Magonjwa hatari zaidi ya zinaa na jinsi yanavyotibiwa

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Abdalla Seif Dzungu
- Nafasi, BBC Swahili
- Twitter,
- Akiripoti kutoka Nairobi Kenya
Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), Maambukizi ya Zinaa (STIs) ni tatizo kubwa la afya duniani, huku zaidi ya kesi milioni moja za magonjwa ya zinaa yanayotibika zikipatikana kila siku.
Maambukizi haya ambayo huenezwa kwa njia ya kujamiiana, kupitia uke, sehemu ya nyuma, na ngono ya mdomo yanaweza kusababisha matatizo makubwa ya kiafya.
Ifuatayo ni orodha ya magonjwa matano ya magonjwa ya zinaa hatari zaidi na jinsi yanavyotibiwa.
ONYO: Taarifa hii ni kwa madhumuni ya habari tu. Kwa ushauri wa matibabu au uchunguzi, wasiliana na mtaalamu.
1. HIV/AIDS
UKIMWI ni ugonjwa sugu wa mfumo wa kinga unaosababishwa na virusi vya ukimwi (VVU).
Kulingana na WHO, VVU huharibu mfumo wa kinga na huingilia uwezo wa mwili wa kupambana na maambukizi na magonjwa.
VVU vinaweza kuambukizwa kwa kugusa damu iliyoambukizwa, shahawa, au maji maji ya ukeni. Hakuna tiba ya VVU/UKIMWI, lakini dawa zinaweza kudhibiti maambukizi na kuzuia kuendelea kwa maradhi.
Baadhi ya watu wenye VVU hupata dalili kama za mafua wiki 2 hadi 4 baada ya kupata virusi. Watu wanaotumia dawa za VVU wanaweza wasiwe na dalili nyingine kwa miaka.
Virusi huongezeka na kuharibu seli za kinga, dalili zinaweza kutokea kama vile homa, uchovu, na nodi za lymph kuvimba.
Bila kutibiwa, VVU kwa kawaida hubadilika na kuwa UKIMWI katika takriban miaka 8 hadi 10, na hivyo kuufanya mwili kuwa katika hatari ya kuambukizwa magonjwa yanayonyemelea.
Tiba
Hakuna tiba ya VVU/UKIMWI, lakini dawa zinaweza kudhibiti VVU na kuzuia kuendelea kwa ugonjwa. Kupitia matibabu, watu wengi wenye VVU nchini Marekani hawapati UKIMWI.
2. Homa ya Ini (Hepatitis B na C)
Hepatitis B na C ni magonjwa ya virusi ambayo husababisha kuvimba kwa ini. Yote husambazwa kupitia damu, lakini hepatitis B pia inaweza kuenea kupitia majimaji mengine ya mwili kama shahawa.
Magonjwa yote mawili yanaweza kusababisha maambukizo ya papo hapo (ya muda mfupi) au sugu (ya muda mrefu). Hepatitis B na C sugu zinaweza kusababisha shida kubwa za ini kama kile maradhi ya cirrhosis na saratani ya ini.
Maradhi hayo pia yanaweza kuenezwa kutoka kwa mama hadi kwa mtoto wakati wa kuzaliwa, kwa njia ya kujamiiana, na kwa kutumia sindano moja au vifaa vingine vya kudunga dawa za kulevya kwa zaidi ya mtu mmoja.
Tiba
Hakuna tiba ya hepatitis B ya muda mrefu, lakini dawa za kuzuia virusi zinaweza kusaidia kudhibiti maambukizi na kupunguza hatari ya uharibifu wa ini.
Chanjo inapatikana na inapendekezwa ili kuzuia maambukizi ya hepatitis B.

Chanzo cha picha, Getty Images
3. Herpes {Malengelenge}
Virusi vya Herpes simplex (HSV) ni maambukizi ya virusi ambayo husababisha vidonda kwenye sehemu za siri au mdomo.
Ni maambukizi ya kawaida ambayo yanaweza kusababisha malengelenge yenye uchungu au vidonda. Kimsingi huenea kwa kugusa ngozi hadi ngozi.
Kuna aina mbili za virusi vya herpes simplex.
Aina ya 1 (HSV-1) mara nyingi huenea kwa mguso wa mdomo na kusababisha maambukizo ndani au karibu na mdomo (malengelenge ya mdomo au vidonda vya baridi).
Inaweza pia kusababisha malengelenge ya sehemu za siri. Watu wazima wengi wameambukizwa na HSV-1.
Aina ya 2 (HSV-2) huenea kwa kujamiiana na husababisha malengelenge sehemu za siri.
Tiba
Kulingana na shirika la Afya Duniani WHO, dawa mara nyingi hutumiwa kutibu dalili za kwanza au za mara kwa mara (milipuko) ya herpes.
Hatua hiyo inaweza kupunguza muda wa dalili na makali ya maradhi hayo lakini haiwezi kuponya maambukizi.
Matibabu ya dalili zinazojirudia huwa na ufanisi zaidi yanapoanza ndani ya saa 48 baada ya dalili hizo kuanza.
Dawa za kuzuia virusi zinazotolewa kwa kawaida ni pamoja na acyclovir, famciclovir na valacyclovir.
Kuchukua kipimo cha chini cha mojawapo ya dawa hizi kila siku (matibabu ya kukandamiza) pia kunaweza kupunguza mara dalili zinapojitokeza.
Kulingana na WHO matibabu ya kila siku mara nyingi hupendekezwa kwa watu ambao hupata uchungu mwingi au ya mara kwa mara au ambao wanataka kupunguza hatari ya kusambaza maradhi hayo kwa mtu mwingine.
Dawa zinazotumiwa kupunguza maumivu yanayohusiana na vidonda ni pamoja na paracetamol (acetaminophen), naproxen au ibuprofen. Dawa zinazoweza kutumika kutibu eneo lililoathiriwa ni pamoja na benzocaine na lidocaine.
4. Kaswende
Kaswende ni maambukizo ya bakteria ambayo yanaweza kusababisha vidonda kwenye sehemu za siri, au mdomo, na pia yanaweza kuenea katika sehemu nyingine za mwili ikiwa haitatibiwa.
Ugonjwa huu ni ugonjwa unaozuilika na unaotibika wa magonjwa ya zinaa (STI). Ikiwa haijatibiwa, inaweza kusababisha shida kubwa za kiafya.
Watu wengi wenye kaswende hawana dalili au hawazitambui.
Kaswende wakati wa ujauzito inaweza kusababisha kuzaliwa mfu, vifo vya watoto wachanga na watoto kuzaliwa na kaswende (ya mazazi).
Matumizi sahihi na ya mara kwa mara ya kondomu wakati wa kujamiiana yanaweza kuzuia kaswende.
Vipimo vya haraka vinaweza kutoa matokeo kwa dakika chache, ambayo inaruhusu kuanza kwa matibabu mtu anapotembelea kituo cha afya.
Tiba
Kaswende ina tiba. Watu wanaoshuku kuwa wanaweza kuwa na kaswende wanapaswa kuzungumza na mtoaji wao wa huduma ya afya.
Hatua ya mapema ya kaswende inatibiwa kwa sindano ya benzathine penicillin (BPG).
BPG ni matibabu ya mstari wa kwanza kwa kaswende na tiba pekee inayopendekezwa na WHO kwa wanawake wajawazito walio na kaswende.
Kama matibabu ya mstari wa pili, madaktari wanaweza pia kutumia doxycycline, ceftriaxone au azithromycin, ambazo ni dawa za antibiotiki.
BPG pia hutumiwa kutibu hatua za baadaye za kaswende, lakini dozi zaidi zinahitajika. Dozi kawaida hutolewa mara moja kwa wiki kwa wiki tatu mfululizo, ikiwa ni pamoja na wakati ambapo ni vigumu kutambua hatua za maambukizi.
BPG inaweza kuzuia kaswende kutoka kwa mama hadi kwa mtoto. Watoto waliozaliwa na kaswende (kaswende ya kuzaliwa), au watoto ambao mama yao alikuwa na kaswende ambayo haijatibiwa, wanahitaji kutibiwa mara moja ili kuepuka matatizo makubwa ya afya.

Chanzo cha picha, Getty Images
5. Clamydia
Klamidia ni maradhi ya zinaa (STI) yanayosababishwa na bakteria Chlamydia trachomatis.
Ni maambukizi ya kawaida ambayo yanaweza kutibiwa kwa dawa za antibiotics, lakini yakiachwa bila kutibiwa, yanaweza kusababisha matatizo makubwa ya afya, hasa kwa wanawake.
Ugonjwa huu husambazwa kupitia majimaji ya mwili kama maji ya ukeni na shahawa. Chlamydia mara nyingi haina dalili, hivyo ni vigumu kutambua. Hata hivyo, dalili zinapoonekana, zinaweza kujumuisha kutokwa na majimaji yasiyo ya kawaida katika uke au urethra, maumivu wakati wa kukojoa, na katika baadhi ya matukio, maumivu chini ya tumbo au korodani.
Tiba
Kulingana na WHO, Klamidia ina tiba.
Klamidia isiyo ngumu inatibiwa kwa vidonge vya antibiotiki ikiwa ni pamoja na doxycycline au azithromycin.
Maambukizi ya mara kwa mara yanaweza kutokea ikiwa wenzi wa ngono hawatatibiwa, na ikiwa watu watafanya ngono bila kondomu na mtu ambaye ana maambukizi.
Watoto wachanga walio na maambukizi ya jicho la chlamydial (conjunctivitis) hutibiwa na azithromycin.
Watu wanapaswa kusubiri siku 7 baada ya kunywa dawa kabla ya kufanya ngono au, kama haiwezekani, kutumia mipira ya kondomu kwa usahihi.
Wanapaswa kuwaarifu wapenzi wao ili kupimwa na kutibiwa, ikibidi.
Taarifa hii inatokana na vyanzo vya WHO
Imehaririwa na Yusuph Mazimu