Afya: Magonjwa hatari ambayo wanasayansi hawajayapatia tiba kamili na namna yanavyotibiwa

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Alzheimer ni ugonjwa wa ubongo
  • Author, Dinah Gahamanyi
  • Nafasi, BBC News Swahili
  • Akiripoti kutoka Nairobi

Kuna magonjwa mengi ambayo wanasayansi na madaktari duniani wanaweza kuyatibu kwa urahisi kutokana na kwamba yamefanyiwa utafiti na tiba yake imepatikana. Hata hivyo kuna baadhi ya magonjwa ambayo bado tafiti nyingi za kisayansi zimeshindwa kuyaelewa, na kuyapatia tiba kamili. Magonjwa hayo yamekuwa kero kwa waathiriwa kutokana na kwamba hayatibiki.

Haya ni baadhi ya magonjwa hayo:

Ugonjwa wa Alzheimer

w

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kupoteza kumbukumbu na ufahamu, na kuchanganyikiwa ni mojawapo ya dalili za ugonjwa huu unaosababisha kufa kwa seli za ubongo.

Alzheimer ni ugonjwa wa ubongo unaosababisha kudhoofika kwa ufanisi wa ubongo huwapata waathiriwa kwa viwango tofauti. Sababu halisi ya ugonjwa huu haijaeleweka na hauwezi kutibiwa kwa ufanisi. Kupoteza kumbukumbu na ufahamu, , kuchanganyikiwa, tabia isiyotabirika, na matatizo ya kisaikolojia ni baadhi ya dalili zake.

Mwaka 2023 wanasayansi nchini Uingereza na Ubelgiji walitangaza kuwa huenda wamegundua jinsi seli za ubongo hufa na kusababisha ugonjwa wa Alzheimer. Hatahivyo bado utafiti kuhusu ugonjwa huo na tiba yake unaendelea, na hakuna mafanikio yaliyokwisha patikana.

Unaweza pia kusoma:
g

Chanzo cha picha, Uganda Wildlife Authority

Maelezo ya picha, Inaaminiwa kuwa VVU/Ukimwi vilitoka kwenye sokwe na kusambaa hadi kwa binadamu

VVU/Ukimwi

Tangu ulipotambuliwa kwa mara ya kwanza miaka ya 80, bado hakuna tiba ya ya Upungufu wa Kinga Mwilini. UKIMWI unasalia kuwa miongoni mwa magonjwa yanayouwa watu wengi zaidi duniani, hasa katika nchi zinazoendelea. Inaaminiwa kuwa ugonjwa huo ulianzia kwa sokwe na kusambaa hadi kwa binadamu, utafiti ulibainisha.

Waathiriwa wa Ukimwi hatahivyo hupewa dawa za kupunguza makali ya virusi vya ugonjwa huo kama vile Anti-retravirals na wengi wao huishi kwa muda mrefu.

g

Chanzo cha picha, DOREEN MORAA MORACHA

Maelezo ya picha, Doreen Moraa Moracha, kutoka Kenya, alizaliwa na Virusi vya Ukimwi lakini aligundua akiwa na umri wa miaka 13, mwaka wa 2005.

Homa ya mafua ya ndege (Bird Flue)

Mafua ya ndege husababishwa na virusi ambavyo viligunduliwa karibu miaka 150 iliyopita, na kusambaa kutoka kupitia ndege wa wanaohamahama .

Homa ya mafua ya ndege ambayo kwa sasa inafahamika kwa lugha ya kitaalamu kama H5 husambaa kwa binadamu kupitia milipuko ya ndege mbalimbali wakiwemo wanaofugwa nyumbani kama kuku, na wanyama hata ng’ombe.

Japo mafua ya ndege huwa makali na vigumu kutibika, Taasisi ya Afrika ya udhibiti wa magonjwa (CDC), inashauri kuwa dawa ya avian influenza inaweza kutumika haraka ndani ya kipindi cha siku tano za maambukizi, licha ya kwamba dawa za kukabiliana na virusi za neuraminidase inhibitors zinaweza kutumika wakati wowote mtu anapokuwa mgonjwa.

Mafua ya Kawaida

Ingawa watu wanaokadiriwa kufikia bilioni moja nchini Marekani kila hupata na mafua ya kawaida kila mwaka, madaktari bado wana taarifa chache sana kuhusu mafua hayo ambayo husababisha mtiririko wa makamasi kutoka puani pia kikohozi.

Wataalamu wengi wanashauri watu kunywa supu ya kuku, maji ya ndimu au limao mara nyingi ni dawa pekee inayosaidia na sio dawa za maambukizi za Antibiotiki.

Ugonjwa wa Pica

Pica ni tatizo au hali ya kiafya ya ulaji ambapo mgonjwa khulazimika kula vitu ambavyo sio vyakula ambavyo havina thamani yoyote ya lishe. -

Watu waliogunduliwa kuwa na Pica huwa na hamu kubwa ya kula vitu visivyo vya chakula kama vile uchafu, karatasi, gundi na udongo.

Maradhi haya yanaweza kusababisha matatizo makubwa ikiwa mtu mwenye hali hii atakula kitu chenye sumu au hatari.

Ingawa ugonjwa wa pica unaaminika kuhusishwa na upungufu wa madini, wataalam wa afya hawajapata sababu halisi na hakuna tiba ya ugonjwa huo wa kipekee.

Magonjwa ya Autoimmune

Magonjwa ya autoimmune ni hali ambayo mfumo wako wa kinga ya mwili huharibu vibaya seli zenye afya katika mwili wako. Hali hii husababisha magonjwa mbali mbali ikiwa ni pamoja na mpasuko kwenye ute wa unaounganisha viungo, hali inayofahamika kama arthritis ya rheumatoid, ugonjwa wa Crohn, na hali fulani inayoathiri tezi.

Kwa kawaida, mfumo wetu wa kinga unaweza kujua tofauti kati ya seli za kigeni na seli zako.

Lakini ikiwa una ugonjwa wa autoimmune, mfumo wako wa kinga hushindwa kutambua sehemu za mwili wako, kama vile viungo vyako au ngozi, kama seli za kigeni. Hutoa protini inayoitwa autoantibodies ambayo hushambulia seli zenye afya.

Ugonjwa wa Autoimmune ni ugonjwa ambao hauna tiba, hivyo basi mgonjwa hupewa dawa za kutuliza maumivu na kupunguza uvimbe mwilini (antinflammations)

Schizophrenia

Schizophrenia ni ugonjwa unaosababisha madhara makubwa kwa ukuaji wa binadamu kimwili na kiakili kwa kuvuruga ufanisi wa utendaji wa ubongo. Huathiri mawazo ya mtu ,kumbukumbu, hisia na tabia, matokeo yake unaweza kuishi kwa maisha ya mahangaiko katika maisha ya kila siku.

Ujonjwa huu ambao pia hauna matibabu, umechukuliwa na baadhi ya watu kama hali ya kawaida kwa kiasi fulani. Unakadiriwa kuwaathiri watu 221 kati ya watu 100,000.

Asilimia ndogo ya wagonjwa, wanaweza kupona schizophrenia kabisa. Lakini hakuna tiba ya kwa sababu hakuna njia ya kujua iwapo ugonjwa huu umepona kabisa au unaweza kumpata tena mgonjwa. Watu wanaohisi kuwa dalili za ugonjwa huu wanashauriwa kutembelea kliniki za za magonjwa ya akili ili kupata ushauri unaoweza kuwasaidia kuepuka kufikiria kuwa wanahukumiwa bila makosa au kuhisi wameaibika.

Ugonjwa wa Creutzfeldt-Jakob

d

Chanzo cha picha, SPL

Maelezo ya picha, Kipimo cha mkojo kinaweza kubaini ugonjwa wa Creutzfeldt-Jakob

Ugonjwa wa Creutzfeldt-Jakob,unaojulikana pia kama CJD, ni ugonjwa wa ubongo wa nadra ambao unaoathiri akili. Ni ya mojawapo ya hali inayowapata binadamu na wanyama inayojulikana kama matatizo ya prion.

Dalili za ugonjwa wa Creutzfeldt-Jakob zinaweza kufanana na zile za ugonjwa wa ubongo wa Alzheimer. Lakini ugonjwa wa Creutzfeldt-Jakob kwa kawaida huwa mbaya zaidi na kusababisha kifo.

Aina zote za CID ni mbaya lakini ni nadra sana. Karibu kisa 1 hadi 2 vya hugunduliwa kati ya watu milioni moja duniani kila mwaka, kulingana na taasisi ya tiba ya Mayo Clinic. Ugonjwa huu mara nyingi huwaathiri watu wazima.

Miongoni mwa dalili zake ni pamoja na kupoteza fahamu na kukosa usingizi.

Ugonjwa wa Creutzfeldt-Jakob na hali zinazohusiana nao zinaonekana kusababishwa na mabadiliko ya aina ya protini zinazoitwa prion.

Protini hizi kwa kawaida huzalishwa katika mwili. Lakini zinapokutana na protini za prion zenye maambukizi , hujikunja na kuwa na sura nyingine ambayo sio ya kawaida. Zinapoenea huweza kuathiri ufanisi wa utendaji wa mwili.

Ugonjwa huu hauna tiba kwani unaweza kujitokeza bila sababu yoyote au pale muathiriwa anapokuwa amerithi jeni zenye marathi hayo kutoka kwa familia. Lakini wataalamu wanasema sababu ya urithishwaji wa jeni za kifamilia ni kwa kiwango cha 15% pekee.

Ugonjwa wa Morgellons

g

Chanzo cha picha, Dermatology Nurses' Association

Ugonjwa huu ni wa ajabu, ambao umezuka hivi karibuni.

Wanaugua ugonjwa huu hutokwa na vidonda kwenye ngozi na wengi wao huwa na imani kwamba ngozi yao imepata maambukizi kutoka kwa wadudu.

Hali hiyo si ya kawaida na chanzo chake huwa hakielewi kikamilifu. Vipimo vya maambukizi ya bakteria au vimelea kwa kawaida huwa ni hasi.

Wagonjwa kwa ujumla huwa na dalili kama vile upele wa ngozi, hisia ya muwasho mkali, huhisi kama kuna wadudu wanaotambaa chini ya ngozi na uchovu.

Hakuna tiba moja ambayo imepatikana ya ugonjwa wa Morgellons, lakini ufuatiliaji wa mara kwa mara na daktari pamoja na matibabu ya hali yoyote inayohusiana kama vile wasiwasi au msongo wa yanaweza kusaidia.