Wasichana walivyogeukia ufumaji mazulia baada ya marufuku ya shule Afghanistan

Katika karakana huko Kabul ambapo mazulia yanatengenezwa, mamia ya wanawake na wasichana wanafanya kazi katika nafasi finyu, hewa nzito na ya kudumaza.
Miongoni mwao ni Salehe Hassani mwenye umri wa miaka 19. "Sisi wasichana hatuna tena nafasi ya kusoma," anasema huku akitabasamu. "Mazingira yamechukua haki hiyo kutoka kwetu, kwa hivyo tuligeukia semina."
Tangu kundi la Taliban kunyakua mamlaka mwaka 2021, wasichana wenye umri wa zaidi ya miaka 12 wamezuiwa kupata elimu, na wanawake kutoka kwenye kazi nyingi.
Mnamo 2020, ni 19% tu ya wanawake walikuwa sehemu ya wafanyakazi,mara nne chini ya wanaume. Idadi hiyo imepungua zaidi chini ya utawala wa Taliban.
Ukosefu wa fursa, pamoja na hali mbaya ya kiuchumi ambayo nchi inakabiliana nayo, vimewasukuma wengi katika siku ndefu, ngumu za kufuma mazulia, moja ya biashara chache ambazo serikali ya Taliban inaruhusu wanawake kufanya kazi.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, maisha ya Waafghanistan milioni 1.2 hadi 1.5 yanategemea sekta ya ufumaji zulia, huku wanawake wakiwa karibu 90% ya nguvu kazi.
Katika uchumi ambao Umoja wa Mataifa ulionya katika ripoti ya 2024 "kimsingi umeporomoka" tangu Taliban kuchukua madaraka, biashara ya kuuza mazulia inakua.
Wizara ya Viwanda na Biashara ilibaini kuwa katika miezi sita ya kwanza ya 2024 pekee, zaidi ya kilo milioni 2.4 za mazulia yenye thamani ya $8.7m (£6.6m), zilisafirishwa kwenda nchi kama vile Pakistan, India, Austria na Marekani.
Lakini hii haimaanishi mishahara bora zaidi kwa wafumaji. Baadhi ya waliozungumza na BBC walisema hawakuona faida yoyote kutokana na kipande kilichouzwa Kazakhstan mwaka jana ambacho kiliingiza $18,000.

Ndani ya Afghanistan, mazulia yanauzwa kwa bei ndogo sana, kati ya $100-$150 kwa kila mita ya mraba. Wakihitaji pesa kusaidia familia zao na kuwa na chaguzi chache za kuajiriwa, wafanyakazi wamenaswa katika kazi inayowalipa kidogo.
Wafumaji wa mazulia wanasema wanapata takribani $27 kwa kila mita ya mraba, ambayo kwa kawaida huchukua takribani mwezi mmoja kuzalisha. Hiyo ni chini ya dola moja kwa siku licha ya zamu ndefu, zenye kuchosha ambazo mara nyingi huchukua hadi saa 10 au 12.
Nisar Ahmad Hassieni, mkuu wa kampuni ya Elmak Baft, ambaye aliruhusu BBC kuingia ndani ya karakana zake, alisema kuwa huwalipa wafanyakazi wake kati ya $39 na $42 kwa kila mita ya mraba. Alisema wanalipwa kila baada ya wiki mbili, na siku ya kazi ya saa nane.
Kundi la Taliban limesema mara kwa mara kwamba wasichana wataruhusiwa kurejea shuleni mara matatizo yao, kama vile kuoanisha mtaala na maadili ya Kiislamu, yatakapotatuliwa, lakini hadi sasa, hakuna hatua madhubuti zilizochukuliwa kufanikisha hilo.
Bw Hassieni alisema kuwa, kufuatia kuongezeka kwa serikali ya Taliban, shirika lake lilifanya kuwa dhamira yake ya kusaidia wale walioachwa nyuma na kufungwa.
"Tulianzisha karakana tatu za kusuka zulia na kusokota sufu," anasema.
"Takriban 50-60% ya mazulia haya yanasafirishwa kwenda Pakistani, huku mengine yanatumwa China, Marekani, Uturuki, Ufaransa na Urusi ili kukidhi mahitaji ya wateja."

Shakila, mwenye umri wa miaka 22, anatengeneza zulia na dada zake katika moja ya vyumba vya nyumba ya kukodisha ambayo pia wanaishi pamoja na wazazi wao wazee na kaka watatu. Wanaishi katika eneo maskini la Dasht-e Barchi, viunga vya magharibi mwa Kabul.
Wakati mmoja alikuwa na ndoto za kuwa wakili, lakini sasa anaongoza shughuli ya kutengeneza mazulia ya familia yake.
"Hatukuweza kufanya kitu kingine chochote," Shakila ananiambia. "Hakukuwa na kazi zingine".
Anaeleza jinsi baba yake alivyomfundisha kufuma akiwa na umri wa miaka 10 na alikuwa akipata nafuu kutokana na ajali ya gari.
Kile ambacho kilianza kuwa ustadi wa lazima katika nyakati za magumu sasa kimekuwa tegemeo la familia.
Dada yake Shakila, Samira mwenye umri wa miaka 18, alitamani kuwa mwandishi wa habari. Mariam, 13, alilazimika kuacha kwenda shule kabla hata hajaanza kuwa na ndoto ya kazi.
Kabla ya kurudi kwa Taliban, wote watatu walikuwa wanafunzi katika Shule ya sekondari ya Sayed al-Shuhada.
Maisha yao yalibadilishwa moja kwa moja baada ya milipuko mibaya ya mabomu katika shule hiyo mnamo 2021 kuua watu 90, wengi wao wakiwa wasichana wadogo, na kuwaacha karibu 300 wakiwa wamejeruhiwa.
Serikali iliyopita iliilaumu Taliban kwa shambulio hilo, ingawa kundi hilo lilikanusha kuhusika kwa vyovyote vile.
Kwa kuhofia msiba mwingine, baba yao alifanya uamuzi wa kuwaondoa shuleni.

Samira, ambaye alikuwa shuleni wakati mashambulizi yakitokea, ameachwa na kiwewe, akizungumza kwa kigugumizi na kujitahidi kujieleza. Bado, anasema antafanya chochote kiwezekanacho kurudi kwenye elimu rasmi.
"Nilitaka sana kumaliza masomo yangu," anasema. "Sasa kwa vile Taliban wako madarakani, hali ya usalama imeimarika na kumekuwa na mashambulizi machache ya kujitoa muhanga.
"Lakini shule bado zimefungwa. Ndiyo maana inabidi tufanye kazi."
Licha ya malipo duni na saa nyingi za kazi ambazo wanawake hao wanakabili, roho za wengine hazijavunjika.
Akiwa amerudi kwenye karakana moja, Salehe, akiwa amedhamiria na mwenye matumaini, alijieleza kuwa amekuwa akisoma Kiingereza kwa miaka mitatu iliyopita.
"Ingawa shule na vyuo vikuu vimefungwa, tunakataa kusitisha elimu yetu," anasema.
Siku moja, Salehe anaongeza, ana mpango wa kuwa daktari kiongozi na kujenga hospitali bora zaidi nchini Afghanistan.