Endometriosis ilimhangaisha kila mwezi - na kumuua akiwa na umri wa miaka 38
Na Basilioh Rukanga ,
BBC News, Nairobi

Chanzo cha picha, Nation Media Group
Mary Njambi Koikai, anayejulikana zaidi kama Jahmby Koikai, alitumia muda mwingi wa maisha yake mafupi kuwaambia Wakenya wenzake kuhusu hali mbaya ya endometriosis, iliyosababisha kifo chake wiki hii akiwa na umri wa miaka 38 pekee.
Kama mtangazaji maarufu wa redio na DJ wa reggae, alikuwa na jukwaa bora.
Kwa ujasiri, alishiriki matatizo yake, mara nyingi akiwataka wale walio na mamlaka kuwajibika, akidai huduma bora za afya kwa wanawake, hasa wale wanaosumbuliwa na ugonjwa wa hedhi.
"Watu walitambua mateso yake, na maumivu yake," mwanaharakati mwenzake Doris Murimi aliambia BBC.
Kuanzia umri mdogo wa miaka 13, alipata mateso ya kila mwezi - maumivu makali ambayo yalikuja na mzunguko wake wa hedhi.
Walakini, ilichukua miaka 17 kujua haswa alikuwa akiugua nini na kupata utambuzi sahihi wa hali hiyo.
Hiyo ilikuwa kwa sababu ya ukosefu wa vifaa vya ndani vilivyo bora katika matibabu ya endometriosis.
Endometriosis ni ugonjwa wa uzazi unaohusishwa na hedhi ambapo tishu zinazofanana na ukuta wa tumbo la uzazi hukua katika maeneo mengine ya mwili, ikiwa ni pamoja na mirija ya uzazi, mfupa wa nynga /pelvis, utumbo, nakatika sehemu za uke .
Endometriosis haizingatiwi kuwa hatari, lakini katika hali nadra inaweza kusababisha shida zinazohatarisha maisha.
Dalili ni pamoja na maumivu makali hadi ya kudhoofisha mwili mara nyingi katika eneo la mfupa wa nyonga / pelvic, uchovu, na hedhi nzito.
Katika hali nadra, inaweza pia kuonekana katika sehemu zingine za mwili ikiwa ni pamoja na mapafu, ubongo, na ngozi.
Kisa cha Bi Koikai kilikuwa mojawapo ya visa hivyo vilivyokithiri, huku hali yake ikizidi kuwa mbaya kadiri miaka inavyosonga, haswa viungo vyake vya uzazi vikizidi kukomaa.
Iliathiri masomo yake, mahusiano, kazi na mambo mengine mengi ya maisha yake.
Alisimulia BBC mnamo 2020 kwamba wakati fulani akiwa chuo kikuu, alifanya mtihani lakini hakuweza kuandika chochote kwa sababu ya maumivu. Ilibidi arudie miaka kadhaa, akichelewesha kuhitimu.
Mnamo 2015, mapafu yake yalipata matatizo kutokana na kwa endometriosis ya thoracic, udhihirisho wa nadra wa ugonjwa huo. Hali hiyo ingejirudia katika miezi na miaka iliyofuata, mara nyingi ikihitaji upasuaji maalum.
Mojawapo ya picha za kudumu za Bi Koikai ni akiwa katika kitanda cha hospitali huku sehemu ya juu ya mwili wake akiwa amefungwa bandeji nyingi, na mirija mingi upande wa kulia wa kifua.
Hii ilikuwa mnamo 2018, wakati mapafu yake yalipofeli na kuhitaji upasuaji.
Alikuwa amelazwa katika hospitali maalumu nchini Marekani na alikuwa akichangisha fedha kwa ajili ya matibabu hayo ya gharama kubwa.
Alikuwa dhaifu na mwenye maumivu makali. "Sitaelezea uchungu kwa sababu sina maneno yanayolingana na yale ambayo nimepitia," alisema wakati huo.
Hali hiyo ilikuwa imeharibu mwili wake. Katika hospitali ya Marekani, tishu zilizokua kwa sababu ya endometriosis zilitolewa kutoka kwa uterasi, sehemu za matumbo na ovari.
Changamoto kubwa zaidi, alisema, ilikuwa mapafu yake.
Ilikuwa imeenea sana, kwa sababu ya jinsi ilivyokuwa imeshughulikiwa nyumbani hapo awali kwamba daktari wa upasuaji huko Marekani hakuweza "kuamini yote yaliyofanywa".
Licha ya makovu yake mengi, bado alikuwa akitabasamu.

Chanzo cha picha, Jahmby Koikai
“Makovu makubwa. Kovu bichi." Alipoeleza, "kila kovu lilisimulia hadithi. Ninaona yote ambayo nimepambana nayo. Kihisia. Kiakili. Kimwili."
Hata hivyo alichagua kupambana na hali yake kwa ujasiri, huku akitoa ufahamu wa wazi kuhusu hali hiyo.
Bi Koikai alizaliwa mwaka wa 1986 viungani mwa mji mkuu, Nairobi.
Alilelewa na mama na nyanya yake , ambao walimfundisha kuwa mvumilivu na jasiri katika kila hali ya maisha.
Alikuwa akitaka kuwa mtangazaji tangu utotoni
Licha ya hali yake, alifanikiwa kumaliza masomo yake ya chuo kikuu na kuwa mtangazaji maarufu wa redio na DJ wa reggae - anayejulikana pia kama Fyah Mummah kwa mashabiki wake.
Inawezekana kwamba watu wengi nchini Kenya walipata kujua hali hiyo kwa sababu yake.
Mambo manne kuhusu endometriosis:
- Inaathiri takriban 10% ya wanawake na wasichana wa umri wa kuzaa ulimwenguni
- Ni ugonjwa sugu unaoambatana na maumivu makali na ya kuathiri maisha hasa wakati wa hedhi, kujamiiana na kupata haja kubwa.
- Haina tiba inayojulikana na matibabu kwa kawaida hulenga kudhibiti dalili
- Ingawa utambuzi wa mapema na matibabu madhubuti ya endometriosis ni muhimu, hii mara nyingi ni changamoto au nadra sana katika nchi za kipato cha chini na cha kati
Doris Murimi, mwanzilishi wa shirika lisilo la kiserikali la Endo Sisters East Africa ambalo hufahamisha watu kuhusu hali hiyo, alikuwa mmoja wa walioshiriki katika moja ya majukwaa katika kituo kimoja cha runinga wakati Bi Koikai aliposimulia hadharani masaibu yake kwa mara ya kwanza.
Alisema hadi wakati huo, watu wengi hawakuonekana kuelewa endometriosis, hata wakati shirika lake lilipoenda kutoa mafunzo na kuzungumza na watu.
Baada ya hapo, "siku zote alikuwa mtu wa kutegemewa kuhusu hali hiyo, kwa hivyo kimsingi alikuwa sura ya ufahamu wa ugonjwa wa endometriosis katika nchi hii", Bi Murimi aliambia BBC.
Endometriosis huathiri takriban 10% (milioni 190) ya wanawake na wasichana walio katika umri wa kuzaa ulimwenguni, kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO).
Hakuna tiba inayojulikana, kwa hivyo matibabu ni kawaida tu kudhibiti dalili.
Lakini Bi Koikai alikiri kwamba "changamoto kubwa" kwa watu walio na endometriosis ilikuwa "utambuzi usio sahihi na hii inasababisha upasuaji usiofaa, dawa zisizo sahihi".
Ndivyo alivyokuwa amepitia, alisema, huku madaktari wakilazimika kukabiliana na uharibifu uliosababishwa na utambuzi mbaya kabla ya kudhibiti ugonjwa huo.
Alikaa takriban miaka miwili Marekani huku madaktari wakimtibu.
Kisha kwa miaka iliyofuata, aliandika yote aliyoyapitia,na kuwafanya watu wengi kujihusisha na kutambua hali hiyo.
Bi Murimi anaamini kwamba kwa kuishi na kusimulia hadithi yake, Bi Koikai alikuwa amesababisha nchi kuelewa jambo hilo gumu kueleweka.
Watu wengine wengi wametoa pongezi kwa nguvu zake katika kutetea wanawake wanaougua endometriosis.
Mcheshi Senje, ambaye pia ana ugonjwa huo, anasema kutiwa moyo na Bi Koikai ni muhimu sana katika mapambano yake mwenyewe.
“Ulinipa nguvu kila nilipohisi kukata tamaa, nilikutazama kwa sababu niliamini kama ungefanikiwa basi mimi pia ningefaulu .. Moyo wangu umevunjika,” alisema mchekeshaji huyo ambaye jina lake halisi ni Sylvia Savai.
Dennis Itumbi, mtaalamu wa mikakati katika muungano unaotawala Kenya, alibainisha juhudi za Bi Koikai za kuhamasisha watu hadi siku zake za mwisho.
"Katika siku zako za mwisho, ulisukuma uelewa na kuongeza ufahamu kuhusu shida ambayo wasichana wengi wanakabiliana nayo -thoracic endometriosis . Uliaga dunia ukinielimisha na kunitia moyo,” aliandika.
Mnamo Mei 20, aliandika chapisho lake la mwisho kwenye Instagram aliloelekeza kwa Rais William Ruto, akitaka upatikanaji bora wa afya "kwa mamilioni ya wanawake wanaopambana na endometriosis kimya kimya".
Alifariki wiki mbili baadaye katika hospitali ya Nairobi kutokana na matatizo yaliyohusishwa na hali hiyo.
Mwishowe, maisha yake, mapambano yake na kampeni zilileta tofauti.
"Mengi yamebadilika, kwa sababu ya Koikai," alisema Bi Murimi, akibainisha kuwa tangu mwaka jana, kulikuwa na "kituo cha endometriosis…na tuna wataalamu kama wawili au watatu".
Lakini mapambano ya kukabiliana na matatizo ya hedhi yataendelea, alisema.
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah