'Jehanamu halisi': Wanawake wa Sudan wanavyokabiliwa na ubakaji na unyanyasaji nchini Libya

"Tunaishi kwa hofu,"Layla anasema kwa njia ya simu kwa sauti ya kunong'oneza ili mtu asimsikie . Alitoroka Sudan na mumewe na watoto sita mapema mwaka jana kutafuta usalama na sasa yuko Libya.
Kama ilivyo kwa wanawake wote wa Sudan ambao BBC ilizungumza nao kuhusu uzoefu wao wa kusafirishwa kwenda Libya, jina lake limebadilishwa ili kulinda utambulisho wake.
Tahadhari: Hadithi hii ina maelezo ambayo yananaweza kuwasikitisha baadhi ya watu
Kwa sauti ya kutetemeka anaelezea jinsi nyumba yake huko Omdurman ilivyovamiwa wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Sudan, ambavyo vilizuka mnamo 2023.
Familia hiyo ilikwenda Misri kwanza baada ya kuwalipa wasafirishaji dola 350 (£338) kuwapeleka Libya, ambako waliambiwa maisha yatakuwa bora na wataweza kupata kazi za usafi na hoteli.
Lakini mara baada ya kuvuka mpaka, Layla anasema wasafirishaji waliwashikilia mateka, kuwapiga na kudai pesa zaidi.
"Ilibidi mwanangu atibiwe baada ya kupigwa mara kwa mara usoni," aliiambia BBC.
Wasafirishaji hao waliwaachia huru baada ya siku tatu, bila kusema ni kwa nini. Layla alidhani maisha yake mapya nchini Libya yameanza kuwa mazuri baada ya familia hiyo kufanikiwa kusafiri magharibi na kukodi chumba na kuanza kufanya kazi.
Lakini siku moja mume wake aliondoka kwenda kutafuta kazi na hakurudi tena. Kisha binti yake wa miaka 19 alibakwa na mwanamume anayejulikana kwa familia kupitia kazi ya Layla.
"Alimwambia binti yangu kuwa angembaka dada yake mdogo ikiwa angezungumza juu ya kile alichomfanyia," Layla anasema.
Anazungumza kwa sauti ya kutetemeka akihofia familia itafukuzwa mwanamke mwenye nyumba alikopangisha atasikia anachokisema.
Layla anasema kwa sasa wamekwama nchini Libya: hawana pesa za kuwalipa wasafirishaji wa watu kuondoka na hawawezi kurudi katika Sudan iliyokumbwa na vita.
"Hatuna chakula cha kutosha," anasema, akiongeza kuwa watoto wake hawaendi shuleni. "Mwanangu anaogopa kuondoka nyumbani kwani watoto wengine mara nyingi humpiga na kumtusi kwa kuwa mweusi. Nahisi ni kama nitarukwa na akili."

Chanzo cha picha, Getty Images
Mamilioni ya watu wameikimbia Sudan tangu vita kati ya jeshi na vikosi vya kijeshi vya Rapid Forces (RSF) vilipozuka mwaka 2023. Pande hizo mbili kwa pamoja zilifanya mapinduzi mwaka 2021, lakini mapambano ya kuwania madaraka kati ya makamanda wao yaliitumbukiza nchi hiyo katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Zaidi ya watu milioni 12 wamelazimika kuyakimbia makaazi yao, wakati njaa imesambaa katika maeneo matano, huku watu milioni 24.6, ikiwa ni karibu nusu ya idadi ya watu - wanahitaji msaada wa haraka wa chakula, wataalamu wanasema.
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesema zaidi ya wakimbizi 210,000 wa Sudan sasa wako nchini Libya.
BBC imezungumza na familia tano za Wasudan ambao awali walikwenda Misri, ambako walisema walikabiliwa na ubaguzi wa rangi na vurugu, kabla ya kuhamia Libya, wakiamini kuwa itakuwa salama na fursa bora za kazi. Tuliwasiliana nao kupitia mtafiti katika masuala ya uhamiaji na kutafuta hifadhi nchini Libya.
Salma ameiambia BBC kuwa tayari alikuwa akiishi mjini Cairo, Misri, akiwa na mume wake na watoto watatu wakati vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Sudan vilipozuka, lakini wakati idadi kubwa ya wakimbizi walipoingia nchini humo, hali ya wahamiaji nchini humo ilizidi kuwa mbaya.
Waliamua kuhamia Libya, lakini kilichokuwa kinawasubiri kilikuwa ni "jahanamu halisi", Salma anasema.
Anaelezea jinsi, mara tu walipovuka mpaka, walivyowekwa katika ghala linaloendeshwa na wasafirishaji wa binadamu. Wanaume hao walitaka pesa ambazo zilikuwa zimelipwa mapema kwa wasafirishaji wa bidhaa za magendo upande wa Misri wa mpaka, lakini hazikufika.
Familia yake ilikaa karibu miezi miwili katika ghala. Wakati mmoja, Salma alitenganishwa na mumewe na kupelekwa kwenye chumba cha wanawake na watoto. Hapa, anasema yeye na watoto wake wawili wakubwa walifanyiwa ukatili wa aina mbalimbali kwasababu walitaka pesa.
"Viboko vyao viliacha alama kwenye miili yetu. Walimpiga binti yangu na kuweka mikono ya mwanangu kwenye oveni inayowaka wakati nikitazama.
"Wakati mwingine nilitamani sote tufe pamoja. Sikuweza kufikiria njia nyingine ya kutoka."
Salma anasema mtoto wake na binti yake waliathirika na tukio hilo na wameteseka kutokana na usumbufu tangu wakati huo. Baada ya hapo anapunguza sauti yake.
"Walinipeleka kwenye chumba tofauti, 'chumba cha ubakaji' na wanaume tofauti kila wakati," anasema. "Nimemzaa mtoto wa mmoja wao."
Hatimaye, alikusanya pesa kupitia rafiki yake huko Misri na wasafirishaji wakaiachilia familia yake.
Anasema daktari alimwambia kuwa alikuwa amechelewa sana kutoa mimba, na mumewe alipogundua kuwa alikuwa mjamzito alimuacha yeye na watoto, na kuwaacha wakila mabaki ya chakula kutoka kwenye mapipa ya takataka na kuombaomba mitaani.
Walipata hifadhi katika shamba la mbali kaskazini magharibi mwa Libya kwa muda, wakikaa siku nzima bila kupata chakula. Walikata kiu yao kwa kunywa maji machafu kutoka kwenye kisima kilicho karibu.
"Inavunja moyo wangu kusikia mwanangu akisema kuwa anakufa kwa njaa," Salma anasema kwa njia ya simu, huku vilio vya watoto wake vikizidi kuongezeka.
"Ana njaa sana," anasema, "lakini sina chochote, hata maziwa ya kutosha katika matiti yangu kumlisha."

Chanzo cha picha, Getty Images
Jamila, mwanamke wa Sudan mwenye umri wa miaka 40, pia aliamini taarifa ndani ya jamii ya Sudan kwamba maisha bora yanawasubiri nchini Libya.
Alitoroka machafuko ya awali katika jimbo la magharibi mwa Sudan la Darfur mwaka 2014 na alikaishi Misri kwa miaka kadhaa kabla ya kuhamia Libya mwishoni mwa mwaka 2023. Anasema binti zake wamekuwa wakibakwa mara kwa mara tangu wakati huo - walikuwa na umri wa miaka 19 na 20 wakati tukio hilo lilipotokea kwa mara ya kwanza.
"Niliwatuma kufanya kazi ya usafi wakati nilipokuwa mgonjwa; walirudi usiku wakiwa wamejaa uchafu na damu - wanaume wanne waliwabaka hadi mmoja wao alipozimia," aliiambia BBC.
Jamila anasema pia alibakwa na kushikiliwa mateka kwa wiki kadhaa na mwanamume, mdogo kwake kiumri, ambaye alikuwa amempa kazi ya kusafisha nyumba yake.
"Alikuwa akiniita 'mzungu mweusi'. Alinibaka na kusema, 'Hilo ndio wanawake waliloumbiwa,'" anakumbuka.
"Hata watoto hapa hawana maana kwetu, wanatuchukulia kama wanyama na wachawi, wanatutukana kwa kuwa weusi na Waafrika, wao si Waafrika ");