'Mtoto kuzaa mtoto': Sera yenye utata ya Urusi kushughulikia tatizo la idadi ya watu

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wanafunzi wa chini ya miaka 25 na - katika mikoa mitatu - wanafunzi wa kike wanastahiki usaidizi wa kifedha
Pia unaweza kusoma

Mipango mipya ya kulipa posho nchini Urusi kwa wanafunzi wajawazito, wakiwemo wasichana wa shule ya upili, imezua utata.

Wakosoaji wanaonya kuwa sera hiyo inaweza kushinikiza mimba za vijana.

Lengo kuu la mpango huo ni kupambana na kushuka kwa viwango vya kujifungua nchini.

Kulingana na takwimu zilizokusanywa na BBC Russia, tangu Januari mwaka huu, mikoa 27 nchini Urusi imeanzisha mipango ambayo wanafunzi katika elimu ya juu ambao ni wajawazito wanaweza kupokea posho.

Katika mikoa mingi, wanawake walio chini ya umri wa miaka 25 hupatiwa posho hiyo.

Kiasi cha posho hiyo kinatofautiana, lakini katika mikoa mingi ni karibu rubles 100,000 ($ 1,210)

"Hili ni janga, sio ujasiri"

Kesi zenye utata zaidi zimetokea katika mikoa mitatu ya Oryol, Bryansk na Kemerovo, ambapo mipango ya serikali imejumuisha wasichana wa shule ya upili wajawazito.

Hii ina maana kwamba vijana walio na umri wa miaka 18 au chini wamejumuishwa. Hakuna kikomo maalum cha umri, ingawa umri wa kisheria wa idhini ya ngono nchini Urusi ni 16.

Ksenia Goryacheva, mwanachama wa Jimbo la Duma na mtu mwaminifu kwa serikali ya Putin, ni mkosoaji wa sera hii.

"Mtoto anapozaa mtoto mwingine, si ujasiri, ni janga," anasema. "Tusiruhusu kirahisi watoto kutumiwa kurekebisha takwimu za idadi ya watu."

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mwaka jana, idadi ya chini ya watoto ilizaliwa nchini Urusi katika kipindi cha miaka 25 iliyopita

Nina Ustanina, naibu mashuhuri wa Duma kuhusu haki za familia, pia alionya kwamba msaada huo ungeweza kuonekana kuwa "matangazo ya mimba za utotoni" na kupingana na "maadili ya kimapokeo." Hata hivyo, alisisitiza kuwa serikali haina nia ya kuwahimiza vijana walio chini ya miaka 18 kujifungua.

Meya wa Oryol Andrei Klychkov anasema sera hiyo ilianzishwa katika eneo lake baada ya kupokea agizo kutoka kwa Wizara ya Kazi ya Urusi, ingawa agizo hilo halijawekwa wazi.

"Hatua hii inapaswa kuonekana kama msaada wa serikali ulioidhinishwa na serikali kwa watu walio katika hali ngumu - sio vichwa vya habari vya utata na vya kupotosha," anaongeza.

"Janga kwa mustakabali wa nchi"

Mwaka jana iliona kiwango cha chini cha kuzaliwa kwa Urusi katika miaka 25; ni watoto milioni 1.2 tu ndio walizaliwa.

Mnamo Juni, msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alielezea kiwango cha kuzaliwa kama "chini sana" na "janga kwa mustakabali wa nchi."

Makadirio ya Shirika la Takwimu la Urusi (Rostat) yanaonyesha kuwa idadi ya watu nchini itaongezeka kutoka milioni 146 mwanzoni mwa 2023 hadi milioni 139 mnamo 2046.

Suala la idadi ya watu limekuwa lengo la hotuba za Vladimir Putin kwa miaka.

"Kuboresha hali ya idadi ya watu, kusaidia viwango vya uzazi na familia kubwa ni moja ya vipaumbele vya kitaifa," alisema Desemba iliyopita.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rais wa Urusi Vladimir Putin, pichani akitembelea hospitali ya uzazi mwaka 2013, amezungumza mara kwa mara kuhusu kiwango cha kuzaliwa nchini humo.

Katika miezi ya hivi karibuni, kumekuwa na ongezeko la wito kwa wanawake kuanzisha familia katika umri mdogo.

Katika mkutano wa Februari, Igor Kogan, profesa katika Chuo cha Sayansi cha Kirusi, alisema kuwa uzoefu wa kwanza wa kijinsia wa wasichana wa Kirusi (ambayo hutokea karibu na umri wa miaka 16) inapaswa "kuishia kwa ujauzito na kuzaa kwa mafanikio."

Baadaye alifafanua kwamba kwa "zama za asili zaidi" kwa suala hili alimaanisha kati ya 19 na 22

Mtaji wa uzazi

Hadi sasa, ni kikundi kidogo tu cha wanawake ambacho kimepokea msaada huo. BBC imekusanya taarifa kuhusu wanafunzi 66 wajawazito ambao wamepokea kati ya rubles 20,000 na 150,000 ($242 na $1,815) katika mikoa mbalimbali ya Urusi tangu Januari.

Anton Kutyakov, Waziri wa Kazi na Ustawi wa Jamii wa Urusi, anasema malipo hayo hayalengi kuhimiza uzazi wa mapema, bali kusaidia akina mama wanaokabiliwa na hali ngumu ya maisha.

"Msaada wa serikali unapaswa kupatikana kwa akina mama wote wanaouhitaji. Haijalishi wana umri gani-hatuwezi kuwaacha peke yao katika mazingira magumu."

Manufaa haya yanaongezwa kwa mipango mingine iliyopo, ikijumuisha "mtaji wa uzazi." Mpango huo ulizinduliwa mwaka wa 2007 na awali ulilipwa kwa akina mama walio na mtoto wa pili pekee, lakini baadaye ulitolewa kwa akina mama wa mara ya kwanza.

Familia sasa hupokea rubles 690,000 ($8,349) kwa kuzaliwa kwa mtoto wao wa kwanza na rubles 222,000 ($2,686) kwa kuzaliwa kwa mtoto wao wa pili.

Ruzuku mpya kwa wanafunzi na wasichana wa shule ya upili ni nyongeza ya miradi hii

Mwenendo wa kimataifa wa kushuka kwa viwango vya kujifungua

Kupungua kwa viwango vya kuzaliwa na tabia ya wanawake kuchelewesha kuzaa ni jambo la kimataifa, haswa katika nchi tajiri.

Nchini Urusi, kiwango cha kuzaliwa kilishuka sana katika miaka ya 1990 kufuatia kuanguka kwa Umoja wa Kisovieti na migogoro ya kiuchumi, kutoka kwa watoto milioni mbili mwaka 1990 hadi milioni 1.2 mwaka 1999.

Ingawa idadi hii iliongezeka katika miaka ya 2000, imekuwa ikipungua tena tangu 2016. Kupungua huku kunatokana na idadi ndogo ya watu waliozaliwa katika miaka ya 1990, pamoja na kupungua kwa kiwango cha uzazi kwa kila mwanamke.

Kulingana na takwimu za OECD za 2022, kiwango cha uzazi nchini Urusi kilikuwa watoto 1.4 kwa kila mwanamke, juu kuliko Italia (1.2) lakini chini kuliko Ufaransa (1.8). Kwa utulivu wa idadi ya watu (bila kujumuisha uhamiaji), nambari hii inapaswa kukaribia 1.2.

Wachambuzi wengine pia wanataja sababu kama vile vita vya Ukraine, kuyumba kwa uchumi, kutumwa kwa wanaume katika mstari wa mbele wa vita , na kuhama kwa wanaume kutoroka kusajiliwa kuwa wanajeshi.

Kiwango cha juu na cha chini

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wataalamu wanasema usalama wa kifedha ndio sababu kuu katika uamuzi wa kupata watoto

Wataalamu wanasema juhudi za serikali za kubadilisha mwelekeo wa idadi ya watu hazijafanikiwa kwa muda mrefu.

"Katika miongo michache iliyopita, hakuna mtu aliyefanikiwa kuongeza kiwango cha kuzaliwa kwa watoto wa kwanza, si katika Urusi au katika nchi nyingine," anasema Alexey Rakhsha, mwanademografia wa kujitegemea wa Kirusi.

Hata hivyo, anaamini kuwa mpango wa "mtaji wa uzazi" hapo awali uliwezasha kuzaliwa kwa mtoto wa pili.

John Ermish, profesa mstaafu wa demografia ya familia katika Chuo Kikuu cha Oxford, anasisitiza kwamba athari za usaidizi wa kifedha mara nyingi ni za muda: "Kwa kawaida huwa na kiwango cha juu cha muda mfupi, kisha hupungua."

Hana matumaini zaidi kuhusu sera za kuongeza viwango vya kuzaliwa kati ya wanawake walio na umri wa chini ya miaka 20: "Nchini Uingereza na Marekani, lengo ni kupunguza mimba za ujana, kwa sababu aina hizi za mimba kwa kawaida husababisha madhara ya kijamii na kiafya, si familia kubwa, kama serikali fulani zinavyotumaini."

Wataalamu wote wawili wanaamini kuwa usalama wa kiuchumi ndio ufunguo wa kuongeza kiwango cha kuzaliwa.

"Bila hali ya usalama na utulivu, hakuna mwanamke atakayekuwa tayari kupata mtoto, hata kwa usaidizi wa kifedha," anasema Ermish.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Seif Abdalla