Mama anayefanya kampeni ya kukusanya faini kumuokoa mwanae dhidi ya hukumu ya kunyongwa Saudia

Stephen Munyakho pichani mwaka 2010, mwaka mmoja kabla ya kukamatwa kwake

Chanzo cha picha, Dorothy Kweyu

  • Author, Waihiga Mwaura
  • Nafasi, BBC Focus on Africa TV, Nairobi

Mama mmoja raia wa Kenya, ambaye ameongoza kampeni ndefu na ngumu ya kumuokoa mwanawe kutoka kwenye adhabu ya kunyongwa nchini Saudi Arabia, alipata ahueni kidogo alipopewa muda wiki hii.

Stephen Munyakho, mwenye umri wa miaka 50, alipaswa kunyongwa siku ya Jumatano kwa mauaji ya raia wa Yemen mwaka 2011.

Hukumu hiyo ingetekelezwa kwa kukata kichwa, kukata kichwa ni njia ya kawaida sana katika ufalme huo au kwa kunyongwa, sindano ya sumu au kwa kutumia kikosi cha kufyatua risasi. .

Lakini kukaa kwake kabla ya kunyongwa ni kwa muda tu, na Dorothy Kweyu, 73, ameiambia BBC kuwa bado hajapewa maelezo zaidi kuhusu kesi ya mtoto wake na Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya.

Wasiwasi wake haujapungua. Bado anajaribu kuchangisha "diyah" au pesa za damu ambazo chini ya mfumo wa sheria wa Kiislamu, unaojulikana kama Sharia, zinaweza kupatia msamaha kutoka kwa familia ya mwathirika.

Saudi Arabia ni dola ya Kiislamu na mfumo wake wa mahakama unategemea Sharia kwa kesi za jinai na za madai.

Rufaa ya umma kufikia sasa imekusanya chini ya 5% ya $1m inayohitajika (£790,000), anasema Bi Kweyu, mwandishi wa habari anayeheshimika nchini Kenya.

Kupata muda zaidi wa kuchangisha pesa hizo huenda kukawa kile ambacho maafisa wa serikali ya Kenya, wakijadiliana kwa niaba ya Bi Kweyu, wanatumai kuwa njia ya kusonga mbele.

Akitangaza kucheleweshwa kwa utekelezaji wa hukumu siku ya Jumatatu, Korir Sing'Oei, afisa mkuu katika wizara ya mambo ya nje, alisema wapatanishi walikuwa wakibuni "mikakati ya kufikia hitimisho linalokubalika zaidi, na haraka zaidi kwa familia zote mbili" .

Bw.Munyakho, anayejulikana kama Stevo kwa marafiki na familia yake, alikwenda kufanya kazi Saudi Arabia akiwa na miaka 20 na miaka 13 iliyopita alikuwa meneja wa ghala katika hoteli ya kitalii ya Red Sea.

Kulingana na Bi Kweyu, mwanawe aligombana na mwenzake, ambaye alisema alimdunga Stevo na kifaa chenye ncha cha kufungulia bahasha.

Stevo alilipiza kisasi kwa kunyakua kifaa hicho na kumvamia mfanyakazi mwenzake na kusababisha kifo chake.

"Hapo awali, mwanangu alipatikana na hatia ya kuua bila kukusudia na akahukumiwa kifungo cha miaka mitano jela," aliiambia BBC.

"Tulitarajia angekuwa ndani kwa miaka miwili na nusu, kwa mujibu wa kanuni za kimataifa, lakini haikuwa hivyo."

"Mahakama iliamuru kwamba mwanangu akabiliwe na adhabu ya kifo, ambayo inamaanisha hukumu ya kifo," Bi Kweyu alisema.

"Baadaye, hata hivyo, familia ya marehemu ilishawishiwa na ujumbe wa Kenya nchini Saudi kuchukua ofa ya diya ya pesa za damu."

Lakini mazungumzo yameonekana kuwa marefu na magumu na kutafuta pesa kwa Stevo, ambaye ana watoto watatu, haikuwa rahisi.

Mahakama iliweka tarehe 15 Mei kuwa tarehe ya mwisho ya kulipwa kwa pesa hizo za damu.

“Siku moja niliuliza: ‘Je, kuna njia ambayo tunaweza kubadilishana, ili waniue mimi badala ya Steve mwanangu?’ Lakini nilikaripiwa na kuambiwa niache kuzungumza hivyo,” Bi Kweyu alisema.

Dorothy Kweyu akiwa amezungukwa mwaka wa 2002 na watoto wake tisa, Stephen Munyakho anaonekana kwenye miwani kwenye safu ya nyuma.

Chanzo cha picha, Dorothy Kweyu

Chini ya sheria ya Kiislamu, diyah humlipa mwathirika au familia yake. Inaweza kulipwa kwa aina mbalimbali za uhalifu kutoka kwa mauaji hadi kuumia na uharibifu wa mali.

Inaweza kusababisha kupunguzwa kwa hukumu na katika hali fulani msamaha. Kwa sasa inatumika katika nchi zipatazo 20 za Mashariki ya Kati na Afrika, zikiwemo Sudan na kaskazini mwa Nigeria.

Quran, kitabu kitakatifu cha Kiislamu, kinaunga mkono ulipaji wa fedha za damu, na hili lilifafanuliwa zaidi na Mtume Muhammad SAW, ambaye alieleza katika mafundisho yake kwamba adhabu kutokana na mauaji inapaswa kuwa ngamia 100.

Ufafanuzi wa sasa unamaanisha kuwa kiasi hiki hutofautiana katika nchi tofauti kwani diyah sasa hulipwa kwa pesa taslimu.

"Nchini Saudi Arabia ngamia mmoja ni wastani wa riyal 30,000 za Saudi [$8,000, £6,300] hivyo kama mtu yeyote atagharamia maisha ya mtu, atalazimika kulipa takribani $80,000," mwanazuoni wa Kiislamu wa Nigeria Sheikh Husseini Zakaria aliiambia BBC.

Mambo mengine, kama vile jinsia na malezi ya kidini ya mwathiriwa, yanaweza pia kuamua kiasi cha pesa za damu zinazodaiwa. Inahitaji pia makubaliano ya mwathirika au familia zao.

Bi Kweyu anasema aliombwa kwanza kulipa takribani $2.6m, lakini akafanikiwa kujadiliana hadi $950,000.

Haijulikani ikiwa Stevo amebadili dini akiwa gerezani. Katika taarifa ya Bw Sing'Oei, iliyochapishwa kwenye X (zamani Twitter), alibainisha kuwa Stephen sasa anajulikana kama "Abdulkareem".

Kubadilika kwa jina hilo ilikuwa habari kwa familia yake, ambao wanaweza kuwasiliana naye mara kwa mara anapowapigia simu kutoka gerezani.

Imekuwa ngumu kwa watoto wake. Mdogo wake, Evans Mwanze mwenye umri wa miaka 23, hajamuona kwa zaidi ya miaka 20.

“Kuna nyakati nina matumaini kwamba baba yangu atakuja nyumbani,” aliniambia.

"Wakati mwingine mimi huvunjika moyo na kujiuliza ikiwa mabaya zaidi yanaweza kutokea. Sikuwahi kumjua baba yangu. Aliondoka nikiwa na umri wa miaka mitatu na hiyo ndiyo ilikuwa mara ya mwisho kumuona.”

Bi Kweyu anasema uwezekano wa kukatwa kichwa ni wa kweli kabisa. Mwaka jana, kulikuwa na watu 172 walionyongwa nchini Saudi Arabia, kulingana na takwimu zilizotolewa na mamlaka.

“Kuna siku mwanangu alinipigia simu na kuniambia kuwa rafiki yake mmoja amekatwa kichwa. Ulikuwa wakati mgumu sana. "

Mamlaka za Saudia hazijajibu ombi la BBC la kuzungumzia suala hilo, lakini serikali ya Kenya imekuwa ikishukuru kwa msaada wao katika kesi hii.

"Tutaendelea kuegemea urafiki wa dhati tulio nao na washirika wetu wa Saudia," Bw Sing'Oei alisema, akiahidi mazungumzo zaidi yatafanyika katika siku zijazo.

"Tutawashirikisha wadau wa Nairobi na Riyadh, ikiwa ni pamoja na wawakilishi kutoka kwa uongozi wetu wa kidini, ili kukubaliana juu ya hatua inayofuata ya haraka."

Imetafsiriwa na Lizzy Masinga.