WARIDI WA BBC: ‘Kwanini watu hufikiria walemavu hawana hisia za mapenzi?’

Na Anne Ngugi

.

Chanzo cha picha, Mwende

Josphine Mwende kutoka nchini Kenya anaishi na hali inayoathiri ubongo kwa jina maarufu ‘Cerebral palsy’ kwa kiingereza akiwa sasa ametimiza umri wa miaka 34 mwaka huu.

Anatumia simulizi ya maisha yake hasa kuwapa moyo wanawake wanaoishi na hali moja au nyengine ya ulemavu kujikubali na kujipenda jinsi walivyo.

Uzoefu wake umetokana na maisha hasa yake alipoingia kwenye uhusiano wa kimapenzi, hali kadhalika ulipowadia wakati wake wa kujifungua yapata miaka saba iliyopita.

Ulimwengu wa mapenzi

.

Josphine kama watoto wengine wa rika lake alikulia mazingira ya mashambani na anasema ilichukua muda kwake kufahamu kuwa ana maumbile tofauti na watoto wengine.

Umri ambao alitakikana kuanza kujihudumia mwenyewe katika mambo kama vile kula, kunywa, kuoga na kadhalika, iligunduliwa kwamba hakuwa na uwezo wa kutumia mikono yake. Ikiwa ni mojawapo ya athari za hali anayoishi nayo ya Cerebral palsy.

Na kuanzia wakati huo alianza kutumia miguu yake kwa kazi zote za kawaida.

Alipohitimisha masomo yake, tayari alikuwa ameamua kuwa atapigania haki za watu kama yeye.

Moja ya changamoto kubwa ambazo anasema alikabiliana nazo kama kijana wa kike na ambaye anaishi na ulemavu ilikuwa ni ulimwengu wa kupata mpenzi na kuchumbiana.

“Tangu nikiwa mdogo, nilifahamu kuwa jamii inayonizunguka ina dhana tofauti kuhusiana na watu kama mimi kuwa katika mahusiano ya kimapenzi. Nilihisi kana kwamba watu walikuwa na maoni kwamba mtu kama mimi hapaswi kujihusisha na mapenzi ila hali halisi ni kuwa, hata sisi tunahisia kama watu wengine,” Josphine anasema.

Miaka minane iliyopita Josphine Mwende aliingia kwenye uhusiano wa kimapenzi na mwanamume mmoja.

Mwanamke huyu anasema kuwa mapenzi yao yalikuwa kama ya watu wengine na hakukuwa na bugudha zozote.

Anakumbuka penzi likinoga na mpenzi wake akimwahidi kuwa na wakati mzuri wakati wakichumbiana.

Ila wakati Josphine alipogundua ameshika ujauzito, anasema kwamba mambo yalibadilika kwa kiasi kikubwa licha ya kuwa mpenzi wake alimpongeza kwa kushika mimba.

Baada ya habari hizo za ujauzito, mpenzi wake alipotea na hakuonekana tena.

Josphine na familia yake walikubali ukweli kwamba angekuwa mama mlezi wa pekee.

“Baada ya kumweleza kuwa nina ujauzito, mpenzi wangu hakuonekana tena. Alimuona mtoto wetu akiwa na umri wa mwaka mmoja na tangu wakati huo sijamuona wala kumsikia. Sijui ikiwa ulemavu wangu ulichangia yeye kuniacha mpweke au vipi ila nimekubali hali hiyo,” Josphine anasema.

.

Tukio la kujifungua

Muda uliwadia wa mwanadada huyo kujifungua na pilkapilka za kwenda hospitalini, vilevile, zilikuwa na changamoto zake.

Hospitali ya kwanza aliyoingia anadai kuwa walimkataa kwa misingi ya ulemavu wake. Hospitali ya pili mwanadada huyu anasema kuwa pia walimtataa na anaongeza kwamba muuguzi aliyekuwa kwenye zamu alisema ‘’Huwa hatuwahudumii watu kama nyinyi,” Josphine anakumbuka.

Mwanamke huyu anasema kuwa matamshi hayo yalimsononesha sana na anashukuru Mungu kwamba hatimaye hospitali moja ilikubali kumhudumia na alijaaliwa kujifungua mtoto wa kiume na kuamua kumwita jina ‘GIFT’ ikimaanisha ZAWADI, kama njia ya kukumbuka safari aliyoipitia na kumuona mwanae kama zawadi kuu kwake.

.

Chimbuko la ndoto ya Josphine

Tukio hilo lilikuwa chimbuko la maono ya Josphine Mwende kuzungumza na wanawake walemavu juu ya changamoto zinazowakabili wakati wa ujauzito hadi wakati wa kujifungua.

Mwanadada huyo anasema kuwa ni wakati wanawake walemavu wasimamie haki zao na pia kujumuika pamoja ili waweze kutiana moyo hasa katika nyakati ambazo wanakabiliwa na unyanyapaa kwa mfano, wakiwa na ujauzito, wakati wa kuchumbiwa au kuchumbiana na kadhalika.

Pia unaweza kusoma:

Imeandaliwa na Anne Ngugi