'Mnibake mimi na sio binti zangu' - vita vya kutisha vya Sudan

Chanzo cha picha, BBC/Mohanad Hashim
- Author, Barbara Plett Usher
- Nafasi, BBC Africa correspondent, Omdurman
Sudan iko katika hali mbaya.
Baada ya miezi 17 ya vita vya kikatili vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoiangamiza nchi hiyo, jeshi limefanya mashambulizi makubwa katika mji mkuu Khartoum, yakilenga maeneo yaliyo mikononi mwa mpinzani wake mkali, Kikosi cha RSF
RSF iliteka sehemu kubwa ya Khartoum mwanzoni mwa mzozo, wakati jeshi linadhibiti mji pacha wa Omdurman, ng'ambo ya Mto Nile.
Lakini bado kuna mahali ambapo watu wanaweza kuvuka kati ya pande hizo mbili.
Wakati mmoja, nilikutana na kikundi cha wanawake ambao walikuwa wametembea kwa saa nne hadi sokoni katika eneo linalodhibitiwa na jeshi kwenye ukingo wa Omdurman, ambapo chakula ni cha bei nafuu.