Ugaidi Msumbiji: Jinsi kujiondoa kwa vikosi SADC kunavyoliacha eneo hilo katika hatari ya wapiganaji wa Kiislamu

Na Ian Wafula

BBC

Wanajeshi kutoka vikosi vya usalama vya Rwanda karibu na eneo la gesi asilia la Afungi nchini Msumbiji mnamo 2021

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Wanajeshi kutoka vikosi vya usalama vya Rwanda

"Kama wangejua mimi ni afisa wa serikali, wangenikata kichwa," Tomas Alberto, mtumishi wa serikali kaskazini mwa Msumbiji, aliiambia BBC.

Anahisi alikuwa na bahati ya kutoroka.

Mwezi uliopita, aliamshwa asubuhi na mapema, Tomas alichungulia nje ya dirisha lake na kuona watu wanne wenye silaha wamesimama nje ya nyumba yake. Aliogopa sana na kukimbilia porini ambako alijificha kwa siku tatu akiishi kwenye mimea ya mihogo.

"Nilikuwa na bahati walinitukana tu nilipokuwa natoroka," alisema.

Mwezi Mei tarehe 10 wakaazi wa Macomia, mji wa jimbo la Cabo Delgado, waliamshwa na milio ya risasi.

Wanamgambo wanaohusishwa na Islamic state walilenga majengo ya serikali katika mji huo kabla ya kupora maduka na maghala. Watu hao wenye silaha walilizingira eneo hilo kwa siku mbili, na kusababisha hali ya hofu na machafuko miongoni mwa wakazi.

Wanamgambo hao walivamia kituo cha matibabu kinachosimamiwa na Médecins Sans Frontières (MSF), na kukamata magari na vifaa vya matibabu. Shirika hilo la misaada limesema halina budi ila kuwahamisha wafanyikazi na kusimamisha shughuli zake huko Macomia.

Alfane Mussa, baba wa watoto watano, aliambia BBC kuwa alizuiliwa na kuhojiwa na wanaume wanane waliokuwa na bunduki.

"Walikuwa wamevalia magwanda ya kijeshi na kubeba silaha hatari," alisema. "Waliniambia nikimbie msituni la sivyo wataniua nikikaa mjini." Mussa alisema ilichukua siku mbili kwa askari wa kikosi cha serikali kufika katika eneo lake, lakini wakati huo wanamgambo hao walikuwa tayari wameondoka.

Zaidi ya watu 700 walitoroka duru hii mapigano, kulingana na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji. Wale waliobaki nyuma, kama Mussa na Alberto, wameachwa bila vifaa vya matibabu, hakuna umeme, na wanaishi kwa hofu ya mara kwa mara ya shambulio jingine.

Pia unaweza kusoma:
Msafara wa vikosi vya usalama vya Rwanda ukishika doria katika eneo la Macomia mnamo Januari 3, 2023.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Idadi ya wanajeshi wa kimataifa waliotumwa inapunguzwa ingawa ghasia zinaendelea

Kuondoka kwa wanajeshi wa kimataifa

Ujumbe wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambao unajumuisha wanajeshi kutoka nchini nane, umesema utaondoa vikosi vyake kutoka Msumbiji ifikapo Julai 15, kwa kuzingatia mkataba wake wa miaka mitatu.

Wataalamu wa usalama wa kikanda wameibua wasiwasi hata hivyo kwamba yote haya yanaweza kutokea mapema mno - kabla eneo halijatulia.

Botswana na Lesotho tayari zimewaondoa wanajeshi wao, huku Angola na Namibia zikiwa katika harakati za kuondoka. Hata hivyo, gazeti la kibinafsi la Zambeze mjini Maputo liliripoti kuwa Tanzania, ambayo inapakana na Msumbiji upande wa kaskazini, itadumisha wanajeshi wake 300.

Dastan Kweka, mtaalamu wa masuala ya utawala mjini Dar-es-Salaam, aliiambia BBC kwamba mamlaka inatarajia usalama katika eneo hilo kuzorota zaidi.

Afrika Kusini, ambayo kwa sasa inachangia zaidi ya wanajeshi 1000 katika juhudi za sasa za kulinda amani imesema itaweka wanajeshi wake nchini Msumbiji hadi mwisho wa 2024, lakini sio kama sehemu ya ujumbe wa SADC.

Jukumu la Rwanda

Mwezi Aprili, Rwanda ilitangaza kutuma wanajeshi 2000 zaidi nchini Msumbiji.

Brigedia Jenerali Ronald Rwivanga, Msemaji wa Jeshi la Rwanda, aliambia BBC kwamba walikuwa 'wakiimarisha' nguvu zao. Uamuzi huo hauhusiani na kujiondoa kwa SADC au mashambulizi ya hivi karibuni, alisema.

Rwanda ilipotuma wanajeshi wake 1000 wa kwanza nchini Msumbiji mwaka 2021 serikali ilisema inalenga kuunga mkono juhudi za kurejesha mamlaka ya serikali ya Msumbiji kupitia operesheni za mapambano na usalama, pamoja na mabadiliko ya sekta ya usalama.

Hatua hii ilifuatia kutiwa saini kwa mikataba kadhaa baina ya nchi hizo mbili mwaka 2018.

Wanajeshi wa ziada wa Rwanda watasaidia kujaza mapengo yaliyoachwa na vikosi vya SADC kaskazini mwa Msumbiji.

Meron Elias, mchambuzi wa Afrika Mashariki na Kusini wa Kundi la Mgogoro alisema ujumbe wa SADC nchini Msumbiji unakabiliwa na matatizo ya kifedha, ukitegemea zaidi michango ya nchi wanachama ili kuendelea kuhudumu.

Alisema kambi ya kikanda badala yake imeelekeza mwelekeo wake kuleta utulivu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Mnamo Desemba 2023, SADC ilipeleka wanajeshi DRC kusaidia serikali kupambana na makundi ya waasi.

Ramani ikionesha eneo la Macomia mjini Cabo Delgado, kaskazini mwa Msumbiji

Ghasia mpya Cabo Delgado

Kundi la Islamic State lisilo na uhusiano na kundi la al-Shabaab nchini Somalia - limekuwa likiendesha shughuli zake huko Cabo Delgado tangu 2017. Wanamgambo wameua mamia ya watu, kuziacha jamii bila makao na kuteketeza miji na vijiji.

Wamekuwa wakipigania udhibiti wa eneo hilo lenye utajiri wa gesi asilia na madini kama vile hidrokaboni, grafiti na rubi. Mnamo Julai 2021, kampuni kubwa ya nishati ya Ufaransa ya Total Energies ililazimika kusimamisha mradi wake wa gesi asilia iliyosafishwa kwa $20 bilioni kufuatia mashambulizi.

Baada ya kutumwa kwa wanajeshi wa SADC na Rwanda mwaka huo huo, mashirika ya misaada na serikali waliripoti kuwa usalama umeimarishwa katika baadhi ya maeneo na maisha ya kawaida yalikuwa yakirejea taratibu.

Lakini kwa bahati mbaya, hatua zilizopigwa zilikuwa za muda mfupi.

Tangu Desemba 2023 mashambulizi yamekuwa yakiongezeka. Zaidi ya watu 110,000 wametoroka makazi yao kulingana na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji.

Tomas Queface, mtafiti katika tovuti ya uchambuzi ya Cabo Ligado inayofuatilia ghasia nchini Msumbiji, alisema wanamgambo hao walifanikiwa kuteka eneo la Macomia kwa muda mrefu kwa kusajili wapiganaji zaidi, wakiwemo watoto katika vikosi vyao.

Ripoti ya Human Rights Watch ilitaja watu wawili kutoka kwa familia moja waliomwona mpwa wao mwenye umri wa miaka 13 akipora pamoja na wanamgambo wakati wa shambulio hilo.

Watu waliohamishwa kutoka mkoa wa Cabo Delgado wanatembea katika mitaa ya Namapa, wilaya ya Erati ya Nampula, Msumbiji mnamo Februari 27, 2024.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Zaidi ya watu 100,000 wamekimbia makazi yao kutokana na mzozo wa Cabo Delgado

Je hatua hii ina maana gani kwa eneo hilo?

Mnamo mwaka wa 2020, wanamgambo kutoka Msumbiji walishambulia vijiji vya mpakani mwa Tanzania, na kuua karibu watu 25, kupora maduka na kuchoma nyumba.

Tangu wakati huo, Tanzania imeimarisha usalama wake kwa kuweka amri ya kutotoka nje katika baadhi ya vijiji vya mpakani, kuongeza doria na kuzuia harakati kati ya nchi hizo mbili.

Dastan Kweka alisema kuwa pamoja na kwamba mkakati huu umefanikiwa umekuwa wa gharama kubwa. Bajeti ya ulinzi ya Tanzania imeongezeka kwa 10% kila mwaka tangu 2021.

Wakati huo huo, kuna wasiwasi kwamba iwapo uasi wa Cabo Delgado utashika kasi zaidi nchi nyingine ambazo zinapakana na majimbo ya kaskazini mwa Msumbiji kama Malawi zinaweza kuathirika kulingana na Meron Elias.

Anasema tayari kuna uhusiano wa kikanda unaoendelea zaidi kati ya al-Shabab nchini Msumbiji na Vikosi vya Ulinzi vya washirika wa ISIS wanaofanya kazi nchini DRC na sehemu za Uganda.

Ugaidi Msumbiji: Wanajeshi wa Tanzania kusalia Msumbiji - Stergomena Tax

Ujumbe wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambao unajumuisha wanajeshi kutoka nchini nane, umesema utaondoa vikosi vyake kutoka Msumbiji ifikapo Julai 15, kwa kuzingatia mkataba wake wa miaka mitatu.

Botswana na Lesotho tayari zimewaondoa wanajeshi wao, huku Angola na Namibia zikiwa katika harakati za kuondoka.

Hata hivyo, gazeti la kibinafsi la Zambeze mjini Maputo liliripoti kuwa Tanzania, ambayo inapakana na Msumbiji upande wa kaskazini, itawabakisha mamia ya wanajeshi wake.

Kutokana na hali hiyo muda mfupi uliopita BBC Swahili imezungumza na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wa Tanzania Stergomena Tax ambaye anaanza kuelezea sababu za Tanzania kubakisha wanajeshi wake.

Kwanini Tanzania inabakiza?

Maelezo ya sauti, Ugaidi Msumbiji: Wanajeshi wa Tanzania kusalia Msumbiji-Stergomena Tax

Imetafsiriwa na Seif Abdalla