'Nilitaka tu kuwa na nyumba na kulipa madeni, nikaamua kuuza figo yangu'

myanmar

"Nilitaka tu kuwa na nyumba yangu mwenyewe na kulipa madeni yangu ndiyo sababu nilamua kuuza figo yangu," anasema Zeya, mfanyakazi wa shamba nchini Myanmar.

Bei zilikuwa zimepanda baada ya mapinduzi ya kijeshi mwaka 2021 kusababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe. Alikuwa hawezi kumudu chakula cha familia yake changa na alikuwa na madeni makubwa.

Wote waliishi katika nyumba ya mama mkwe wake, katika kijiji chenye nyumba za nyasi kando ya barabara za vumbi, saa chache kwa gari kutoka jiji kubwa zaidi nchini humo, Yangon.

Zeya, ambaye jina lake limebadilishwa ili kulinda utambulisho wake, alijua watu wa eneo hilo waliokuwa wameuza figo zao. "Walionekana kuwa na afya kwangu," anasema. Hivyo akaanza kuuliza maswali.

Yeye ni mmoja wa watu wanane katika eneo hilo walioliambia BBC Burmese kwamba waliuza figo zao kwa kusafiri hadi India.

Mpango wa biashara hiyo

Ununuzi au uuzaji wa viungo vya binadamu ni kinyume cha sheria nchini Myanmar na India, lakini Zeya anasema alimpata mtu anayemwita "dalali".

Anasema mtu huyo alipanga vipimo vya kitabibu, na wiki chache baadaye, akamwambia kwamba mpokeaji wa figo ambaye ni mwanamke wa Kiburma amepatikana, na kwamba wote wawili wangeweza kusafiri hadi India kwa ajili ya upasuaji.

Nchini India, ikiwa mtoaji na mpokeaji si ndugu wa karibu, lazima waonyeshe kwamba nia yao ni ya kiutu na kueleza uhusiano wao.

Zeya anasema dalali huyo alighushi nyaraka, ikiwemo hati ambayo kila kaya nchini Myanmar lazima iwe nayo, inayoeleza maelezo ya wanakaya.

"Dalali aliweka jina langu kwenye sehemu ya familia ya mpokeaji," anaeleza.

Anasema dalali alifanya ionekane kama alikuwa anatoa figo kwa mtu wa karibu.

myanmar

Kisha, anasema, dalali alimpeleka kukutana na mpokeaji huko Yangon. Huko, anasema, mwanamume aliyemtambulisha kama daktari alikamilisha makaratasi zaidi na kumwonya Zeya kwamba angehitajika kulipa kiasi kikubwa cha pesa ikiwa angebadilisha mawazo.

BBC iliwasiliana na mtu huyu baadaye, ambaye alisema jukumu lake lilikuwa tu kuangalia kama mgonjwa alikuwa katika hali nzuri ya kufanyiwa upasuaji, si kuthibitisha uhusiano kati ya mtoaji na mpokeaji.

Zeya anasema aliambiwa kwamba angepokea kyat milioni 7.5 za Myanmar ni kama dola $1,700 na $2,700 katika miaka ya hivi karibuni, kiwango cha ubadilishaji kisicho rasmi kimekuwa kikibadilika tangu mapinduzi hayo.

Anasema alisafiri kwa ndege hadi kaskazini mwa India kwa ajili ya upasuaji, ambao ulifanyika katika hospitali kubwa.

Upandikizaji wote wa viungo vinavyohusisha raia wa kigeni nchini India lazima upitishwe na jopo linaloitwa kamati ya idhini, ambalo huanzishwa na hospitali au serikali ya eneo husika.

Zeya anasema alihojiwa na watu wapatao wanne kupitia mtu aliyekuwa anatafsiri.

"Waliuliza kama nilikuwa ninatoa figo yangu kwa hiari, bila kulazimishwa," anasema.

Anasema alieleza kuwa mpokeaji alikuwa jamaa yake na upasuaji huo ukaruhusiwa.

Zeya anakumbuka madaktari wakimpa dawa ya usingizi kabla ya kupoteza fahamu.

"Hakukuwa na matatizo makubwa baada ya upasuaji, isipokuwa sikuweza kutembea bila maumivu," anasema, akiongeza kuwa alikaa hospitalini kwa wiki moja baada ya upasuaji huyo.

Mzazi 'feki'

Mtoaji mwingine wa figo, Myo Win, pia si jina lake halisi – aliambia BBC kwamba naye alijifanya kuwa ndugu wa wa mgeni.

"Dalali alinipa kipande cha karatasi, na ilibidi nikariri kilichoandikwa," anasema, akiongeza kuwa aliambiwa aseme kuwa mpokeaji alikuwa ameolewa na mmoja wa jamaa zake.

"Mtu aliyekuwa anashughulikia kesi yangu pia alipiga simu kwa mama yangu, lakini dalali alimpanga mama 'feki' akapokea simu hiyo," anasema. Anaongeza kuwa mtu aliyepokea simu hiyo alithibitisha kwamba alikuwa akitoa figo yake kwa jamaa kwa ridhaa yake.

Myo Win anasema aliahidiwa kiasi sawa cha pesa kama Zeya, lakini kiliwasilishwa kama "mchango wa hisani," na ilibidi amlipe dalali takriban 10% ya kiasi hicho.

Wanaume hao wawili wanasema walipokea theluthi moja ya pesa hizo kabla ya upasuaji. Myo Win anasema hili lilikuwa akilini mwake alipokuwa akiingia katika chumba cha upasuaji.

"Nilijiambia kwamba ilibidi nifanye hivyo kwa sababu tayari nilikuwa nimechukua pesa zao."

Anaongeza kuwa "alichagua njia hii" kwa sababu alikuwa akihangaika kulipa madeni na bili za matibabu za mke wake.

Ukosefu wa ajira na umasikini

myanmar
Maelezo ya picha, Mapinduzi ya mwaka 2011, yameleta athari nyingi za kiuchumi nchini Myanmar

Viwango vya ukosefu wa ajira vimepanda nchini Myanmar tangu mapinduzi yafanyike. Vita vimeharibu uchumi na kuwafanya wawekezaji wa kigeni kukimbia. Mnamo 2017, robo ya watu walikuwa wakiishi katika umaskini, lakini kufikia mwaka 2023, idadi hiyo ilikuwa imeongezeka hadi nusu, kulingana na shirika la maendeleo la Umoja wa Mataifa, UNDP. Kukosa ajira na kuwa katika dimbwi la umasikini ndio chanzo cha wengi kuuza figo zao.

Myo Win anasema dalali hakumwambia kwamba kuuza figo ni kinyume cha sheria.

"Singefanya hivyo kama angeniambia. Ninaogopa kuishia gerezani," anasema.

BBC haikutaja mashirika au watu waliokuwa sehemu ya mpango huu ili kulinda utambulisho na usalama wa waliohojiwa.

Hata hivyo, mwanamume mwingine nchini Myanmar, ambaye pia alizungumza kwa faragha, aliambia BBC kwamba alikuwa amesaidia takriban watu 10 kununua au kuuza figo zao kupitia upasuaji nchini India.

Imetafsiriwa na Yusuph Mazimu na kuhaririwa na Ambia Hirsi