Malkia wa Hisabati akiwa na misheni ya kuwainua wasichana

Angela Tabiri

Chanzo cha picha, Angela Tabiri

Akijulikana nchini Ghana kama Malkia wa Hesabu, Dk Angela Tabiri ndiye Mwafrika wa kwanza kushinda shindano la Big Internet Math Off, mafanikio makubwa kabisa kwa mtu ambaye hakuwa amepanga kusoma hisabati.

Mghana huyo mwenye umri wa miaka 35 "anafurahia kutatua mafumbo na maswali ya hesabu" na ana matumaini kuwa ushindi wake wa mwaka 2024 utafungua ulimwengu wa hisabati kwa wanawake wengine wa Kiafrika ambao kwa kawaida wamekata tamaa ya kujikita kwenye mada hiyo.

Wanahisabati kumi na sita walialikwa kushindana kumpata "mtaalamu wa hisabati wa kuvutia zaidi duniani", tukio la upigaji kura ya umma lililoanzishwa katika 2018 na blogu ya Aperiodical.

Mshindi wa kwanza alikuwa Dr Nira Chamberlain, mtaalamu wa kwanza mweusi wa hisabati kujumuishwa katika kitabu cha kumbukumbu cha Uingereza 'Who's Who' na makamu wa rais wa bodi ya wataalamu ya Institute of Mathematics and its Applications.

Wakati wa tukio hilo wote hushindana dhidi ya kila mmoja, wawili katika kila mechi na kisha huenda robo fainali na nusu fainali hadi kumpata aliyeelezea dhana ya hisabati vyema zaidi.

Malengo yalianza Afrika Kusini na kisha kupanuka hadi Ghana, Senegal, Cameroon na Rwanda, kutoa mafunzo ya baada ya kuhitimu na utafiti katika sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati.

Dk Tabiri pia ni meneja wa kitaaluma wa Programu ya Wasichana katika Sayansi ya Hisabati, mpango wa ushauri na usaidizi kwa wasichana wa shule za sekondari nchini Ghana.

Ilianzishwa na Aims-Ghana mnamo 2020 ili "kuhakikisha kuwa tunatoa nafasi kwa wasichana wadogo ambao watakuwa wakiongoza katika utafiti na uvumbuzi katika sayansi ya hisabati".

Dk Angela Tabiri anavunja dhana kwamba hisabati ni "somo la wavulana"

Chanzo cha picha, Angela Tabiri

Dkt.Tabiri anasema idadi ya wasichana na wavulana wanaosoma hesabu katika shule ya sekondari ni takribani sawa lakini inashuka katika ngazi ya chuo kikuu.

Hii kwa kiasi fulani ni kwa sababu, anasema, wanafunzi wa kike hudhani kuwa kama watafanya hesabu, kazi pekee wanayoweza kufanya ni kufundisha, kwa sababu hesabu bado inaonekana kama "somo la mvulana" na kuna mifano michache sana ya kike.

Hili ni jambo ambalo Dk Tabiri anajaribu kubadilisha hilo.

Lakini safari yake katika hisabati haikuwa rahisi.

Alikulia Ashaiman, mojawapo ya vitongoji maskini zaidi, vilivyo na watu wengi vya Tema, kitovu cha viwanda na bandari iliyo umbali wa saa moja kwa gari mashariki mwa mji mkuu, Accra.

Nyumba ya familia yake ilikuwa na furaha, ana dada wanne na Dkt. Tabiri mara nyingi alikuwa akitafuta amani na utulivu wa kituo cha jumuiya ya vijana ili aweze kusoma.

Alitaka kufuata nyayo za dada wawili na kusomea usimamizi wa biashara katika chuo kikuu.

Lakini alama zake, ingawa zilikuwa juu, hazikuwa za juu vya kutosha na kwa hivyo alikubaliwa badala yake kwenye mchepuo wa hisabati na uchumi.

Dk Tabiri anasema. "Nambari na mafumbo vilinivutia, lakini sikuwahi kufikiria kuwa taaluma ya hisabati ilikuwa kwangu."

Mnamo 2015, Dk Tabiri alipata ufadhili wa kusoma Shahada ya Uzamivu katika Chuo Kikuu cha Glasgow huko Scotland. Ilikuwa kazi ngumu, anasema na hapo ndipo alipata wakati mzuri.

Alienda kutazama filamu iitwayo Figures Hidden, kuhusu wanahisabati wanawake weusi Wamarekani ambao walifanya kazi katika shirika la anga za juu la Marekani, Nasa, katika miaka ya 1950, wakati wa enzi za ubaguzi nchini Marekani.

"Ilikuwa filamu ya kufurahisha kuona hadithi ya wanawake hawa weusi ikisimuliwa kwenye jukwaa la kimataifa," anakumbuka. " Mwili ulinisisimka nilipokuwa nikiitazama."

Alitiwa moyo hasa na Catherine Johnson, ambaye ujuzi wake wa ajabu wa hisabati na hesabu ulikuwa muhimu sana kwa mafanikio ya safari za anga za juu za Marekani.

"Catherine Johnson alifanya kazi kwa bidii sana na kwa muda mrefu kazi yake ilifichwa. Alinifanya kutambua kwamba lazima niendelee tu.

"Kama kazi yako hata haitambuliwi sasa, itatambuliwa wakati mwingine katika siku zijazo. Ilikuwa ni mabadiliko ya kweli kwangu."

Ghana ilifikia hatua ya kihistoria mnamo 2024 wakati Dk Gloria Botchway alipokuwa mwanamke wa kwanza kuhitimu Chuo Kikuu cha Ghana naShahada ya Uzamili katika hesabu.

Ilikuwa ni safari iliyojaa shida, ikiwa ni pamoja na kuuza maji na viazi vikuu kando ya barabara kama mtoto wa miaka sita.

Dk Tabiri anajaribu kusaidia wasichana na wanawake wengine wa Kiafrika walio na malezi duni kufuata ndoto zao katika hisabati kupitia shirika lake lisilo la faida la FemAfricMaths.

Dkt Angela Tabiri anataka watoto wawe na malengo ya juu

Chanzo cha picha, Angela Tabiri

Sambamba na wafanyakazi wengine wa kujitolea, anatoa masomo kwa wanafunzi wachanga zaidi wa shule ya sekondari ana kwa ana na mtandaoni.

Pia huchapisha kwenye mahojiano ya mitandao ya kijamii anayofanya na wanahisabati wanawake kutoka kote ulimwenguni.

Dk Tabiri pia ana shauku kubwa juu ya uwezo wa sayansi na teknolojia ya kiasi ambacho hisabati ni muhimu kwao.

Watafiti na makampuni makubwa ya teknolojia kutoka duniani kote - ikiwa ni pamoja na China, Marekani, Uingereza, Australia na Afrika Kusini sasa wanakimbia kuendeleza teknolojia ya quantum, ikiwa ni pamoja na kompyuta za quantum na vifaa vya kupima vyema na vya sensorer.

Matumaini ni kwamba mafumbo magumu yatatatuliwa kwa kasi ya umeme na kutakuwa na ubunifu mkubwa katika maeneo kama vile dawa, sayansi ya mazingira, uzalishaji wa chakula na usalama wa mtandao.

"Kuna mazungumzo mengi sasa, faida na hasara, kazi ambazo zitazalishwa," anasema Dk Tabiri.

Imetafsiriwa na Lizzy Masinga