'Mchumba wangu mtarajiwa kutoka Kenya alinilaghai pauni elfu 85'

Chanzo cha picha, Rodrick Lodge
Mjane aliye katika mazingira magumu ameachwa bila makao na "anateseka kweli" baada ya kushawishiwa kutuma pauni 85,000 kwa mwanamke ambaye hakuwa mtu halisi-alikuwa mtu feki.
Rodrick Lodge, 69, alikuwa akiishi Leiston, Suffolk, wakati rafiki yake ambaye alikuwa amekutana naye miaka mitatu kabla nchini Kenya alipowasiliana na "mwanamke" anayeitwa Anita.
Baada ya kujenga uhusiano kupitia mitandao ya kijamii, alijihisi kuanza penzi kwa mara ya kwanza tangu kifo cha mkewe Pauline mnamo 2019, na baadaye akakubali kuhamia Nairobi kumuoa.
Lakini kile ambacho Bw Lodge alikuwa akitaka ni ulaghai mkubwa, ambao hatimaye ungesababisha akiba yake yote ya maisha kupotea kutoka kwa benki yake na kumuacha bila chochote.

Chanzo cha picha, Contributed
"Alisema alikuwa na nyumba yenye vyumba vinne lakini ili kuoa ningehitaji kulipa mahari, kwa hivyo nilikubali kumjengea nyumba yake, hayo ndiyo yalikuwa makubaliano," alisema Bw Lodge, ambaye awali aliishi Surrey.
“Kwa hiyo, nilianza kumtumia pesa kwa ajili ya ujenzi wa sehemu mbalimbali za nyumbani na alikuwa akinitumia picha za nyumba hiyo ikiboreshwa, pamoja na picha nyingine za ndani.
"Aliniambia kuwa alikuwa mkurugenzi mkuu wa kampuni ya bidhaa za urembo iliyokuwa na wafanyakazi wapatao 30, hivyo nilifikiri alikuwa mwanamke mwenye mali."
Bw Lodge alitambua tu kilichotokea wakati ulipofika wa kusafiri hadi Kenya ili kuungana na mwanamke ambaye alifikiri kuwa alikuwa mpenzi wake mpya na mke mtarajiwa.
Lakini alipotua kwenye uwanja wa ndege, hakumpata, na kila alipokuwa akijaribu kumtafuta aliambiwa visingizio vya mara kwa mara.

Chanzo cha picha, Contributed
Baada ya kufanya upelelezi , Bw Lodge aligundua kuwa yule mwanamke anayejifanya Anita alikuwa ni rafiki yake ambaye ndiye aliyewakutanisha kwanza.
"Makubaliano yalikuwa kwamba tungekutana Nairobi, lakini hilo halikufanyika na ikawa ni ulaghai na Anita hakuwahi kuwepo," aliongeza mfanyakazi huyo wa zamani wa Umoja wa Mataifa.
"Yeye ndiye mbaya zaidi, lakini nilikuwa mjinga na mpumbavu, najua hilo, na sasa ninalipa gharama mbaya sana. Ninaamini kweli alikuwepo. Nina aibu."
Baada ya kurejea Uingereza, Bw Lodge alilala katika Uwanja wa Ndege wa Heathrow kwa siku tatu. Sasa anaishi katika makazi ya watu wasio na makazi huko Woking na alisema hana matumaini ya siku zijazo.
Bw Lodge alisema: "Baada ya kumpoteza mke wangu, mtu muhimu zaidi maishani mwangu, nilikuwa hatarini sana kwa sababu nilitaka mpenzi na ubora wa maisha.
"Sasa hii imeharibu maisha yangu ya baadaye - sina maisha sasa na sina cha kustahimili. Sina familia, ni marafiki wachache tu wanaoniita mjinga.
"Kwa kweli ninateseka kwasababu sina pesa. Amechukua kila senti niliyokuwa nayo na hivyo ninatumai kweli kwamba mwanamke huyu mwovu ataozea kuzimu - samahani kusema hivyo, lakini ninamwaanisha hivyo."
Kituo cha kitaifa cha kuripoti ulaghai na uhalifu mtandaoni nchini Uingereza, Action Fraud, kimetoa ushauri wa jinsi ya kumgundua " mlaghai ya mapenzi ".
Kilisema ni muhimu, haijalishi umezungumza kwa muda gani na mtu ambaye hujakutana naye ana kwa ana, usimpe pesa.
Pia kilionya dhidi ya kuruhusu ufikiaji wa benki, kuchukua mkopo kwa ajili ya mtu usiyemjua, kutoa nakala za hati za kibinafsi au kukubali kupokea au kutuma vifurushi kwa niaba ya walaghai.
Waathiriwa wa ulaghai wa mapenzi wanapaswa kuwasiliana na benki yao mara moja na kuripoti kwa Action Fraud, kupitia actionfraud.police.uk au kwa kupiga simu nambari 0300 123 2040.
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Yusuf Jumah