Zifahamu nchi nane zilizo hatarini zaidi kwa maambukizi ya UKIMWI

Dawa za kudhibiti makali ya virusi zinastahili kutumezwa kila siku - na hatua yoyote ya kuvuruga matibabu inaweza kusababisha madhara makubwa.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Dawa za kudhibiti makali ya virusi zinastahili kutumezwa kila siku - na hatua yoyote ya kuvuruga matibabu inaweza kusababisha madhara makubwa.
  • Author, mariam Mjahid
  • Nafasi, BBC Swahili

Uamuzi wa Serikali ya Trump kusitisha misaada ya kigeni iliyokuwa ikisimamiwa na Shirika la misaada la Marekani USAID imesambaratisha usambazaji na matibabu ya virusi vya VVU kwa nchi nane, ambazo kutakuwa na uhaba wa dawa za kupunguza makali ya virusi hivi, Shirika la Afya duniani WHO yaonya.

Kusambaratika kwa programu za kuzuia na kukabiliana na HIV huenda kukalemaza juhudi zilizoafikiwa ndani ya miaka 20 ,'' Mkurugenzi Mtendaji wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema hayo katika kikao na wanahabari.

Alisema kuwa Shirika hilo lina wasiwasi kwani upungufu wa dawa hizi za VVU utasababisha maambukizi mapya milioni 10 na vifo milioni tatu vilivyochochewa na makali ya VVU.

Juhudi za kukabiliana na magonjwa kama vile VVU, Malaria, Kifua kikuu na Polio zimeathirika pakubwa baada ya Trump kusitisha misaada ya kigeni iliyoelekezwa kwa programu hizo dakika chache baada ya kuingia katika ikulu ya White House.

Kadhalika, Shirika la WHO ambalo linaratibu mtandao wa Maabara ya Surua na Rubella, wenye tovuti zaidi ya 700 duniani kote, pia huenda ukafungwa hivi karibuni.

Haya yanajiri wakati ambapo ugonjwa wa Surua unarejea nchini Marekani.

Marekani ina "jukumu la kuhakikisha kwamba ikiwa itaondoa ufadhili wa moja kwa moja kwa nchi, inafanywa kwa utaratibu na utu unaowaruhusu kutafuta vyanzo mbadala vya ufadhili," Ghebreyesus alisema Jumatatu.

Hebu tuangazie mataifa ambayo yataumia zaidi na uhaba wa dawa za kupunguza makali ya VVU, kama WHO ilivyoainisha na kuzibainisha.

Pia unaweza kusoma:

1.Kenya

Kenya, ikiwa na watu zaidi ya milioni 1.4 wanaoishi na VVU, ni nchi inayopata ufadhili mkubwa kutoka Marekani.

Mashirika yanayopambana na kukabiliana na virusi vya UKIMWI nchini Kenya yalipokea dola milioni 187 mwaka jana 2024.

Ni nchi ambayo hutegemea sana programu zinazofadhiliwa na Marekani kusambaza ARVS.

Usitishaji wa misaada ya kigeni kupitia Shirika la USAID utakuwa tishio katika matibabu ya maelfu ya watu wanaoishi na VVU na huenda ikazidisha sugu dhidi ya dawa za virusi hivyo na kuongeza idadi ya maambukizi mapya.

Mnamo Machi tarehe 4 , takriban vituo vya afya 167 vilifungwa kutokana na upungufu wa ufadhili, na iwapo hakuna mikakati ya haraka itawekwa huenda vituo vya afya 220 vikafungwa ifikapo Mwezi Juni.

Mamlaka chini ya Wizara ya Afya ya Kenya imeanzisha mikakati ya haraka ya kutafuta wafadhili wa programu hizo ili kuepuka janga la afya nchini humo.

Kenya inahitaji shilingi bilioni 5 kufadhili programu za matibabu ndani ya miezi mitatu.

Ikiwa virusi vya HIV haviwezi kutibiwa vinaweza kuwaua asilimia 60 ya watoto katika kipindi cha miaka miwili unusu.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Ikiwa virusi vya HIV haviwezi kutibiwa vinaweza kuwaua asilimia 60 ya watoto katika kipindi cha miaka miwili unusu.

2. Nigeria

Nigeria, taifa lenye watu wengi zaidi barani Afrika, lina zaidi ya watu milioni 1.7 wanaoishi na VVU, na kuifanya kuwa nchi ya tatu yenye mzigo wa VVU Afrika.

Mwaka 2024, Nigeria ilipokea msaada wa dola milioni 220 za UKIMWI kutoka Marekani, na kuifanya kuwa miongoni mwa wanufaika wakubwa wa usaidizi wa kigeni.

Ijapokuwa viwango vya maambukizi vimekuwa vikipungua Nigeria, athari za kufungwa kwa USAID zinaweza kurudisha nyuma mafanikio haya.

"Ikiwa utaondoa mchango huu mkubwa wa serikali ya Marekani, tunatarajia kwamba katika miaka mitano ijayo, kutakuwa na vifo milioni 6.3 vya ziada vinavyohusiana na Ukimwi," Winnie Byanyima, mkuu wa UNAids, aliiambia BBC Africa Daily podcast.

3. Sudan Kusini

Mfumo wa huduma ya afya wa Sudan Kusini tayari ni dhaifu kutokana na migogoro inayoendelea na watu kuyahama makazi yao.

Nchi inategemea sana ufadhili kutoka nje kutoa matibabu ya VVU.

WHO inaonya kwamba kusitishwa kwa misaada ya Marekani kunaweza kusababisha uhaba mkubwa wa ARVs, na hivyo kusababisha ongezeko kubwa la vifo vinavyotokana na VVU ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa.

4. Mali

Mali ni mojawapo ya nchi chache za Afrika ambako maambukizi mapya ya VVU yanaongezeka.

Maambukizi ya VVU miongoni mwa watu muhimu ni kubwa zaidi kuliko wastani wa kitaifa.

Inashangaza, ni asilimia 62 tu ya Wamali wanaoishi na VVU wanajua hali zao, wakati asilimia 56% tu ndio wanatumia ART, na ni asilimia 48% tu wamefanikiwa kupunguza viwango vya virusi mwilini.

Bila ufadhili, huduma ya matibabu inaweza kupungua zaidi, ikirudisha nyuma miaka ya juhudi za kudhibiti VVU.

5.Lesotho

Lesotho ina moja ya viwango vya juu zaidi vya maambukizi ya VVU duniani, ikiwa na mtu mzima mmoja kati ya watano anaishi na virusi hivyo.

Nchi hii pia ina moja ya asilimia kubwa zaidi ya watu wanaopata tiba ya ARV (ART) kwa asilimia 89%, mafanikio makubwa katika udhibiti wa VVU.

Walakini, kusimamishwa kwa msaada wa Marekani kunaweza kuhatarisha matibabu yanayoendelea, na kusababisha dharura ya afya ya umma

6.Burkina Faso

Burkina Faso ina moja ya viwango vya juu zaidi vya maambukizi ya VVU katika Afrika Magharibi, na watu 74,340 walipokea ARV mwaka 2021.

Hata hivyo, nchi imefikia moja tu ya malengo matatu ya kimataifa ya VVU 95-95-95, ambayo inalenga asilimia 95% ya watu kujua hali yao ya VVU, asilimia 95% ya wale waliogunduliwa kwenye matibabu, na asilimia 95% ya wale wanapoke matibabu ya kupuguza kiwango cha virusi vya VVU mwilini.

Kusitishwa kwa msaada wa Marekani kunaweza kusababisha uhaba wa matibabu, na hivyo kuzoretesha hali ya afya kwa maelfu ya wagonjwa.

7.Haiti

Kwa mujibu wa Shirika la UNAIDS, maambukizi ya UKIMWI miongoni mwa watu wazima ni asilimia 1.8%, huku idadi ya wanawake ikiwa ya juu ukilinganisha na wanaume.

Matibabu ya VVU ambayo yamekuwa yakikumbwa na changamoto haswa baada ya wahudumu wa afya kuvamiwa na magenge na kuhamishia vituo vya kupambana virusi hivyo kutoka Port-au-Prince mwaka jana.

Dkt. Jean Ardouin Louis Charles, katibu wa Chama cha Madaktari wa Haiti (AMH), alisema kuwa PEPFAR imekuwa njia ya maisha kwa mwitikio wa VVU/UKIMWI wa Haiti.

Tangu 2023, mpango huo umefadhili zaidi ya asilimia 80% ya programu za afya zinazohusiana na VVU nchini.

Hiyo ndiyo imesaidia juhudi za ushirikiano za nchi hiyo kupunguza kuenea kwa virusi na kukandamiza athari zake kwa walioambukizwa.

"Utawala wa Trump haukupa hata nchi hizi ndogo muda wa kupanga kuondoka," Dkt. Louis Charles alisema.

"Uamuzi huo ulikuwa wa ghafla, bila kuacha muda wa mpito. Hata kama Haiti inaweza kununua dawa zake yenyewe, itachukua muda kupata hifadhi," aliendelea. "Hakuna jibu kwa kile kinachotokea ikiwa kuna uhaba. Litakuwa pigo kubwa."alisema hayaakizungumza na gazeti moja nchini humo Haiti.

8. Ukraine

Takriban raia wa Ukraine 118,444 wanaishi na VVU.

Kutokana na usitishaji wa msaada wa USAID, kuna pengo la ufadhili la dola milioni 1.9 kwa ajili ya kununua dozi 30,000 za ARV za miezi mitatu zinazohitajika ili kuendeleza matibabu hadi mwaka wa 2025.

Wizara ya Afya ya Umma ya Ukraine inaweza kuomba nyongeza ya mgawo wa bajeti ya serikali ili kuziba pengo la ufadhili la USD 1.9 milioni kwa ununuzi wa ARV, ingawa matarajio bado hayana uhakika.

Wasiwasi wa kudhibiti maambukizi mapya ya Virusi vya VVU

HH

Chanzo cha picha, ASHRAF SHAZLY/AFP/Getty Images

Kwa miongo kadhaa, Marekani imekuwa mshirika muhimu zaidi wa afya ya umma barani Afrika.

Hasa kupitia mpango wake wa kimsingi wa kukabiliana na kuenea kwa VVU duniani, ambao ulizinduliwa mwaka 2003. Unaoitwa Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kusaidia Ukimwi (Pepfar), umeokoa maisha zaidi ya milioni 25.

Kulingana na mkuu wa Vituo vya Afrika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC), USAID ilitoa msaada wa $8bn kwa Afrika katika mwaka uliopita.

"Asilimia sabini na tatu walikwenda kwenye huduma za afya," Jean Kaseya aliambia BBC Newsday mwezi uliopita.

Wataalamu wa afya wanaonya kuwa kuchukua nafasi ya ufadhili huu itakuwa vigumu sana.

Serikali za Afrika zimepiga hatua katika kupunguza utegemezi wa misaada. Kenya sasa inafadhili karibu 60% ya mwitikio wake wa VVU. Afrika Kusini inafadhili karibu 80%.

Lakini kwa mataifa mengi ya kipato cha chini, mizigo ya madeni, majanga ya hali ya hewa na misukosuko ya kiuchumi hufanya suala kujitosheleza kuwa changamoto.

Amref Health Africa, mojawapo ya mashirika yasiyo ya kiserikali ya kiafya katika bara hilo, inaonya kwamba bila hatua za haraka, usalama wa afya duniani uko hatarini.

"Hii ingehitaji serikali za Afrika na Afrika CDC kuongeza ufadhili wao wenyewe, jambo ambalo haliwezekani chini ya hali ya sasa ya dhiki ya madeni," Mkurugenzi Mtendaji wake Dkt Githinji Gitahi aliiambia BBC.

"Kwa kuharakisha milipuko ya mabadiliko ya hali ya hewa na migogoro ya binadamu na mazingira, hii ingeacha dunia kuwa tete na isiyo salama - sio tu kwa Afrika lakini kwa kila mtu."

Shirika la misaada la matibabu la Médecins Sans Frontières (MSF) pia limeonya juu ya hatari ya kukatiza matibabu ya VVU.

"Dawa za VVU lazima zinywe kila siku au watu watakuwa katika hatari ya kupata ukinzani au matatizo hatari kiafya," Tom Ellman, kutoka MSF Kusini mwa Afrika, amesema katika taarifa yake.

Ulimwenguni kote mnamo 2023, kulikuwa na vifo 630,000 vinavyohusiana na Ukimwi na maambukizo mapya milioni 1.5.

Athari za Marekani kujiondoa WHO

GG

Chanzo cha picha, Getty Images

Mipango ya Marekani ya kujiondoa kwenye Shirika la Afya Duniani WHO pia imelilazimisha shirika la Umoja wa Mataifa, ambalo kwa kawaida hupokea takribani moja ya tano ya ufadhili wake wa kila mwaka kutoka kwa Marekani, kusimamisha uajiri na kuanzisha upunguzaji wa bajeti.

WHO ilisema Jumatatu kuwa inapanga kupunguza lengo lake la ufadhili kwa shughuli za dharura hadi dola milioni 872 kutoka dola bilioni 1.2 katika kipindi cha bajeti ya 2026-2027.