Mambo sita kuuelewa msimamo wa Papa mpya

Chanzo cha picha, Evandro Inetti/Zuma Press Wire
Robert Francis Prevost alichaguliwa kuwa Papa wa 267 na ataongoza Kanisa Katoliki lenye watu bilioni 1.4. Ni mzaliwa wa Chicago, Marekani. Ingawa baadhi ya misimamo yake kuhusu baadhi ya masuala bado hayako wazi, kuna yale ambayo yanaonekana yako wazi.
Papa Leo alichaguliwa kuwa kiongozi mpya wa Kanisa Katoliki Alhamisi kufuatia kifo cha mtangulizi wake, Papa Francis, katika kongamano la siku mbili katika Jiji la Vatican.
Alieleza kuwa amechagua jina Leo kwa heshima ya Papa wa karne ya 19 aliyejulikana kwa mafundisho yake juu ya haki za kijamii.
Papa Leo atasimikwa rasmi katika Ibada ya Misa Takatifu katika uwanja wa St Peter's Square wiki ijayo tarehe 18 Mei.
Vita na Amani
Miaka mitatu iliyopita, akiwa Askofu Robert Prevost, alikosoa uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine na kusema ni vita vya kibeberu na kulaani uhalifu dhidi ya ubinadamu aliosema unafanywa huko.
Baada ya kuchaguliwa kuwa Papa hakujizuia kuzungumzia amani. Papa Leo XIV alitoa wito wa "kusiwe na vita tena" katika ujumbe kwa mataifa yenye nguvu duniani wakati wa hotuba yake ya Jumapili ya kwanza huko Vatikani.
Akitafakari juu ya migogoro ya sasa, Papa alitoa wito wa "amani ya kudumu" katika vita vya Ukraine, kusitishwa mapigano huko Gaza, na kukaribisha makubaliano ya kumaliza uhasama wa hivi karibuni kati ya India na Pakistani.
Alisema "anaumizwa sana" na yanayoendelea Gaza, alionyesha kufurahishwa na "makubaliano ya kusitisha mapigano" kati ya India na Pakistan, na alitaka "amani ya kweli, na ya kudumu" nchini Ukraine.
Unyanyasaji wa watoto
Prevost anashutumiwa "kupuuza madai" ya unyanyasaji wa kijinsia uliofanywa na makasisi wawili nchini Peru, na "ana historia ya kupinga ufichuzi wa taarifa za unyanyasaji kwa umma," kulingana na shirika la waathiriwa wa unyanyasaji la Bishopability.
“Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, alipokuwa akiongoza Baraza la Maaskofu, alisimamia kesi za maaskofu wanaotuhumiwa kwa unyanyasaji na kuzificha,” anasema Anne Barrett Doyle, mkurugenzi mwenza wa Bishopability. "Alidumisha usiri wa mchakato huo, hakutoa majina wala data. Chini ya uangalizi wake, hakuna askofu aliyevuliwa cheo chake."
Kulingana na ripoti ya Chuo cha Makadinali kuhusu yeye, wafuasi wa Leo "wanamtetea na kusema kesi hizo zimeripotiwa kwa njia isiyo sahihi na isivyo haki kwenye vyombo vya habari." Wanasisitiza alifuata taratibu zinazofaa katika kesi ya makasisi wawili wa Peru wanaotuhumiwa kuwadhalilisha wasichana.
Suala la unyanyasaji wa kijinsia na kufichwa kwa kesi hizo, huenda likamsumbua Papa Leo kama ilivyokuwa kwa Francis. Ingawa Francis alielewa vyema ukubwa wa tatizo hilo katika kanisa, lakini waathiriwa wanasema hakuchukua hatua madhubuti za kutosha na watakuwa wanamfuatilia Papa Leo.
Masuala ya LGBTQ+
Katika miaka ya hivi karibuni, Prevost kwa kiasi kikubwa amejizuia kuzungumzia maswala ya mapenzi ya jinsia moja. Mwaka 2012, alionyesha wasiwasi wake kwamba vyombo vya habari vya magharibi na tamaduni za kisasa, kwamba mambo hayo "yanachochea imani na matendo ambayo yanapingana na Injili," akimaanisha hasa "maisha ya ushoga" na "familia zinazojumuisha wapenzi wa jinsia moja na watoto wao wa kuasili."
Mwaka jana, hakukubali wala kukataa baraka kwa wapenzi wa jinsia moja, akisema kuna tofauti za kitamaduni kote ulimwenguni, huku baadhi ya nchi zikiendelea kuharamisha uhusiano wa watu wa jinsia moja.
Mwaka 2016, Leo alipinga kufundisha masomo ya jinsia na ngono katika shule za Peru, kulingana na vyombo vya habari vya huko.
Wanawake na Uongozi wa Kanisa

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa mujibu wa gazeti la The Guardian, Oktoba 2023, Prevost alisema kuwaweka wanawake katika nafasi za uongozi kama kuwafanya makasisi - hakutasuluhisha matatizo ya kanisa na kunaweza kuunda matatizo mapya.
Alisema, "mapokeo ya kitume ni jambo ambalo limeelezwa kwa uwazi sana, hasa kama unataka kuzungumzia suala la kuwafanya wanawake kuwa makasisi.”
Lakini, aliongeza: “Naamini kutakuwa na utambuzi unaoendelea kwamba wanawake wanaweza kuchangia mambo mengi katika maisha ya kanisa katika nafasi nyingine mbalimbali.”
Mwaka 2022, aliteua wanawake watatu kumsaidia katika kazi yake ya ushauri kwa Papa Francis juu ya uteuzi wa maaskofu.
Mabadiliko ya tabia nchi
Akiwa kardinali, Prevost aliwahi kuhimiza jamii iondoke katika maneno na kwenda katika vitendo "kushughulikia tatizo la mabadiliko ya tabia nchi." Kuitawala dunia hakupaswi kuwa kwa "udhalimu," alisema kulingana na Vatican News, na badala yake lazima kuwe na "uhusiano mwema" na mazingira.
Francis naye alijitolea kushughulikia shida ya mabadiliko ya tabia nchi: Aliandika sana juu ya mabadiliko hayo, na kuwa mwenyeji wa mikutano ya kilele ya mazingira na alikutana na wanaharakati na watunga sera.
Uavyaji mimba
Wakati akiwa chuo kikuu Leo alikuwa mwanachama wa klabu ya Villanovans for Life alipokuwa akihudhuria Chuo Kikuu cha Villanova huko Philadelphia, kulingana na rais wa klabu hiyo Eileen Sceski. Leo alipata shahada ya kwanza ya hisabati kutoka chuo kikuu mwaka 1977.
“(Leo) alikuwa miongoni mwa wanachama wa awali wa klabu, pamoja na waanzilishi-wenza Margaret Mary Filoromo na Robert Dodaro,” anasema Sceski, na kuongeza, “Villanovans for Life ni klabu kongwe ya chuo kikuu ya kupinga utoaji mimba.”
Kanisa Katoliki limepinga kwa muda mrefu utoaji wa mimba, na Papa Francis aliita hiyo ni "dhambi kubwa" na akaulinganisha utaratibu huo na "kuua," na akaeleza huruma yake kwa wanawake ambao wametoa mimba, akisema uamuzi wao ni wa "kuumiza na wenye uchungu."
Imetafsiriwa na Rashid Abdalla