Wachangiaji wa mayai ya uzazi washauriwa wasichangie kwa ajili ya pesa

fc

Chanzo cha picha, Tracey Langford / BBC

Maelezo ya picha, Yasmin Sharman amechangia mayai mara tatu
  • Author, Charlotte Edwards
  • Nafasi, BBC

Fidia ya watoaji wa mayai itaongezeka kwa mara ya kwanza katika kipindi cha muongo mmoja nchini Uingereza, lakini watu hawapaswi kuchangia kwa ajili ya pesa tu, mdhibiti wa uzazi ameonya.

Ni kinyume cha sheria kumlipa mtu kwa mayai yake nchini Uingereza lakini fidia hulipwa ili kulipia gharama. Fidia hiyo itapanda kutoka pauni 750 hadi 986 tarehe 1 Oktoba, ili kuakisi kupanda kwa bei.

Uingereza kwa sasa ina uhaba wa wafadhili wa mayai, hasa kutoka kwa watu weusi na jamii za wachache, anasema mdhibiti huyo.

Yasmin Sharman alihamasishwa kutoa mchango wa mayai kwa mara ya kwanza akiwa na umri wa miaka 18. "Niligundua kuwa kulikuwa na ukosefu wa watu weusi kufadhili mayai na hilo lilinikasirisha na hivyo kunifanya nitake kuchangia."

"Mimi ni mpenzi wa jinsia moja, kwa hivyo nilikuwa na mawazo kichwani mwangu kwamba huenda nikalazimika kupitia njia tofauti kupata watoto," anaeleza.

Akiwa na umri wa miaka 26, Mx Sharman amechangia mara tatu na alipoweka taarifa hizo kwenye TikTok. Maoni mengi yalilenga kuuliza kuhusu fidia kwamba ni kidogo.

"Ukiinua sana kiwango cha pesa ya fidia, kuna hatari watu watachangia mayai kwa sababu ya pesa pekee, jambo ambalo linawaweka watu wa kipato cha chini hatarini," anasema.

Fidia hiyo itapanda kwa mara ya kwanza tangu 2011 kutokana na mfumuko wa bei, ilisema Mamlaka ya Urutubishaji Yai na Mbegu na Kiinitete (HFEA).

"Ni pesa ya kufidia watu kwa wakati wao lakini watu watambue kuwa nchini Uingereza, kuchangia yai ni kitendo cha kujitolea," anasema Clare Ettinghausen, mkurugenzi wa mikakati na ushiriki kutoka HFEA.

Kuchangia kwa ajili ya pesa tu kunapaswa kuja na "onyo la wazi la kiafya" kwani kuna hatari kadhaa, anasema Bi Ettinghausen.

"Sio kwamba hakuna hatari kabisa kabisa. Unapitia kwanza matibabu baada ya mayai kutolewa. Yanaweza kukupa hofu,” anasema.

Wafadhili pia wanafahamishwa kuwa watoto wanaozaliwa kutokana na mayai yao wanaweza kuwasiliana nao mara tu wanapofikisha miaka 18.

Pia unaweza kusoma

Uhaba wa wachangiaji mayai

c

Chanzo cha picha, Tracey Langford / BBC

Maelezo ya picha, Charlotte Holmes anatoa mayai yake kwa mara ya pili

Charlotte Holmes, mwenye umri wa miaka 35, pia anaeleza kupitia mitandao ya kijamii kuhusu kuchangia mayai.

Kwa sasa yuko katika mchakato wa kuchangia kwa mara ya pili kwa wanandoa waliowasiliana naye mtandaoni.

"Ninatoa damu. Nimetoa nywele zangu. Ni kitu cha ziada kwangu kufanya hasa kwa kuwa sitaki watoto," anasema Bi Holmes.

"Mara ya kwanza nilipochangia ilikuwa mwaka jana. Nilichangia kwa Benki ya Mayai ya London na mwaka huu baada ya wanandoa kuwasiliana nami kwenye Instagram, nitawachangia."

Holmes aliiambia BBC hatapokea pesa zozote za ziada kutoka kwa wanandoa hao - atapokea tu fidia ya sasa ya pauni 750 kutoka kliniki.

Kulingana na taarifa kutoka HFEA, mchango wa mayai umesalia kuwa ule ule tangu kupanda kwa fidia 2011 lakini mahitaji ya mayai yameongezeka.

Holmes hafikirii kuwa watu wanapaswa kuchangia kwa madhumuni ya kifedha tu lakini anaamini kuongezeka kwa fidia kunaweza kusaidia kukabiliana na uhaba uliopo wa wafadhili.

Baadhi ya kliniki zinatumai kupanda kwa fidia kutasaidia kukabiliana na uhaba wa wafadhili wa mayai.

cv

Chanzo cha picha, Tracey Langford / BBC

Maelezo ya picha, Belle Brittle anafikiria kuchangia tena

"Kuongeza fidia kwa wafadhili wa mayai nchini Uingereza hadi pauni 986 ni haki kwani inaakinisi muda, juhudi, na hatari za matibabu zinazohusika katika mchango wa mayai na husaidia kukabiliana na uhaba wa wafadhili," anasema Dkt. Thanos Papathanasiou, mtendaji mkuu na mkurugenzi wa matibabu katika kliniki ya uzazi ya Bourn Hall.

"Mchakato wa uchangiaji bado unahitaji dhamira ya kweli ya mtu binafsi, hivyo kuongeza fidia hakuwezi kudhoofisha motisha za kujitolea na uchangiaji wa mayai lakini ni kutambua nia njema ya wafadhili."

Wafadhili wote wa mayai hupewa ushauri na kliniki na wanapaswa kupitia vipimo kadhaa vya matibabu kabla ya kuchangia. Ni lazima uwe na zaidi ya miaka 18 na chini ya miaka 36 ili kuchangia.

Wafadhili walioidhinishwa wanaweza kuchangia hadi mara 10 na zaid ya watoto 10 wanaweza kuzaliwa kutokana na michango ikiwa mayai kadhaa yatatumiwa na familia moja.

"Elewa ukweli kwamba sio jambo unalolifanya mara moja na limeisha," Yasmin Sharman anasema. "Kuna uwezakano baada ya miaka 18, mwanadamu akakutafuta na kuwasiliana nawe."

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah