Waridi wa BBC: ‘Niliwahi kuacha kutumia ARV kisa kushawishiwa kwenda kwenye maombi’

.

Chanzo cha picha, Doreen Odemba

  • Author, Martha Saranga
  • Nafasi, BBC Swahili

“Niliacha dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi (VVU) maarufu ARV kutokana na ushawishi wa ndugu yangu mmoja aliyenipeleka kwenye maombi,” Doreen Odemba anasimulia mkasa uliomkuta alipokenda kwenye maombi akiaminishwa kuwa angepona maambukizi ya virusi vya Ukimwi.

Anasema alipofika kwenye maombi aliambiwa aache dawa kwa kuwa Yesu amemponya.

Hata hivyo, anasema aliacha dawa kwa muda na alipokwenda kupima, bado alikuwa na maambukizi.

Doreen mwenye umri wa miaka 30 sasa, anasema baada ya hapo alipatwa na changamoto ya kiafya, alikumbwa na kiharusi ambacho kilisababisha kushindwa kujihudumia kwa takribani miaka miwili.

”Nilipata kiharusi, nikakonda sana nikawa wa kubebwa, hata ikafikia kujisaidia kwenye nepi kama mtoto’’, anaeleza na kuongeza kuwa,”Hii imenifundisha sana sirudii kuacha dawa, niwasisitize wengine wenye hali kama yangu wasiache dawa kwa kuambiwa kwamba wameponywa.

Alifahamu vipi ameathirika?

Doreen anaeleza kwa huzuni, ”Nakumbuka dada aliyekuwa akifanya kazi za ndani nyumbani kwa mama mkubwa alinitamkia kwa kunikaripia kutokana na utundu wangu wa kitoto ‘Hivi Doreen unajua kuwa wewe una Ukimwi?’…Baada ya hapo nilikwenda kumuuliza mama mkubwa ambaye alinijibu kuwa ni ukweli ndiyo maana unakunywa dawa, na kwamba nilizaliwa na maambukizi hayo,’’anasimulia.

Doreen anasema aliyafahamu hayo akiwa na umri wa miaka 12 na kisha kuanza kutumia dawa za kufubaza VVU mwaka 2004.

Japo haikuwa rahisi kwake, Doreen anasema shuleni tayari ugonjwa huo ulikuwa ukifundishwa haikuwa vigumu kuelewa kuhusu kuwa na virusi vya Ukimwi, japo anadai ilimhuzunisha.

Unaweza pia kusoma
.

Chanzo cha picha, Doreen Odemba

Kwa nini aliamua kuuelezea umma hali yake ya kiafya?

Anasema lengo lake kubwa lilikuwa ni kuisaidia jamii kiujumla kutokomeza unyanyapaa kadhalika kuwapa matumaini wenye hali kama yake kwa kuwaambia kwamba kupata maambukizi si kufa.

”Baadhi ya watu kwenye jamii si waelewa kabisa lakini ukiwa kwenye hali hii bado unaweza kuwa na ndoto vilevile kufurahia maisha,’’anasema Doreen.

Baada ya kueleza kuwa ana hali ile baadhi ya watu walimwambia ‘amechoka kudanga ndo maana amejitangaza, wengine walisema ameumizwa na mapenzi si bure’.

Je lengo lake la kuisaidia jamii kwa kujitangaza limefanikiwa?

Anasema baadhi ya ndugu walimnyanyapaa mwanzoni lakini sasa wengi wanamchukulia kawaida.

” Nakumbuka nilinyimwa fursa ya kupika chakula mahali, baadhi ya watu waliokuwa wakifahamu kuhusu hali yangu walianza kusema pale kuwa nina virusi. Baada ya hapo nilinyimwa kazi ya upishi katika mgahawa mmoja jijini Dar es Salaam,” anafafanua.

Hata hivyo, unyanyapaa haujamkatisha tamaa. Anasema hajachoka kulizungumzia kwenye mitandao ya kijamii ambako anafurahi kukutana na watu wengi wenye hali kama yake ambao kupitia yeye wameongeza kujiamini na kujithamini.

.

Chanzo cha picha, Doreen Odemba

Atamani kuolewa

Anasema suala la mahusiano kwake amelipa umuhimu sana kwa kuwa anatamani kuolewa na mtu ambaye hana maambukizi.

Pia kulingana na uzoefu wake anasema wanaume wasio na maambukizi wanajali afya wanapokuwa katika mahusiano na wanawake wenye maambukizi.

“Unajua mimi nina maambukizi halafu kusema ninataka kuolewa na mwanaume mwenye maambukizi kama mimi, naona hiyo ni kujinyanyapaa, hivyo nitapenda yule asiyekuwa na maambukizi ili kupunguza kujinyanyapaa,”anafafanua.

.

Chanzo cha picha, Doreen Odemba

Malengo yake

Doreen ambaye anajishughulisha na ujasiriamali ili kumudu maisha yake anasema unyanyapaa umezima ndoto za watu wengi wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi.

”Ninatamani kuona jamii ikishirikiana na serikali na taasisi nyingine za kiraia kutoa elimu sahihi ya VVU,” anashauri.

.

Chanzo cha picha, Doreen Odemba

Hali ya maambukizi ikoje duniani

Kwa mujibu wa takwimu za shirika la kimataifa la kupambana na UKIWMI (UNAIDS), asilimia 44 ya maambukizi mapya ya VVU ni pamoja na wanawake na wasichana na kila wiki wanawake vijana na wasichana 4,000 duniani kote huambukizwa VVU, kati yao, 3,100 wapo nchi za Afrika zilizo Kusini mwa jangwa la Sahara.

Imehaririwa na Florian Kaijage