Homa ya Nyani: Tofauti tano kati ya Mpox na Uviko 19

Chanzo cha picha, Reuters
- Author, Dorcas Wangira
- Nafasi, BBC Africa health correspondent
- Akiripoti kutoka Nairobi
Shirika la Afya Duniani (WHO) lilipotangaza mpox kuwa dharura ya kiafya ya kimataifa kwa mara ya pili katika kipindi cha miaka miwili, watu wengi waliuliza: Je, hii ndiyo Covid-19 mpya?
Wanasayansi wanasema, “Hapana.”
"Mpox sio Covid mpya. Hatari ya mpox kwa watu ni ndogo,” anasema Dk Hans Kluge, mkurugenzi wa kanda wa WHO barani Ulaya.
“Tunajua jinsi ya kudhibiti mpox. Katika kanda ya Ulaya, tunajua hatua zinazohitajika ili kuondoa maambukizi yote.
Magonjwa yote mawili husababishwa na virusi, lakini yana dalili tofauti, na huenea kwa njia tofauti.
"Kuna tofauti nyingi zaidi kuliko kufanana," anasema Prof Rodney Adam, mtaalamu wa magonjwa ya kuambukiza katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Aga Khan nchini Kenya.
Mpox sio virusi vipya
Mpox, ambayo hapo awali ilijulikana kama monkeypox, imekuwepo tangu 1958, na virusi hivi viligunduliwa kwa mara ya kwanza kwa nyani waliofungiwa nchini Denmark.
Kisa cha kwanza kwa binadamu kiliripotiwa katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo mwaka 1970. Tangu wakati huo kumekuwa na milipuko Afrika Magharibi na Kati. Mara ya kwanza kutangazwa kuwa dharura ya kiafya duniani ilikuwa ni 2022, ugonjwa huo ulikuwa umeenea katika nchi zaidi ya 70.
Lakini mlipuko wa 2019 wa Uviko-19 huko Wuhan, China, ambao ghafla ukawa janga la ulimwengu, ulitokana na virusi vipya vya SARS-CoV2 - ambavyo havijatambuliwa hapo awali kwa wanadamu.
Wanasayansi wanasema tunajua zaidi kuhusu mpox, kuliko tulivyojua kuhusu Uviko-19 ilipokuwa dharura ya afya kwa dunia.
Mpox haiambukizi kama Uviko-19
Ingawa magonjwa yote mawili huenezwa kwa njia ya mawasiliano ya kimwili, Uviko-19 huenea haraka kwa njia ya hewa.
Watu wanaweza kuupata kwa kuvuta matone madogo ya majimaji kutoka kwa mtu aliyeambukizwa ambaye anakohoa, kupiga chafya, kuzungumza, kuimba au kupumua mbele yako, kulingana na WHO.
Mpox huenezwa kwa kugusana kwa karibu sana au kwa muda mrefu na mtu aliyeambukizwa, kama vile kugusana ngozi kwa ngozi, ikiwa ni pamoja na wakati wa ngono na kugusa matandiko na nguo zenye maambukizi.
Zaidi ya kesi milioni 760 za Covid-19 zilirekodiwa ulimwenguni kati ya Desemba 2019 na Agosti 2023, WHO inasema, imechukua miaka miwili tangu Mei 2022 kwa maambukizi ya mpox kufikia watu 100,000 ulimwenguni.
Mwaka 2024, Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC), kimerekodi kesi 18,910 na karibu vifo 600.
Chanjo zipo tayari kwa mpox

Chanzo cha picha, Reuters
Mwanzoni mwa janga la Covid-19 kulikuwa na mbio za kutengeneza chanjo. Lakini chanjo zinazotoa kinga dhidi ya mpox zinapatikana sasa.
Mpox inahusiana na ugonjwa wa ndui, ugonjwa ambao ulimwengu uliutokomeza kupitia chanjo mwaka 1980. Chanjo zilizofanya kazi dhidi ya ndui pia zinatoa kinga dhidi ya mpox, hasa katika mlipuko wa 2022.
"Siyo kinga kwa 100%, lakini kulingana na mlipuko mkubwa wa 2022 huko Ulaya na Amerika Kaskazini, wazee walikuwa katika hatari ndogo, na hiyo inadhaniwa kuwa ni kwa sababu walikuwa na kinga kutoka chanjo ya ndui," anasema Prof Adam.
Bavarian Nordic ilitoa zaidi ya dozi milioni 15 za chanjo ya MVA-BN - chanjo ya mpox inayotokana na chanjo ya ndui - kwa zaidi ya nchi 76 duniani kote wakati wa mlipuko wa 2022.
Virusi vya mpox hubadilika polepole

Chanzo cha picha, AFP
Baadhi ya Virusi hubadilika haraka kuliko vingine. Ni kwa sababu mpox husababishwa na virusi vya DNA na Covid-19 husababishwa na virusi vya RNA. Virusi vya DNA havibadiliki kwa uhuru kama virusi vya RNA kulingana na wataalamu.
Kuna familia mbili zinazojulikana au makundi ya virusi vya mpox - clade 1 na clade 2. Virusi vya SARS-CoV2 vina zaidi ya makundi 20 yanayojulikana.
Mlipuko wa sasa unasababishwa zaidi na virusi vya clade 1, vinayojulikana kama clade 1b.
Wanasayansi wa WHO wanasema hawajui kama aina ya 1b inasambazwa kwa urahisi zaidi kuliko aina nyinginezo.
Wanachojua ni kwamba katika mlipuko wa hivi sasa watu walioambukizwa huwa tayari wamepata dalili kali wanaripoti kuwa na ugonjwa huo.
Hakuna uwezekano wa karantini

Chanzo cha picha, EPA
Watu wengi wana wasiwasi kwamba kuenea kwa mpox kutasababisha shughuli kufungwa, kama tulivyoona katika janga la Covid.
Ingawa ugonjwa huo umeenea katika mataifa 16 barani Afrika katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, CDC Afrika haipendekezi kufungwa kwa mipaka.
"Afrika CDC, kwa wakati huu na ushahidi tulionao, haishauri kukatizwa kwa safari za watu na bidhaa," anasema Dk Jean Kaseya, mkurugenzi mkuu wa shirika hilo.
"Safari za watu na bidhaa zitaendelea kama ilivyokuwa zamani, wakati tunapambana na janga hili."
Dk Mike Ryan, mkurugenzi mtendaji wa mpango wa dharura wa afya wa WHO, anakubali.
"Mpox ni virusi ambavyo vinaweza kudhibitiwa ikiwa tutafanya mambo kwa njia sahihi kwa wakati unaofaa na kuweka akili zetu zote katika mapambano. Kama tulivyofanya kwa Covid.
Mpox kawaida huwa haina nguvu na watu wengi hupona ndani ya wiki mbili hadi nne. Lakini, watu wengine hupata ugonjwa mbaya na huhitaji kulazwa hospitalini.
Unaweza kujikinga na maambukizi kwa kuepuka kuwasiliana kwa karibu na watu walioambukizwa, vitu au wanyama. Unawaji mikono au kutumia vitakatisha mwili, baada ya kugusa vidonda na majeraha.
"Tunajua kwamba chanjo ni kinga, kwa hivyo tuna zana bora zaidi kwa sasa, kwa virusi visivyoambukiza sana," anasema Prof Rodney. "Kwa hivyo, janga kama Covid nadhani haliwezekani."
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Seif Abdalla