hakuwa kwenye rada yao.

"Alikulia katika hali isiyojulikana," asema Sir John Sawers, mkuu wa MI6 hadi 2014. "Hakuwekwa katika alama ya kuchukua mamlaka."

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mohammed bin Salman

Mwanamfalme huyo alikulia katika jumba ambalo tabia mbaya ilikuwa na wachache, iwapo ingekuwepo; na hiyo inaweza kusaidia kueleza tabia yake mbaya ya kutofikiria matokeo ya maamuzi yake hadi awe tayari ameyafanya.

MBS alijipatia sifa mbaya kwa mara ya kwanza huko Riyadh katika ujana wake, alipopewa jina la utani "Abu Rasasa" au "Baba wa Risasi", baada ya kudaiwa kufyatua risasi kwa hakimu ambaye alimkosoa katika mzozo wa mali.

“Amekuwa na ukatili fulani,” asema Sir John Sawers. "Yeye hapendi kukosewa. Lakini hiyo pia inamaanisha kuwa ameweza kuendesha mabadiliko ambayo hakuna kiongozi mwingine wa Saudia ameweza kufanya.

Miongoni mwa mabadiliko yanayoungwa mkono zaidi, kwa mujibu wa mkuu huyo wa zamani wa MI6 , ni kukata ufadhili wa Saudia kwa misikiti ya ng'ambo na shule za kidini ambazo zimekuwa vyanzo vya jihadi za Kiislamu - kwa faida kubwa kwa usalama wa Magharibi.

Mama yake MBS, Fahda, ni kutoka kabila la Bedouin na anaonekana kuwa kipenzi cha wake wanne wa baba yake.

Wanadiplomasia wa Magharibi wanaamini kwamba mfalme huyo ameugua polepole kwa miaka mingi kutokana na aina ya ugonjwa wa shida ya mishipa; na MBS ndiye mtoto aliyemgeukia kwa usaidizi.

Wanadiplomasia kadhaa walikumbuka mikutano yao na MBS na baba yake. Mkuu huyo angeandika maelezo kwenye kipakatalishi chake na kuyatuma kwa kipakatalishi cha baba yake, kama njia ya kumuuliza angesema nini baadaye.

"Bila shaka nilijiuliza iwapo MBS alikuwa akimwandikia nini cha kusema," anakumbuka Lord Kim Darroch, Mshauri wa Usalama wa Kitaifa wa David Cameron alipokuwa waziri Mkuu wa Uingereza.

Mwana mfalme huyo alikuwa na haraka ya baba yake kuwa mfalme hivi kwamba mwaka 2014, aliripotiwa kupendekeza kumuua mfalme wa wakati huo - Abdullah, mjomba wake - kwa pete yenye sumu, iliyopatikana Urusi.

"Sijui kwa hakika ikiwa alikuwa akijisifu tu, lakini tulichukulia kwa uzito," anasema Jabri. Afisa huyo mkuu wa zamani wa usalama anasema ameona video ya uchunguzi iliyorekodiwa kwa siri ya MBS akizungumza kuhusu wazo hilo. "Alipigwa marufuku , kupeana mikono na mfalme, kwa muda mrefu."

Katika tukio hilo, mfalme alikufa kwa sababu za asili, na kumruhusu kaka yake, Salman, kutwaa kiti cha enzi mwaka wa 2015. MBS aliteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi na hakupoteza muda kwenda vitani.

Vita huko Yemen

Miezi miwili baadaye, mtoto wa mfalme aliongoza muungano wa Ghuba katika vita dhidi ya vuguvugu la Houthi, ambalo lilikuwa limechukua udhibiti wa sehemu kubwa ya magharibi mwa Yemen na ambalo aliliona kama wakala wa mpinzani wa Saudi Arabia wa kikanda wa Iran.

Vita hivyo vilisababisha maafa ya kibinadamu, na mamilioni ya watu wakipatwa na baa la njaa.

“Haukuwa uamuzi wa busara,” asema Sir John Jenkins, ambaye alikuwa balozi wa Uingereza kabla ya vita kuanza. "Kamanda mmoja mkuu wa jeshi la Marekani aliniambia walipewa notisi ya saa 12 kuhusu vita hivyo hiyo, jambo ambalo halijasikika."

Vita hivyo vilisaidia kumgeuza mwanamfalme asiyejulikana sana kuwa shujaa wa taifa la Saudia. Hata hivyo, yalikuwa maamuzi ya kwanza ya yale ambayo hata marafiki zake wanaamini kuwa yamekuwa makosa makubwa.

Mtindo wa mara kwa mara wa tabia yake ulikuwa ukijitokeza: tabia ya MBS ya kugeuza mfumo wa kimapokeo wa polepole na wa pamoja wa kufanya maamuzi wa Saudia, akipendelea kutenda bila kutabirika au kwa msukumo; na kukataa ‘kuiabudu’ Marekani, au hata kuchukuliwa kama kiongozi wa taifa lililo nyuma.

Jabri akimshtumu MBS kwa kughushi saini ya babake ili kuyaamrisha majeshi ya ardhini kupigana .

Jabri anasema alizungumzia vita vya Yemen katika Ikulu ya White House kabla ya kuanza; na kwamba Susan Rice, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Rais Obama, alimuonya kwamba Marekani ingeunga mkono mashambulizi ya angani pekee.

Hata hivyo, Jabri anadai MBS alikuwa imedhamiria kusonga mbele nchini Yemen kiasi cha kwamba aliwapuuza Wamarekani.

"Tulishangaa kwamba kulikuwa na amri ya kifalme ya kuruhusu jeshi kuingilia kati," Jabri anasema. "Alighushi saini ya baba yake kwa amri hiyo ya kifalme. Afya ya baba yake ilikuwa ikizidi kuzorota.”

Jabri anasema chanzo chake cha madai haya ni "cha kuaminika" na kinahusishwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ambapo alikuwa mkuu wa wafanyikazi.

Jabri anamkumbuka mkuu wa kituo cha CIA huko Riyadh akimweleza jinsi alivyokuwa na hasira kwamba MBS amewapuuza Wamarekani, akiongeza kuwa uvamizi wa Yemen haukupaswa kutokea kamwe.

Mkuu wa zamani wa MI6 Sir John Sawers anasema kwamba ingawa hajui iwapo MBS alighushi nyaraka, "ni wazi kwamba huu ulikuwa uamuzi wa MBS kuingilia kijeshi nchini Yemen.

Haukuwa uamuzi wa baba yake, ingawa baba yake alijumlishwa nao.”

Tumegundua kuwa MBS alijiona kama mgeni tangu mwanzo - kijana aliye na mengi ya kuthibitisha na kukataa kutii sheria za mtu yeyote isipokuwa zake.

Kirsten Fontenrose, ambaye alihudumu katika Baraza la Usalama la Kitaifa la Rais Donald Trump, anasema kwamba aliposoma maelezo mafupi ya kisaikolojia ya CIA kuhusu mwanamfalme huyo, alihisi kwamba hayakueleweka.

"Hakukuwa na mifano ya kumtegemeza," anasema. "Amekuwa na rasilimali zisizo na kikomo. Hajawahi kuambiwa ‘hapana’. Yeye ndiye kiongozi wa kwanza kijana kuakisi kizazi ambacho, kusema ukweli, wengi wetu serikalini ni wazee sana kuelewa.

Kuweka sheria zake mwenyewe

Ununuzi uliofanywa na MBS wa mchoro maarufu mwaka wa 2017 unatueleza mengi kuhusu jinsi anavyofikiri, na hali yake ya kutojali kuwa nje ya hatua na jamii ya kihafidhina ya kidini ambayo anaiongoza.

Na juu ya yote hayo, nia ya kuzishinda nchini za Magharibi katika maonyesho ya uwezo wa kijeshi.

Mwaka mwaka wa 2017, mwanamfalme wa Saudia aliyeripotiwa kuchukua amri za MBS alitumia $450m (£350m) kununua Salvator Mundi, ambayo inasalia kuwa kazi ghali zaidi ya sanaa kuwahi kuuzwa.

Picha hiyo, inayosifika kuwa ilichorwa na Leonardo da Vinci, inamwonyesha Yesu Kristo kama bwana wa mbingu na Dunia, mwokozi wa ulimwengu. Kwa takriban miaka saba, tangu mnada huo, picha hiyo imetoweka kabisa.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Ikiwa Salvator Mundi, mchoro wa miaka 500 wa Kristo, ulichorwa na Leonardo da Vinci bado kuna mbishano

Bernard Haykel, rafiki wa mwanamfalme na Profesa wa Mafunzo ya Mashariki katika Chuo Kikuu cha Princeton, anasema kwamba licha ya uvumi kwamba picha hiyo inaning'inia kwenye jahazi au jumba la mfalme, mchoro huo kwa hakika uko kwenye hifadhi huko Geneva na kwamba MBS anakusudia kuutundika kwenye boti ya makumbusho katika mji mkuu wa Saudi ambayo bado haijaundwa.

"Nataka kujenga jumba kubwa la makumbusho huko Riyadh," Haykel anamnukuu MBS akisema. "Na ninataka kitu ambacho kitavutia watu, kama Mona Lisa anavyofanya."

Vile vile, mipango yake ya michezo inaonyesha mtu ambaye ana tamaa kubwa na asiye na hofu ya kuvuruga hali ilivyo.

Matumizi ya ajabu ya Saudi Arabia katika michezo ya kiwango cha kimataifa - ndiyo mzabuni pekee wa kuandaa Kombe la Dunia la FIFA mwaka wa 2034, na imefanya uwekezaji wa mamilioni ya dola katika mashindano ya tenisi na gofu - imeitwa "kutumia michezo kujitakasa ". Lakini tulichogundua ni kiongozi ambaye hajali sana kile ambacho nchi za Magharibi zinamfikiria kuliko anavyofanya juu ya kuonyesha kinyume chake: kwamba atafanya chochote anachotaka kwa jina la kujifanya yeye na Saudi Arabia kuwa wakuu.

"MBS ana nia ya kujenga mamlaka yake kama kiongozi," anasema Sir John Sawers, Mkuu wa zamani wa MI6, ambaye amekutana naye. "Na njia pekee ya kufanya hivyo ni kwa kujenga mamlaka ya nchi yake. Hicho ndicho kinachomsukuma.”

Miaka 40 ya kazi ya Jabri kama afisa wa Saudi haikunusurika katika uimarishaji wa mamlaka ya MBS. Mkuu wa wafanyikazi wa aliyekuwa Mwanamfalme Muhammed bin Nayef, alitoroka ufalme wakati MBS alipochukua hatamu, baada ya kufahamishwa na idara ya kijasusi ya kigeni kwamba anaweza kuwa hatarini. Lakini Jabri anasema MBS ilimtumia ujumbe na kumuomba arejee ili ampe kazi yake ya zamani.

"Ilikuwa chambo - na sikuuma," Jabri anasema, akiwa na hakika kwamba angeteswa, angefungwa au kuuawa kama angerejea. Ilivyokuwa, na watoto wake Omar na Sarah, waliwekwa kizuizini na baadaye kufungwa jela kwa utakatishaji fedha na kwa kujaribu kutoroka - mashtaka ambayo wanayakanusha. Kikosi Kazi cha Umoja wa Mataifa kuhusu Ufungwaji Kiholela kimetoa wito wa kuachiliwa kwao.

"Alipanga kuuawa kwangu," Jabri anasema. "Hatapumzika mpaka anione nimekufa, sina shaka na hilo."

Maafisa wa Saudi wametoa notisi za Interpol kuhusu kurejeshwa kwa Jabri kutoka Canada, bila mafanikio. Wanadai anasakwa kwa ufisadi unaohusisha mabilioni ya dola wakati alipokuwa katika wizara ya mambo ya ndani. Hata hivyo, alipewa cheo cha meja jenerali na kusifiwa na CIA na MI6 kwa kusaidia kuzuia mashambulizi ya kigaidi ya al-Qaeda

Mauaji ya Khashoggi

Mauaji ya Jamal Khashoggi katika ubalozi mdogo wa Saudia huko Istanbul mnamo 2018 yanamhusisha MBS kwa njia ambazo ni ngumu sana kukanusha. Kikosi hicho cha watu 15 kilikuwa kikisafiri kwa pasipoti za kidiplomasia na kilijumuisha walinzi kadhaa wa MBS. Mwili wa Khashoggi haujawahi kupatikana na inaaminika kukatwa vipande vipande kwa msumeno wa mfupa.

Profesa Haykel alibadilishana ujumbe wa WhatsApp na MBS muda mfupi baada ya mauaji hayo. “Nilikuwa nikiuliza, ‘hii inawezaje kutokea?’,” Haykel akumbuka. "Nadhani alikuwa katika mshtuko mkubwa. Hakugundua mwitikio wa hii ungekuwa wa kina sana."

Dennis Ross alikutana na MBS muda mfupi baadaye. "Alisema hakuifanya na kwamba ilikuwa kosa kubwa," anasema Ross. "Kwa hakika nilitaka kumwamini, kwa sababu sikuweza kuamini kwamba angeweza kuidhinisha kitu [kama] hicho."

.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Mwandishi wa habari wa Saudi Jamal Khashoggi alikuwa amekosoa sera za MBS

MBS daima amekuwa akikana kufahamu njama hiyo, ingawa mwaka wa 2019 alisema alichukua "kuwajibika" kwa sababu uhalifu ulifanyika wakati wake. Ripoti ya kijasusi ya Marekani iliyotolewa Februari 2021 ilidai kuwa alihusika katika mauaji ya Khashoggi.

Niliwauliza wale wanaomjua MBS binafsi iwapo amejifunza kutokana na makosa yake; au iwapo kisa cha Khashoggi, kilimpa nguvu zaidi.

"Amejifunza kwa njia ngumu," anasema Profesa Haykel, ambaye anasema MBS anachukizwa na kesi hiyo kutumika kama chuki dhidi yake na nchi yake, lakini kwamba mauaji kama ya Khashoggi hayatatokea tena.

Sir John Sawers anakubali kwa uangalifu kwamba mauaji hayo yalibadili mamabo mengi. "Nadhani amejifunza ila utu wake unasalia vile vile."

Baba yake, Mfalme Salman, sasa ana umri wa miaka 88. Anapofariki, MBS iaaweza kutawala Saudi Arabia kwa miaka 50 ijayo.

Hata hivyo, hivi majuzi amekiri kuwa anahofia kuuawa, pengine kutokana na majaribio yake ya kurejesha uhusiano wa Saudi na Israel.

“Nafikiri kuna watu wengi wanaotaka kumuua,” asema Profesa Haykel, “na anajua hilo.”

Uangalifu wa milele ndio unaomweka mtu kama MBS salama. Ilikuwa ni kile Saad al-Jabri alichoona mwanzoni mwa mfalme huyo kuingia madarakani, alipokata simu kabla ya kuzungumza naye kwenye kasri lake.

MBS bado ni mtu mwenye dhamira ya kuifanya nchi yake kuwa ya kisasa, kwa njia ambazo watangulizi wake hawangethubutu kamwe.

Lakini pia sio mtawala wa kwanza ambaye ana hatari ya kuwa mkatili hivi kwamba hakuna mtu karibu naye anayethubutu kumzuia kufanya makosa zaidi.

Jonathan Rugman ni mtayarishaji mshauri wa Ufalme: Mwana wa mfalme mwenye nguvu zaidi duniani

Imetafsiriwa na Seif Abdalla