Kwanini Qatar imeshindwa kuipatanisha Israel na Hamas?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Jeremy Howell
- Nafasi, BBC World Service
Serikali ya Qatar imesema inasitisha juhudi za kuleta makubaliano ya amani kati ya Israel na Hamas, kwa sababu pande zote mbili haziko tayari kupatana.
Pia inaripotiwa kuwa inakabiliwa na shinikizo kutoka kwa Marekani kufunga ofisi ya Hamas nchini humo.
Nchi hiyo ndogo na tajiri Mashariki ya Kati -imekuwa ikipata ugumu wa kuleta makubaliano ya usitishaji wa mapigano katika mzozo wa sasa wa Israel na Hamas.
Qatar ni nchi ndogo katika Ghuba ya Uajemi yenye ukubwa wa kilomita za mraba 11,600. Inauza kiasi kikubwa cha gesi asilia nje na mapato ya mtu moja mmoja ni ya sita kwa ukubwa duniani.
Qatar kama mpatanishi

Chanzo cha picha, Getty Images
Serikali ya nchi hiyo imekuwa mpatanishi wa kimataifa. Katika miongo miwili iliyopita imepatanisha imesimamia mikataba kadhaa ya kusitisha mapigano kati ya pande zinazozozana Mashariki ya Kati, Ulaya na Afrika.
Ilikuwa mwenyeji wa mazungumzo kati ya Israel na Hamas kwa ajili ya kusitisha mapigano mwezi Novemba 2023, ambapo mateka 105 wa Israel waliachiwa na wafungwa 240 wa Kipalestina.
Mwaka 2020, Qatar ilileta makubaliano ya amani kati ya Taliban na Marekani ili kukomesha vita vya miongo miwili nchini Afghanistan. Hilo lilipelekea Marekani na washirika wake kuondoa majeshi yao na Taliban kuchukua mamlaka katika nchi hiyo.
Qatar pia ilifanya kazi kama mpatanishi katika makubaliano ya kubadilishana wafungwa kati ya Marekani na Iran mwaka 2023.
Mwaka huo huo, ilifanya upatanishi kati ya Urusi na Ukraine ili kurejeshwa watoto wa Ukraine ambao walichukuliwa kutoka Ukraine na kupelekwa Urusi wakati wa mzozo unaoendelea.
Mwaka 2022, Qatar ilisimamia usitishaji wa vita kati ya serikali ya Chad na makundi 40 ya upinzani, na mwaka 2010 ilisimamia makubaliano ya amani kati ya serikali ya Sudan na makundi yenye silaha katika jimbo la magharibi la Darfur.
Serikali ya Qatar imeandika katika katiba yake juu ya jukumu la nchi hiyo la kuwa mleta amani.
Kifungu cha saba kinasema: “Msingi wa sera ya mambo ya nje ya serikali ni kuimarisha amani na usalama wa kimataifa, kwa kuhimiza utatuzi wa migogoro ya kimataifa kwa njia ya amani.”
Sio tu kwamba Qatar ni mshirika wa karibu wa Marekani, na inahifadhi maelfu ya wanajeshi wake katika kambi ya anga ya Al Udeid, pia imeruhusu makundi yenye itikadi kali kama vile Taliban na Hamas kuanzisha ofisi ndani ya nchi hiyo.
“Hilo linaiwezesha nchi hiyo kufanya kazi kama daraja kati ya wanasiasa ambao hawawezi kuzungumza moja kwa moja,” kulingana na Dkt. HA Hellyer, kutoka Royal United Services, taasisi ya fikra huria yenye makao yake makuu nchini Uingereza.
"Qatar iko katika nafasi nzuri ya kuvifikia vikundi kama vile Taliban na Hamas, kwa sababu hawajawahi kugombana nao," anasema. "Na kwa sababu ya uwepo wa jeshi la Marekani, wawakilishi wa makundi haya wanajiona wako salama huko Doha.
"Wanahisi wanaweza kujadiliana kwa usalama, bila ya majaribio ya mauaji."
Dk Sanam Vakil, wa taasisi ya fikra huria, yenye makao yake makuu nchini Uingereza, Chatham House, anasema:
"Kuwa mpatanishi wa amani kunaifanya Qatar kuwa muhimu kwa Marekani, na ina maana kwamba ina ushawishi katika nchi za Magharibi.
Qatar ina timu ya wanadiplomasia ambao wamefunzwa kusimamia mazungumzo ya amani, anasema Dk Vakil. Hata hivyo, anasema, si mara zote wameweza kuzishawishi pande zinazozozana kufanya mapatano ya amani au kusitisha mapigano ya kudumu.
"Qatar inafanya vyema katika kuzileta pamoja pande mbili za mzozo, zenye kutaka amani wakati wa mwisho wa mzozo na vurugu unapofika," anasema.
Israel na Gaza

Chanzo cha picha, Getty Images
Wizara ya mambo ya nje ya Qatar imesema inasitisha juhudi zake za kupatanisha kati ya Israel na Hamas.
Hata hivyo, imetupilia mbali ripoti kwamba itafunga ofisi ya Hamas mjini Doha.
Serikali ya Israel kwa muda mrefu imeikosoa Qatar ikisema inapendelea upande Hamas na kulea kundi la kigaidi.
Dk Hellyer anasema: "Serikali ya Qatar iliwaalika viongozi wa Hamas kuweka ofisi zao huko kutoka Damascus baada ya kutofautiana na serikali ya Syria mwaka 2012. Walifanya hivyo kwa ushirikiano na Marekani na, pengine Israel."
Anasema Qatar iliisaidia Israel na Hamas kukubaliana kusitisha mapigano katika mizozo ya nyuma, "lakini ilikuwa ni katika kipindi ambacho pande zote mbili zilika kurejesha hali ya utulivu."
"Wakati huu hali ni tofauti," anasema Dk Vakil. “Serikali ya Israel inataka kuhakikisha usalama wake zaidi kuliko inavyotaka amani. Kuendelea na vita kutasaidia kufikia malengo yake. Hamas inataka amani ili iendelee kuwepo.”
Kumekuwa na uvumi kwamba Hamas huenda ikaondoka Qatar na kuhamishia ofisi yake Uturuki au Iran.
Lakini Dk Hellyer anasema Qatar ndio mahali salama zaidi kwa viongozi wake kukaa.
“Ismail Haniyeh alipoondoka Doha na kwenda Iran, aliuwawa na vikosi vya Israel haraka," anasema.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi