Moto wa nyika Los Angeles ulisababishwa na nini?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, James FitzGerald
- Nafasi,
Moto wa nyika ambao umekuwa vigumu kudhibitiwa unateketeza sehemu za Los Angeles, na kusababisha vifo vya takriban watu watano, kuharibu mamia ya majumba, na kulazimisha zaidi ya watu 130,000 kukimbia kutoka majumbani mwao katika jiji la pili kwa ukubwa Marekani.
Licha ya jitihada za wazima moto, miale mikubwa ya moto inaendelea kushika kasi, huku hali ya hewa na athari za mabadiliko ya tabianchi zikitarajiwa kuendelea kuzidisha moto siku zijazo.
Ni yapi yaliojiri?
Zaidi ya watu 137,000 wamekimbia majumbani mwao, wengi wao wakiwa na mizigo kidogo walichoweza kubeba.
Polisi wamesema kuwa watu watano wamepoteza maisha, na miili yao kupatikana karibu na moto wa Eaton, ingawa chanzo cha vifo vyao hakijajulikana. Kama moto wa Palisades ulivyokuwa mkubwa zaidi, moto wa Eaton pia haujaweza kudhibitiwa.
Kwa upande mwingine, moto wa Sunset ambao ulikuwa ukiathiri eneo maarufu la Hollywood Hills umeanza kupungua lakini bado haujadhibitiwa. Amri za uhamishaji kwa eneo la Hollywood Hills West zimeondolewa.
Majumba karibu 2,000 yanajulikana kuharibiwa, ikiwemo nyumba, shule, na biashara katika Barabara maarufu ya Sunset Boulevard. Mtaalamu wa moto, ambaye alizungumza na BBC, alisema kuwa "mitaa yote… imeharibiwa kabisa".
Miongoni mwa watu maarufu waliopoteza nyumba zao ni Leighton Meester na Adam Brody, walioshiriki tu tuzo za Golden Globe siku chache zilizopita, pamoja na Paris Hilton.
Sekta ya bima inahofia kuwa huu unaweza kuwa mmoja wa milipuko mikubwa ya moto katika historia ya Marekani, na hasara za bima zinatarajiwa kuwa zaidi ya dola bilioni 8 (pesa za Uingereza £6.5 bilioni) kutokana na thamani kubwa ya mali kuteketezwa na moto huo wa nyika.
Hata hivyo, kuna tumaini kidogo kwa wazima moto, kwani hali ya hewa ya moto katika kusini mwa California imeshushwa kutoka "yenye hatari sana" hadi "yenye hatari".
Lakini mtaalamu wa hali ya hewa wa BBC, Sarah Keith-Lucas, anasema hakuna mvua inayotarajiwa katika eneo hilo kwa angalau wiki moja ijayo, hivyo hali inabakia kuwa huenda moto ukaendelea.
Mafuta ya umeme yamekatwa katika maeneo mengi ya jiji, na msongamano wa magari umeongezeka.
Kwa kuongeza, baadhi ya shule na Chuo Kikuu cha California, Los Angeles (UCLA) vimefungwa.
Mzozo wa kisiasa kuhusu ufanisi wa maandalizi ya jiji wakati wa dharura umeibuka baada ya kugundulika kuwa mabomba ya baadhi ya wazima moto hayakuwa na maji, jambo ambalo limeibuliwa na rais mteule wa Marekani, Donald Trump.
Lakini katika nchi jirani ya Pasadena, Mkuu wa Zimamoto Chad Augustin alisema eneo hilo lilichelewa kidogo kwa uokozi kutokana na maji ya kuzima moto kukosa shinikizo la kurusha maji maghorofani.Lakini Masuala yote yametatuliwa, alisema.
Alihusisha suala hilo na vyombo vingi vya moto kuvuta maji kwa wakati mmoja pamoja na kupoteza kwa shinikizo la kupunguza nguvu ya kurusha maji ya kuzima moto.
Moto wa nyika umeathiri maeneo gani?
Kwa sasa, moto angalau tano unawaka katika maeneo mapana, kulingana na maafisa wa moto wa California, Alhamisi asubuhi:
Eneo la Palisades: Moto wa kwanza kutokea Jumanne na kuwa moto mkubwa zaidi katika eneo hilo, unaweza kuwa moto mbaya zaidi katika historia ya jimbo. Umechoma sehemu kubwa ya ardhi, ukifunika zaidi ya ekari 17,200, ikiwemo eneo la kifahari la Pacific Palisades.
Ebeo la Eaton: Moto huu umeathiri sehemu ya kaskazini ya Los Angeles, ukiteketeza miji kama Altadena. Ni moto wa pili kwa ukubwa katika eneo hilo, ukiteketeza karibu ekari 10,600.
Eneo la Hurst: Lilio kaskazini mwa San Fernando, lilianza kuchomeka Jumanne usiku na limeongezeka hadi ekari 855, ingawa wazima moto wamefanikiwa kwa kiasi kidogo kudhibiti moto huo.
Eneo la Lidia: Moto huu ulianzia Jumanne alasiri katika eneo la milima la Acton kaskazini mwa Los Angeles na umefikia ukubwa wa ekari karibu 350. Mamlaka zinasema umeweza kudhibitiwa kwa asilimia 40.
Eneo la Sunset: Moto huu ulianzia Jumanne jioni katika Hollywood Hills, ukikua hadi ekari 20 chini ya saa moja. Umezunguka ekari 43 lakini sasa umeanza kupungua.
Moto wa awali wa Woodley na Olivas sasa umeweza kudhibitiwa, kulingana na maafisa wa moto wa eneo hilo.
Chanzo cha moto LA

Chanzo cha picha, Getty Images
Maafisa wanataja upepo mkali na ukame katika eneo hili, ambao umeifanya mimea kuwa kavu na rahisi kuwaka moto.
Athari zinazowezekana za mabadiliko ya tabianchi pia zinatajwa - ingawa mazingira halisi bado hayajulikani.
Zaidi ya asilimia 95 ya mizarani ya moto katika eneo hili inaanzishwa na binadamu, kulingana na David Acuna, mkuu wa kikosi cha moto cha California, ingawa maafisa hawajatoa maelezo kamili kuhusu chanzo cha moto huu wa sasa.
Kipengele muhimu kilichotajwa katika kuenea kwa moto ni upepo wa Santa Ana, ambao unapuliza kutoka bara kuelekea pwani. Kwa kasi ya zaidi ya maili 60 kwa saa (97 km/h), inaaminika kuwa upepo huu umekuwa ukifanya moto kuzidi kuteketeza.
Mabadiliko ya tabia nchi yamechangia vipi?

Chanzo cha picha, Getty Images
Ingawa upepo mkali na ukosefu wa mvua vinachochea moto, wataalamu wanasema kuwa mabadiliko ya tabianchi yanabadilisha hali ya kawaida na kuongeza uwezekano wa milipuko kama hii ya moto.
Utafiti wa serikali ya Marekani hauna shaka katika kuhusisha mabadiliko ya tabianchi na milipuko mikubwa na kali ya moto katika magharibi mwa Marekani.
" Mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo joto kali, ukame mrefu, na anga inayohitaji mvua, imekuwa kichocheo muhimu katika kuongezeka kwa hatari na ukubwa wa mizarani ya moto katika magharibi mwa Marekani," inasema Idara ya Kitaifa ya Oceanic na Hali ya Hewa.
Baada ya msimu wa joto kali na ukosefu wa mvua katika miezi ya karibuni, California iko katika hatari kubwa.
Msimu wa moto kusini mwa California kawaida huaminika kuanza kutoka mwezi Mei hadi Oktoba, lakini gavana wa jimbo hilo, Gavin Newsom, alieleza mapema kuwa milipuko ya moto imekuwa tatizo la kila mwaka.
"Hakuna msimu wa moto," alisema. "Ni mwaka wa moto."
Akizungumza na BBC, Bw. Acuna alisema kuwa Moto wa Palisades ni mara ya tatu tu katika miaka 30 iliyopita ambapo moto mkubwa umeibuka Januari.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid