Afya: Faida za kiafya usizozijua za viungo vya chakula

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Dkt. Emma Davies
- Nafasi, Science Focus
Watu wengi tunapenda chakula kizuri chenye viungo, na licha ya viungo kuwa ghali katika baadhi ya maeneo – watu hawaachi kutoa pesa na kuagiza bila ya pengine kujua manufaa makubwa yaliyomo.
Mfano, bizari katika mchuzi wako inaweza kukusaidia kukuza kumbukumbu, pilipili inaoweza kukusaidia kupunguza maumivu, na zafarani inaweza kuongeza uwezo wako wa kufanya mapenzi.
Zafarani

Chanzo cha picha, Getty Images
Maua ya zafarani ni kiungo cha bei ghali ulimwenguni, zafarani ina rangi ya kuvutia ni yenye ladha ya uchungu kidogo. Zafarani imejaa vioksidishaji na tafiti nyingi zinaonyesha ina sifa ya kupambana na saratani. Pia inasemekana ni nzuri kwa ubongo.
Baadhi ya tafiti zinaonyesha kutumia milligram 30 kwa siku inaweza kusaidia kupunguza unyogovu. Tafiti nyingine zinaonyesha kutumia kila siku kunaweza kuboresha ubongo na kupambana na magomjwa ya kupoteza kumbukumbu.
Utafiti kutoka nchini Iran unaoonyesha matibabu ya kutumia zafarani kwa mwezi mmoja hutoa nguvu ya kufanya mapenzi kwa wanawake wanaosumbuliwa na msongo wa mawazo.
Bizari

Chanzo cha picha, Getty Images
Kiungo hiki hutoka kwenye mzizi wa mmea jamii ya tangawizi. Bizari imetumika kwa matibabu kwa karibu miaka 4,000 na inadaiwa inaweza kutibu magonjwa mengi; maumivu ya viungo na tatizo la uume kutosimama – shukrani kwa unga wake wa njano.
Mwaka 2011, watafiti wa kiharusi katika Kituo cha Matibabu cha Cedars-Sinai, Marekani, waligundua unga wa njano uliweza kutibu kiharusi kwa sungura.
Katika Chuo Kikuu cha Illinois, timu ya watafiti wamegundua njia ambayo inaonekana kuwa na ufanisi katika kutibu kansa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na melanoma na saratani ya matiti.
Vile vile, katika vipimo vya maabara katika Chuo Kikuu cha Florida, wanasayansi wametumia unga wa bizari kuharibu na kupambana na saratani ambayo hugunduliwa kwa watoto.
Pia kuna ushahidi unga wa bizari unaweza kusaidia kwa matatizo ya kumbukumbu. Timu ya Chuo Kikuu cha California, ilichagua kirutubisho kinachopatikana kwa wingi katika unga huo kiitwacho theracurmin kwa ajili ya utafiti wao kwa watu wazima 40 wenye shida ya kumbukumbu.
Washiriki walitumia miligramu 90 mara mbili kwa siku kwa miezi 18. Matumizi hayo yaliwafanya washiriki kuimarika pakubwa kumbukumbu zao.
Mdalasini

Chanzo cha picha, Getty Images
Gome hili la mti lenye harufu nzuri hutumiwa kwenye vyakula vingi vitamu. Mdalasini una ladha nzuri na umetumika kwa muda mrefu katika dawa za jadi, haswa kutibu gesi tumboni na tatizo la kusaga chakula.
Utafiti unaonyesha mdalasini aina ya casia, inaweza kupunguza viwango vya sukari katika damu kwa watu walio na ugonjwa wa kisukari cha aina ya 2. Ingawa matokeo bado hayajathibitishwa.
Utafiti wa Chuo Kikuu cha Ohio unaonyesha mdalasini una ufanisi zaidi katika kupunguza viwango vya sukari ya damu kuliko hata mlo maalumu.
Harufu ya kupendeza ya mdalasini na ladha yake hutokana na kemikali inayoitwa cinnamaldehyde, ambayo ina uwezo wa kuzuia bakteria na kuvu. Utafiti mwingine unaonyesha kemikali hizo zinaweza kusaidia kuzuia unene.
Pia kuna ushahidi mdalasini unaweza kuboresha ubongo. Utafiti katika Kituo cha Matibabu cha Chuo Kikuu cha Rush huko Chicago, Marekani, uligundua kuwa mdalasini ulionekana kusaidia panya kujifunza na uliongeza kiwango cha protini inayohusika katika kumbukumbu na kujifunza inayoitwa CREB.
Watafiti wanasema mwili hubadilisha mdalasini na kuunda sodium benzoate, ambayo hutumiwa sana kama matibabu ya kemikali kwa majeraha ya ubongo. Lakini fikiria mara kabla ya kutumia kiasi kikubwa cha mdalasini, una kemikali zinazoweza kuharibu ini.
Pilipilipili

Chanzo cha picha, Getty Images
Pilipili ya kuwasha ilianzia Mexico zaidi ya miaka 6,000 iliyopita lakini imeenea kote ulimwenguni. Hutumika kama dawa ya kutuliza maumivu mbalimbali, mfano viungo vya mwili na mishipa ya fahamu.
2015, timu kutoka Chuo cha Sayansi ya Tiba cha China ilifuatilia afya ya karibu watu nusu milioni kwa miaka kadhaa. Wale waliokula chakula chenye pilipili mara moja au mbili kwa wiki walikuwa na kiwango cha chini cha vifo kuliko wale ambao hawali pilipili.
Uchunguzi wa Afya na Lishe kutoka China unaonyesha kuwa matumizi ya pilipili pia yanahusishwa na viwango vya chini vya unene wa kupindukia.
Utafiti wa hivi karibuni wa Australia unasema wale wanaokula pilipili wana uwezekano mdogo wa kuwa na shinikizo la damu. Pilipili huongeza uzalishaji wa oksijini katika mishipa ya damu na huilinda dhidi ya kuvimba.
Pia ina uwezo wa kupambana na saratani. Ushahidi unaonyesha pilipili inaweza kusaidia kuzuia saratani fulani kutokea na kuzuia ukuaji wa uvimbe. Inadhaniwa kuwa na uwezo wa kuua seli za saratani ya kibofu cha mkojo.
Hata katika suala la lishe ya kawaida, pilipili ina viwango vya juu vya vitamini A na C. Ikiwa wewe si mpenzi wa pilipili, kumbuka maumivu unayohisi wakati wa kula yatafifia kadiri unavyokula mara kwa mara.
Tangawizi

Chanzo cha picha, Getty Images
Mzizi huu unatoka katika familia moja na manjano - umetumika tangu karne ya 4 kwa maumivu ya tumbo, kichefuchefu na kuendesha (kuhara). Wagiriki wa Kale waliitumia kupambana na kichefuchefu.
Nguvu yake ya kuponya kichefuchefu inamaanisha kuwa inanunuliwa mara kwa mara na wanawake wajawazito. Wakati huo huo, inajulikana pia kuwa na uwezo wa kusaidia kupambana na saratani.
Jambo la kutia moyo ni ukweli usiojulikana kwamba tangawizi huchochea kutokwa na jasho - hivyo hutufanya tuhisi joto, haswa tunapohisi baridi.
Uwezo wa tangawizi wa kupunguza kichefuchefu, ugonjwa wa yabisi na maumivu kwa ujumla unahusishwa na kemikali zinazoitwa gingerols. Inaweza kupunguza kiwango cha sukari kwenye damu na kusaidia kukulinda dhidi ya kisukari cha aina ya 2.
Uchunguzi kutoka Japan kwa panya unaonyesha tangawizi ina uwezo wa kupambana na kisukari kupitia mbinu mbalimbali. Waligundua inaweza kuathiri jeni zinazohusiana na kisukari na kueleza inaweza kutumika kutibu na kuzuia ugonjwa wa kisukari cha aina ya 2.
Tafiti zinaonyesha inaweza kulinda ubongo na kusaidia kupambana na saratani. Vilevile utafiti wa kimaabara wa 2015 nchini India ulifichua kuwa inaweza kusaidia kupambana na saratani ya tumbo na utumbo mpana.
Imetafsiriwa an Rashid Abdallah na kuhaririwa na Munira Hussein.