ZaaZaa: Sharubati ya parachichi kwa ajili ya kufungulia funga

sd

Chanzo cha picha, Alia Al Kasimi

Maelezo ya picha, Tunda kuu katika ZaaZaa ni parachichi

Juisi nzito ya ZaaZaa ya Morocco ni laini na tamu – hutengenezwa kwa parachichi na inatosheleza kama tiba ya baada ya kufunga wakati wa Ramadhani.

"Katika sehemu nyingi za dunia, watu hufikiria parachichi kuwa tunda chufu na si tamu. Nilipokuwa mtoto, tulikuwa tukikata parachichi katikati, na kunyunyiza sukari juu na kisha kula kwa kijiko," anasema Alia Al Kasimu, mwanzilishi wa shule ya mapishi ya mtandaoni ya Flavors of Morocco na mwandishi wa kitabu: Moroccan Cookies: 20 Recipes You Must Try Before You Die.

Kilimo cha parachichi kilianza Morocco mapema miaka ya 2000, na sasa Morocco ndiyo nchi ya tisa kwa kuuza nje matunda hayo. Al Kasimu anasema parachichi limekuwa tunda maarufu sasa.

ZaaZaa inafanana sana na fruti ya matunda mengine. Juisi hiyo nzito inajumuisha parachichi iliyosagwa na maziwa na matunda yaliyokaushwa, kama zabibu na tende.

Mchanganyiko huo hutiwa ndani ya glasi iliyotiwa shira yenye ladha ya chokoleti au sukari iliyopikwa ama ladha ya stroberi, na juu yake inaweza kuwekewa vipande vya matunda yaliyokatwakatwa kama vile ndizi na kiwi.

"ZaaZaa ina kalori nyingi," Al Kasimu anasema. "Ni nzuri sana na lazima uile kwa kijiko. Juisi hii unaweza kula na lozi, jozi, biskuti, chokoleti - ama chochote unachotaka."

Pia unaweza kusoma
zx

Chanzo cha picha, Alia Al Kasimu

Maelezo ya picha, Alia Al Kasimu ndiye mwanzilishi wa shule ya upishi ya mtandaoni iitwayo Flavors of Morocco

Dave Patera, mtafiti wa vyakula na mtengeneza maudhui ambaye hupika mapishi yenye asili ya jamii yake ya Kaskazini mwa Afrika, anasema.

"ZaaZaa ni chakula pendwa nchini Morocco. Watu wanaipenda sana kuna kipengele cha mjadala kidogo kuhusu Zaazaa: Je, uile na nini? Tunaweza kuiweka kwa kiasi gani kwenye glasi?

Ingawa ZaaZaa inapatikana kwa mwaka mzima, hupendwa sana wakati wa Ramadhani kama chakula baada ya kufunga.

Rundo kubwa la parachichi huuzwa na wachuuzi wa mitaani ili wenyeji waweze kujitengenezea ZaaZaa zao nyumbani, na ZaaZaa inauzwa kwenye maduka ambayo yana utaalam wa vyakula vya kifungua kinywa na vitafunio kote nchini. Kwa kawaida hugharimu dirham 20 hadi 30 (pauni 1.60 hadi 2.40).

"Watu hawahesabu kalori wakati wa Ramadhani," Al Kasimu alisema. "Wanatafuta kujisikia kushiba na kupata nguvu tena baada ya kufunga siku nzima."

"Wamorocco, kwa kiasi kikubwa, wanaishi katika jamii ya Kiislamu na hawanywi pombe, kwa hiyo kuna utamaduni wa kijamii wa kutafuta vinywaji laini," Patera anasema. "ZaaZaa ni sehemu muhimu ya maisha ya kijamii."

Licha ya umaarufu wa ZaaZaa miongoni mwa wenyeji, bado haijajulikana kwa walio nje ya nchi.

Al Kasimu anakumbuka alifurahi aliposikia kuhusu kuibuka kwa milkisheki katika miaka ya 2010 katika migahawa nchini Marekani, Uingereza na Australia.

"Kila mtu alikuwa akiona milkisheki ni jambo kubwa na nakumbuka niliwaza, 'tumekuwa na mchanganyiko kama huo kwa muda mrefu nchini Morocco. Ambayo ni ZaaZaa!”

Watalii wanaotaka kujaribu mchanganyiko huo huenda watapata changamoto kwa sababu mara nyingi hauwekwi kwenye orodha ya chakula, kulingana na Amanda na Youssef Mouttaki, mke na mume wanaomiliki kampuni ya Moroccan Food Adventures.

Ni kampuni ya watalii ambayo inalenga kuuza chakula halisi cha Morocco na kuwapa uzoefu watalii wanaozungumza Kiingereza.

“Maeneo unayokwenda kuipata ni ya mtaani sana na mara nyingi utalazimika kuagiza ndipo itengenezwe,” anasema Amanda ambaye kwa mara ya kwanza aliijua ZaaZaa kupitia mumewe walipokuwa wakichumbiana.

Wakati huo huo, Youssef anasema kuna njia rahisi ya kujua kama umeagiza ZaaZaa yenyewe. Ukipata ZaaZaa na kujiuliza nitaanzaje kula hiki! Hiyo ndiyo ZaaZaa sasa."

Namna ya kuandaa ZaaZaa

g

Chanzo cha picha, Alia Al Kasimu)

Maelezo ya picha, Ili kutengeneza ZaaZaa, parachichi huchanganywa na maziwa, karanga na matunda yaliyokaushwa

Parachichi 1 kubwa lililoiva. Vikombe viwili (500ml) vya maziwa baridi. Tende tatu. Kijiko kimoja cha lozi mbichi (almonds). Kijiko kimoja cha jozi (walnuts)

Saga parachichi, maziwa, tende, lozi na jozi hadi viwe laini. Weka shira ya ladha upendayo kwenye glasi. Kisha mimina mchanganyiko wako kwenye glasi. Juu unaweza kuweka tena shira kidogo.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah