Mtandao wa kamera za Taliban zinazofuatilia mamilioni ya watu

- Author, Mahjooba Nowrouzi
- Nafasi, BBC
Katika kituo cha kufuatilia watu, kilichojaa televisheni, jeshi la polisi la Taliban linafuatilia watu kupitia mtandao wake mpya wa kamera 90,000 za CCTV - hutazama maisha ya kila siku ya mamilioni ya watu.
"Tunaufuatilia mji mzima wa Kabul kutokea hapa," anasema Khalid Zadran, msemaji wa ofisi ya mkuu wa polisi wa Taliban.
Serikali inasema ufuatiliaji huo utasaidia kupambana na uhalifu, lakini wakosoaji wanahofia utatumika kuwabana wapinzani na kufuatilia kanuni kali za maadili zilizowekwa na serikali ya Kiislamu ya Taliban chini ya tafsiri yao ya sheria za Kiislamu (Sharia).
Wanahabari wa BBC ndio wa kwanza wa kimataifa kuruhusiwa kuona mfumo huo na namna unavyofanya kazi.
Ndani ya chumba cha ufuatiliaji, maafisa wa polisi huketi wakitazama video za moja kwa moja (mubashara) kupitia maelfu ya kamera, wakifuatilia maisha ya watu milioni sita wanaoishi Kabul. Wakitazama leseni za magari hadi sura za watu.
"Tunapogundua vikundi vya watu tunaowashuku kuwa wanashiriki matumizi ya dawa za kulevya, uhalifu, au kitu cha kutiliwa shaka katika vitongoji, tunawaeleza polisi wa eneo hilo haraka," anasema Zadran.
"Huenda haraka ili kuchunguza mkusanyiko huo."
Chini ya serikali iliyopita, Kabul ilikumbwa na mashambulizi ya kila siku kutoka Taliban na wale wanaojiita wanamgambo wa Islamic State, pamoja na utekaji nyara na wizi wa magari. Taliban ilipochukua tena madaraka mwaka 2021, waliahidi kukabiliana na uhalifu.
Idadi kubwa ya kamera za uchunguzi katika mji mkuu ni ishara ya kukua kwa mbinu za kisasa za Taliban katika kudumisha sheria na utulivu. Kabla ya kurejea kwao, kulikuwa na kamera 850 pekee katika mji mkuu, kulingana na msemaji wa vikosi vya usalama vilivyoondolewa madarakani.
Hata hivyo, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, serikali ya Taliban pia imeanzisha hatua kali mbali mbali zinazokiuka haki na uhuru wa watu, hasa wanawake. Serikali ya Taliban haijatambuliwa rasmi na nchi yoyote duniani.
Mfumo wa ufuatiliaji ambao BBC imeonyeshwa huko Kabul unaweza kufuatilia sura za watu. Kwenye skrini moja, picha za nyuso zinaonekana huku kila uso ukionyesha makadirio ya umri, jinsia na iwapo ana ndevu au barakoa.
"Katika siku ambazo hali ya hewa ni safi, tunaweza kuvuta uso wa mtu kutoka umbali wa kilomita moja," anasema Zadran.
Taliban pia hufuatilia wafanyakazi wao wenyewe. Katika kituo cha ukaguzi, askari walipofungua sehemu ya nyuma ya gari kwa ukaguzi, wafuatiliaji wa kamera walizumu lenzi zao, ili kuchunguza yaliyomo ndani buti.
Wizara ya mambo ya ndani inasema kamera hizo "zimechangia pakubwa katika kuimarisha usalama, kupunguza uhalifu, na kuwakamata wahalifu haraka."
Kuanzishwa kwa CCTV na pikipiki za doria kumepungua viwango vya uhalifu kwa 30% kati ya 2023 na 2024, lakini ni vigumu kuthibitisha takwimu hizi kwa uhuru.
Ukosoaji wa hatua hii

Hata hivyo, vikundi vya haki za binadamu vina wasi wasi kuhusu ufuatiliaji huu. Shirika la Amnesty International linasema kuweka kamera "kwa kisingizio cha 'usalama wa taifa' ni ishara ya muendelezo wa sera za kikatili za Taliban zinazokiuka haki za kimsingi za watu nchini Afghanistan - hasa wanawake katika maeneo ya umma."
Kwa mujibu wa sheria za Taliban wanawake hawaruhusiwi kutoa sauti wawapo nje ya nyumba zao, ingawa kiutendaji hili halisimamiwi kwa ukali. Wasichana wanazuiwa kupata elimu ya sekondari na ya juu. Wanawake wamezuiwa kufanya nyingi ya kazi.
Mwezi Desemba, wanawake wanaofunzwa kuwa wakunga na wauguzi waliiambia BBC kuwa waliamriwa kutorejea darasani. Na wanawake wanaoonekana katika mitaa ya kama Kabul, wanatakiwa kufunika uso (burqa).
Fariba, mhitimu anaeishi na wazazi wake huko Kabul, ameshindwa kupata kazi tangu Wataliban waingie madarakani. Ameiambia BBC kuwa kuna "wasiwasi mkubwa kwamba kamera za uchunguzi zinaweza kutumika kufuatilia hijabu za wanawake."

Taliban wanasema ni polisi wa jiji pekee wanaoweza kuufikia mfumo wa CCTV na Wizara ya maadili ya Taliban – lakini Polisi wa maadili wa Taliban hawatumii kamera hizo.
Lakini Fariba ana wasiwasi kuwa kamera hizo zitawaweka hatarini zaidi wale wanaopinga utawala wa Taliban.
"Watu wengi, hasa wanajeshi wa zamani, watetezi wa haki za binadamu na wanawake wanaoandamana, wanatatizika kutembea kwa uhuru na mara nyingi wanaishi kwa usiri," anasema.
Human Rights Watch, inasema Afghanistan haina sheria za ulinzi wa taarifa ili kudhibiti jinsi picha za CCTV zinavyohifadhiwa na kutumiwa.
Polisi wanasema video hizo hutunzwa kwa muda wa miezi mitatu pekee, na kwa mujibu wa wizara ya mambo ya ndani, kamera hizo hazina tishio kwa faragha kwani "huendeshwa kutoka chumba maalum na cha siri na mtu maalum na mtaalamu anayesimamia".
Kamera hizo zinaonekana kuwa zimetengenezwa na China na chapa yake ni Dahua, kampuni inayohusishwa na serikali ya China. Taarifa za awali kuwa kundi la Taliban walikuwa kwenye mazungumzo na kampuni ya Huawei Technologies ya China ya kununua kamera zilikanushwa na kampuni hiyo.
Maafisa wa Taliban walikataa kujibu maswali ya BBC kuhusu wapi walivitoa vifaa hivyo.
Gharama kwa raia

Baadhi ya gharama za kuendesha mtandao huo mpya zinawaangukia Waafghanistan wa kawaida ambao wanafuatiliwa na mfumo huo.
Katika nyumba moja katikati mwa Kabul BBC ilizungumza na Shella, ambaye aliombwa kulipia baadhi ya kamera zilizowekwa barabarani karibu na nyumba yake.
Hali ya kibinadamu huko Kabul, na Afghanistan kwa ujumla, bado ni mbaya baada ya miaka ya vita. Uchumi wa nchi hiyo uko katika hali mbaya, na ufadhili wa misaada ya kimataifa umesimamishwa kwa kiasi kikubwa tangu Taliban iliporejea madarakani. Kulingana na Umoja wa Mataifa, watu milioni 30 wanahitaji msaada.
"Ikiwa familia zinakataa kulipia [kamera], hutishiwa kukatwa maji na umeme ndani ya siku tatu," Shella anaongeza. "Tulilazimika kuchukua mikopo ili kulipia gharama.
"Watu wanaokufa njaa - kamera hizi zina faida gani kwao");