Chadema ya Tundu Lissu itakuwa ya aina gani?

Lissu

Chanzo cha picha, Getty Images

Hatimaye lile ambalo lilikuwa likingojewa kwa muda mrefu sasa limekamilika, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimepata Mwenyekiti mpya, Tundu Antiphas Mughwai Lissu aliyeshinda kwa kura 513 (51.5%), dhidi ya Freeman Aikaeli Mbowe aliyepata kura 482 (48.3%)

Ni baada ya miaka takribani 20 ya uongozi wa Freeman Aikaeli Mbowe, aliyechukua hatamu za kuwa Mwenyekiti wa Chadema tangu 2003. Hata mpinzani wake katika uchaguzi huu Tundu Lissu, amekiri, kukuwa kwa Chadema kunatokana na kazi kubwa iliyofanywa na Mbowe.

Bila shaka ni jambo la kushukuru kwa wafuasi wa Chadema kwamba kamera za vyombo vya habari hazijanasa matukio ya watu wakishika vikosi katika uchaguzi huu; kwa jinsi ushindani, malumbano na maneno yalivyokuwa mengi, hatimaye uchaguzi umekwenda vyema, na Freeman Mbowe amekubali kushindwa na kumpongeza Lissu, ni kiashiria cha ukomavu wa kisiasa.

Unaweza kusoma

Kupitia Chadema, Lissu ameshika nyadhifa nyingi; ikiwemo Mbunge wa Singida Mashariki, Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Makamu mwenyekiti wa Chadema upande wa Bara, na sasa ni Mwenyekiti.

Kama ilivyo kwa ushindi wowote, kwanza ni furaha lakini kisha, ni kukabiliana na majukumu ya kiuongozi. Swali ambalo wengi sasa wanajiuliza: Je, Lissu atailetea nini Chadema? Pia atakabiliana vipi na changamoto zijazo na zile ambazo tayari ziko mbele yake?

Maridhiano ndani ya chama

Akizungumza katika mkutano mkuu jana, Lissu amesema "nimekaa na mwenyekiti (Mbowe) kwa zaidi ya miaka 20, hatujawahi kugombana, hatujawahi kukosana. Ndio tumetofautiana misimamo, lakini hatujawahi kugombana na hili litaendelea baada ya leo."

Lakini ndiye Lissu huyo huyo ambaye katika mahojiano ya BBC Swahili, alipoulizwa kuhusu uhusiano wake na Mbowe alisema. "Tukikutana hivi, hatupigani ngumi. Lakini uhusiano haupo kama mwanzoni."

Pia akarusha mawe kwa Mbowe kwa kusema, "kugombea kwangu namuokoa Mbowe, namsaidia Mwenyekiti Mbowe kulinda urithi wake. Kuna hatari ya kutoka kuwa Mugabe 'mpigania uhuru' na kuwa 'Mugabe dikteta, rais wa maisha.' Haipaswi kuondoka kwenye madaraka kwa kukufukuzwa kwa sababu watu wamekuchoka."

Kauli hizi zilitoa ishara kuwa mambo kati ya watu hawa wawili hayakuwa sawa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi wa kumsaka mwenyekiti, na hivyo juhudi za makusudi za kuurudisha uhusiano uliotetereka, hazina budi kufanyika kwa faida ya chama.

Vilevile, Mbowe ana wafuasi wengi na bado ushawishi wake ni mkubwa ndani ya Chadema, ana kundi kubwa la watu wanaomuunga mkono, ndio maana hata katika uchaguzi huu, hakupata kura sifuri, kura alizopata ni kielelezo tosha juu ya ukubwa wa jina lake ndani ya chama.

Mbowe pia ameeleza wazi kuwa Chadema imeachwa na majeraha makubwa kutokana namna kampeni za uchaguzi huo zilivyoendeshwa na amemtaka Lissu na viongozi wengine wapya kuleta maridhiano.

Lissu

Chanzo cha picha, Getty Images

Kwa kuzingatia hilo, Lissu kama Mwenyekiti atakuwa na kazi ya kuyaleta pamoja makundi haya mawili, yaani kundi lake na lile na Mbowe. Na kuhakikisha Mbowe na wafuasi wake wanaendelea kutoa mchango wao wa hali na mali katika kuendesha shughuli za chama hicho.

Mpasuko ndani ya chama hudhoofisha chama chochote kile kinachotaka wafuasi wengi wa kukipigia kura na kupata ushindi katika chaguzi.

Atapambana vipi na rushwa?

Januari 17 mwaka huu wakati akizungumza katika mdahalo wa kisiasa, Tundu Lissu alisema, "mimi ndiye niliyekuwa wa kwanza, kupuliza filimbi kwamba kuna rushwa kwenye chaguzi zetu (Chadema). Tuna tatizo. Muda huu tunapozungumza, kuna wajumbe wanasafirishwa, wanawekwa kwenye mahoteli, makambi, wanapewa pesa, wanalishwa na wagombea. Kuna uchafuzi wa aina hiyo, unoafanywa na wagombea na wapambe wao."

Hili ni tatizo ambalo wakati fulani huko nyuma lilizungumzwa pia. Mwezi Mei 2020, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), ilitangaza kuanzisha uchunguzi kuhusu tuhuma za matumizi mabaya ya fedha ndani ya Chadema.

Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo alieleza, "kwa mujibu wa taarifa tulizo nazo, kuna matumizi mabaya ya fedha za michango ya wanachama, ambayo kwa mujibu wa katiba yao wanadai imeanishwa wachangie. Lakini, matumizi yake ndio wanatilia mashaka, kuna fedha nyingi zinatumika ndivyo sivyo, nje ya makubaliano yao. Kwa hiyo, tunachunguza matumizi yasiyo sahihi ya fedha zao."

Ikiwa ufisadi ama rushwa ni tatizo ambalo lipo ndani ya Chadema na lipo kwa muda mrefu, ni matarajio ya wengi kwamba hii itakuwa ni kazi nyingine kubwa ambayo Lissu inamngoja mbele yake.

Uhusiano wa upinzani na serikali

Moja ya hoja ambayo Lissu ameitumia kumkosoa Mbowe, ni namna alivyokuwa akiendesha siasa zake na serikali. Kwa lugha nyingine, Lissu alimwona Mbowe amekuwa laini mbele ya chama tawala na serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan.

"Mwenyekiti aliyekwenda gerezani, si mwenyekiti aliyetoka gerezani miezi minane baadaye. Yule aliyetoka gerezani alikuwa tofauti, akiimba maridhiano anaimba mapendano," alisema Lissu.

Alipoulizwa na BBC juu ya mwelekeo wake mpya wa kisiasa na utakuwa na tofauti gani na hali ya sasa. Tundu Lissu amesema:

"Ni mwelekeo wa harakati za mapambano ya demokrasia, hakuna tena kuimbiana habari ya maridhiano yasiyokuwepo, hakuna habari ya kualikana kuzungumza mambo yasiyojulikana. Nia mapambano ya kudai mabadiliko. Na zitakuwa ni siasa za mshike mshike kweli kweli. Ndio historia ya mapambano ya kidemokrasia ilivyo dunia nzima."

Chadema kama vilivyo vyama vingine vya upinzani, inapigia upatu kuwepo kwa katiba mpya, tume huru ya uchaguzi, inataka uchaguzi huru na haki mwishoni mwa mwaka huu, bila ya wagombea wao kuenguliwa bila sababu za maan, pia inataka viongozi na wafuasi wake wasibughudhiwe na vyombo vya dola wanapokuwa kwenye shughuli zao za kisiasa.

Katika nchi yenye demokrasia inayoeleweka, yumkini hayo sio mambo ambayo utawala unapaswa kuyatoa kama huruma kwa vyama vya siasa, ni mambo ambayo yapo kikatiba na kisheria, bahati mbaya utawala nchini Tanzania – kama ilivyo kwa tawala nyingine nyingi duniani – hautendi haki wakati wote. Kuna nyakati za vuta ni kuvute, pingu kiunoni na kirungu mkononi.

Maswali yanayoibuka kwa muktadha huo: Je, Chadema chini ya Lissu itahitaji kuwa na uhusiano au ushirikiano na utawala ili kuyafanikisha hayo? Au ina uwezo wa kuyafanikisha bila ya mwingiliano wowote na upande wa serikali?

Lissu baada ya kuibuka na ushindi leo alianza hotuba yake kwa kusema, atazungumza kwa kuchagua maneno yake kwa uangalifu, na kweli akafanya hivyo. Je, tutarajie Lissu ambaye ataendelea kuchagua kauli zake hata akiwa katika harakati dhidi ya chama tawala na serikali yake?

Bila shaka, Lissu kwa sasa ndiye mmiliki wa jawabu ya maswali haya yote.