Ziara ya waziri wa mambo ya nje wa Iran nchini Saudi Arabia ina maana gani wakati huu?

h

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia Faisal bin Farhan (kulia) wakati wa mkutano na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi (kushoto) mjini Riyadh, Saudi Arabia, tarehe 09 Oktoba, 2024

Na Reem Al Sheikh

BBC Arabic

Waziri wa mambo ya nje wa Iran Abbas Araghchi ameelekea Saudi Arabia Jumatano, Oktoba 9, kama kituo cha kwanza katika ziara ya Ghuba ambayo pia inajumuisha Qatar.

Kwa mujibu wa wizara ya mambo ya nje ya Iran, lengo la ziara hii ni "kuimarisha uhusiano na nchi jirani, kuhakikisha utulivu na usalama, na kuendeleza ushirikiano wa kiuchumi."

Kwasababu ziara hiyo inakuja wakati kukiwa na mvutano wa kikanda kutokana na vita vinavyoendelea kati ya Israel na Hamas huko Gaza na Hezbollah nchini Lebanon kwa upande mmoja, na kuongezeka kwa mvutano kati ya Israeli na Iran ambao unaweza kuwa vita kamili, ziara hii ni muhimu sana.

Katika ripoti hii, tunapitia vipimo vya kisiasa na kijeshi na matokeo ya ziara ya waziri wa mambo ya nje wa Iran nchini Saudi Arabia, huku kukiwa na matarajio ya kimataifa ya majibu ya Israeli kwa shambulio la kombora la Iran dhidi ya Israeli mapema mwezi Oktoba.

Je, Araqchi anajaribu kufikia nini Riyadh?

Baada ya mazungumzo kati ya waziri wa mambo ya nje wa Iran na mwenzake wa Saudi Arabia Faisal bin Farhan kumalizika, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Esmail Baghaei amesema mawaziri hao wawili wa mambo ya nje walifanya mazungumzo "muhimu na yenye kujenga" kuhusu matukio ya hivi karibuni katika eneo hilo, hasa katika Ukanda wa Gaza na Lebanon, ambapo pande zote mbili zilitoa wito wa kumalizika kwa vita vya Gaza na Lebanon.

Pia walisisitizia umuhimu wa kupeleka misaada ya kibinadamu haraka kwa wakimbizi.

Unaweza pia kusoma:

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Esmail Baghaei alitangaza kupitia jukwaa la X kwamba Araghchi ataizuru Saudi Arabia "kuimarisha juhudi zetu za kidiplomasia na kwa kushirikiana na nchi za eneo hilo."

Je, mataifa ya Ghuba yanaonaje kuongezeka kwa mzozo kati ya Iran na Israel?

Kuhusu ziara hiyo, mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Iran, Imad Abshenas, anasema kuwa Iran "inatoa tawi la mzeituni kwa nchi za kanda hiyo kwa ajili ya amani na usalama." Abshenas ameongeza katika mahojiano yake na BBC kwamba "Ziara ya Araghchi inakuja katika muktadha wa kuratibu mradi wa amani kati ya Waarabu na Iran kuhusu Gaza, Lebanon na eneo lote, na inalenga kuzima moto."

Abshnas anaamini kuwa "nchi za eneo hilo lazima ziungane kuishinikiza Marekani, yenye uwezo wa kuzuia 'wazimu' wa Israeli," alisema.

Akizungumza na BBC, Dkt. Mohammed Al-Harbi, mwanachama wa muungano wa Saudia Arabia wa Sayansi ya Siasa , alisema kuwa mada kuu ya ziara hii ni "kuzuia kuzorota zaidi kwa hali" .

Al-Harbi anasema kuwa "pande zote, ikiwa ni pamoja na Marekani, ziko katika hali ya wasiwasi," na kusisitiza kuwa "Saudi Arabia inataka kupata utulivu katika kanda hiyo kupitia uhusiano wake wa karibu na Marekani na taasisi za kimataifa."

Saudi Arabia: "Hakuna amani na Israel kabla ya hakikisho la suluhisho la mataifa mawili"

Mwandishi wa Saudi Arabia na mchambuzi wa masuala ya kisiasa Suleiman Al-Aqili hapingi uwezekano kwamba "Araghchi ataiomba Riyadh kuweka shinikizo kwa Washington ili kuzuia kuongezeka kwa mashambulizi ya Israel, kwa kuwa Saudi Arabia, ambayo ina uzito wa kisiasa, ilikuwa na ushawishi mkubwa katika kukomesha vita vya mwaka 2006 na uvamizi wa Israel nchini Lebanon mwaka 1982."

h

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu

"Umoja wa kikanda dhidi ya Israeli"

Kabla ya kuelekea Saudi Arabia, waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alitangaza juhudi za nchi yake za "kuunda harakati za pamoja kutoka nchi za kanda hiyo ili kukomesha mashambulizi ya kikatili nchini Lebanon."

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa Imad Abshnas anatoa maoni yake kuhusu suala hili, akisema, "Tatizo kubwa katika eneo hili ni mgawanyiko wa maoni miongoni mwa nchi zake.

Ikiwa maoni yataunganishwa, kuna matumaini ya kufikia suluhisho la kidiplomasia. vinginevyo, vita vya kina vitamchoma kila mtu."

Hani Suleiman, mtaalamu wa masuala ya Iran na mahusiano ya kimataifa, anajibu kwa kusema, "Iran haikutafuta kuunda muungano wakati wa utulivu, na sasa inataka kuonyesha picha nje kana kwamba inaungwa mkono na Waarabu katika kukabiliana na Israeli na Marekani. Hii inathibitisha mambo mawili: la kwanza ni kwamba Iran inajaribu kuondokana na hali ngumu kwa njia zote, na ya pili ni kwamba jukumu la Waaeabu lina ufanisi wakati wa migogoro mbalimbali, kwani nchi za Kiarabu zina uwezo wa kurejesha kile Iran inachokifanya."

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Mohammed Al-Harbi, anasema "kukataa kwa Saudi Arabia kuingia katika muungano wowote ulioelekezwa," na kusema kuwa "nchi yake inashiriki tu katika muungano wa baraza la ushirikiano wa Ghuba na muungano wa Kiislamu ulioidhinishwa na nchi 42 za Kiarabu na Kiislamu."

Kulingana na mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Saudi Arabia Suleiman Al-Aqili anaamini kuwa Iran "inatafuta kuishawishi Saudi Arabia kuhamishia jumuiya ya ushirikiano wa kiislamu ili kusimama na mhimili wa upinzani, ambao ni mhimili ambao Saudi Arabia hapo awali iliumizwa nao kabla ya wengine."

Israel na athari zake kwa mataifa ya Ghuba

h

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Makombora ya Israel ya Iron Dome yazuia kombora.

Ziara ya Araghchi inakuja wakati Tehran ikithibitisha "haki yake ya kujibu kwa nguvu shambulio lolote la Israel katika ardhi yake."

Mapema mwezi Oktoba, Iran ilianzisha mashambulizi ya makombora dhidi ya Israel, kujibu mauaji ya katibu mkuu wa Hezbollah Hassan Nasrallah katika shambulio la anga la Israel katika viunga vya kusini mwa Beirut, na mauaji ya mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas Ismail Haniyeh mjini Tehran mwishoni mwa mwezi Julai, katika shambulio lililohusishwa na Israel.

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Iran, Imad Abshenas, anasema: "Iran haitafuti kupigana vita kamili, lakini pia ina uwezo wa kijeshi wa kukabiliana na Israel na Marekani."

Baada ya shambulio la Iran... Israel inaweza kujibu vipi, na Tehran itafanya nini?

Mnamo tarehe 8, Oktoba , Shirika la habari la Reuters lilinukuu chanzo cha juu cha Iran kikisema kuwa "Tehran imeyaambia mataifa ya Ghuba ya Kiarabu kwamba kuruhusu matumizi ya anga au kambi zao za kijeshi kufanya mashambulizi dhidi ya Iran haitakubalika, na kuonya kuwa hatua hiyo itasababisha majibu."

Kauli hizi zilitanguliwa na msimamo wa Ghuba ambao ulitaka kuihakikishia Iran "kwamba mataifa jirani ya Ghuba yatabaki kuwa yasiyoegemea upande wowote katika mzozo wa Iran na Israeli." Hapa Abshanas anatoa maoni yake, akisema, "Kama mataifa ya Kiarabu yanaamini kwamba kutoegemea upande wowote katika mzozo huu kunaweza kuwaondolea hatari ya kujihusisha katika vita pana, basi wanakosea."

Abshenas anasema kuwa Iran "italenga kambi zozote za kijeshi katika eneo lolote ambalo mashambulizi yataanza dhidi yake," na Abshenas hapingi uwezekano kwamba "Iran italenga ndege katika kambi za Marekani katika mataifa ya Ghuba hata kabla ya kuanza safari."

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Saudi Arabia, Suleiman Al-Aqili, anasema kuwa Saudi Arabia "haitajiruhusu kuwa mwanzo au njia ya vita dhidi ya Iran, kwakuwa hakuna kambi kubwa za Marekani nchini humo, isipokuwa kwa timu za mafunzo na matengenezo ndani ya mfumo wa ushirikiano wa nchi mbili."

f

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wapiganaji wakipita kwenye bango la makombora ya masafa marefu ya Iran, na maneno ya Kiarabu "Ahadi ya uaminifu " na maneno ya Kiajemi "Israeli ni dhaifu kuliko mtandao wa spider", katika medani huko Tehran.

Dkt. Muhammad Al-Harbi, mwanachama wa muungano wa Sayansi ya Siasa cha Saudi Arabia, anaamini kwamba "taarifa zozote za onyo kutoka vyanzo vya siri na nje ya wigo wa kauli za rais wa Iran na wizara ya mambo ya jje haziihusu Saudi Arabia," na anasema kuwa Iran sasa iko katika nafasi "ambayo haikubali vitisho, baada ya kupokea mapigo makali kupitia mikono yake katika eneo hilo, ambayo yameanza kuanguka."

Waziri wa ulinzi wa Marekani Lloyd Austin amesisitizia kuhusu ahadi ya nchi yake ya kuilinda Saudi Arabia, akisema katika mazungumzo na mwenzake wa Saudi Arabia, "Uwezo wetu katika eneo hilo unasaidia ulinzi wa washirika wa kikanda wa Marekani, kuwalinda wafanyakazi wa Marekani, na kuzuia uchokozi."

Katika ngazi ya kiuchumi, Al-Harbi anakumbuka athari mbaya kwa mfumo wa kimataifa ikiwa vita vitapanuka, akisema kwamba Iran lazima "iache, kuhakikisha utulivu wa eneo hilo, na kuingia katika tanuru la kiuchumi, hasa kwa kuwa inashika nafasi ya pili katika suala la hifadhi ya gesi asilia, na ni mwanachama wa OPEC Plus."

Uhusiano kati ya Iran na Saudi Arabia unaelekea wapi?

f

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wenye magari wakipitisha magari yao mbele ya ubao wa matangazo unaotangaza makombora ya balistiki ya Iran, linalosema "Ahadi ya Kweli na Imani," na sentensi katika lugha ya Kiajemi inayosema "Israeli ni dhaifu kuliko utando wa buibui," katika moja ya viwanja vya Tehran.

Inaonekana kwamba Iran pia ilitaka ziara ya Araghchi mjini Riyadh kutuma ujumbe kwamba uhusiano wa nchi hizo mbili unasonga mbele katika "muelekeo sahihi."

Alipowasili Riyadh, waziri wa mambo ya nje wa Iran alielezea uhusiano kati ya Iran na Saudi Arabia kama "kukua na kusonga mbele katika mwelekeo mzuri."

Mnamo Oktoba 2, Rais wa Iran Masoud Pezeshkian na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia Faisal bin Farhan walikutana katika mji mkuu wa Qatar, Doha, ambapo Pezeshkian alielezea kwa Prince Faisal "kuridhika kwake na uhusiano unaokua kati ya Iran na Saudi Arabia."

Makubaliano haya ya Iran na faraja yanakuja baada ya miaka saba ya mtengano, ambao ulimalizika kwa mpango wa China ambao ulisababisha maridhiano kati ya Iran na Saudi Arabia mwaka 2023.

Je, kurejea kwa uhusiano kati ya Saudi Arabia na Iran kutamaliza mgogoro wa sasa?

"Marekani na Israel wanafanya kila wawezalo kuvuruga uhusiano kati ya Iran na Saudi Arabia, lakini naamini kuwa sera mpya za serikali zote mbili za Saudi Arabia na Iran zitasababisha kuwepo kwa maelewano makubwa kati ya pande hizo mbili," anasema mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Iran Emad Abshenas.

Dkt. Mohammed Al-Harbi anaamini kuwa uhusiano wa nchi hizo mbili umekuwa mzuri au bora zaidi, na anaeleza kuwa kwa kusema kuwa "tangu wakati wa maridhiano kati ya Saudi Arabia na Iran, nchi za baraza la ushirikiano wa Ghuba hazijashuhudia mvutano wowote kutoka Iran au kupitia silaha zake katika eneo hilo," akimaanisha kundi la Wahouthi la Ansar Allah, ambalo halijazilenga meli za Kiarabu katika bahari ya Shamu tangu Oktoba 7, 2023.

Al-Harbi anaamini kuwa haya yote ni ushahidi wa "uaminifu wa Iran na hamu yake ya uhusiano wa usawa."

Kulingana na mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Saudi Arabia, Mubarak Al-Ati, "Saudi Arabia ina uwezo wa kushikilia kijiti katikati, kwa hivyo haitapoteza mshirika wake wa kimkakati wa Marekani, na wakati huo huo haitapoteza uhusiano wake na Iran; kwa kuzingatia kanuni ya suluhisho la mataifa mawili, ujirani mwema, kutoingilia mambo ya ndani ya nchi, na kukataa matumizi ya nguvu kutatua migogoro."