Mbegu za kiume zamsaliti mwanaume aliyemuua mtalaka wake baada ya miaka 45

Chanzo cha picha, NEWSLINE MEDIA
Polisi wamemkamata na kumfungulia mashitaka mwanaume mmoja ambaye amekuwa akitoroka kwa miaka 45 baada ya kumuua mke wake wa zamani huko Scotland.
Christopher Harrison anatokea Aberdeen kaskazini-mashariki mwa Scotland. Alimuua mke wake mwaka 1978, mwaka mmoja baada ya kuachana na mke wake huyo, Brenda Page.
Mmoja wa wachunguzi katika kesi hiyo James Callender alieleza jinsi walivyompata muuaji wa Brenda Page.
“Alidhani anatoroka mkono wa sheria. Lakini katika kuhojiwa bila ya kujua alikiri,” alisema James.
Miaka 45 baada ya kifo cha Brenda Page, Harrison amekamatwa na kuhukumiwa.
Baada ya miongo mitatu

Filamu ya BBC inayoangazia mauaji haya imetolewa. Filamu hiyo iliyopewa jina la The Killing of Dr. Brenda Page, inaanza na picha za kukamatwa kwa Harrison mwaka 2020.
Katika tukio la ufunguzi, Harrison anasikika akisema, 'Hakuuawa hapa,' huku polisi wakimwendea.
Dkt. Brenda Page, mtaalamu wa vinasaba, alipatikana akiwa amevuja damu hadi kufa kitandani mwake Julai 14, 1978.
Hapo awali ilishukiwa kuwa mume wake wa zamani Harrison inawezekana kamuua. Polisi walimkamata saa chache baada ya mauaji hayo.
Lakini upelelezi wa kesi hiyo ulipokuwa ukiendelea, polisi hawakuweza kupata ushahidi wowote kwamba alifanya mauaji hayo.
Polisi Scotland na vyombo vya habari waliendelea kutafuta ushahidi wa mauaji hayo. Lakini kwa muda mrefu hakukuwa na mtuhumiwa wa mauaji hayo.
Baada ya hapo, kesi hiyo iliahirishwa. Lakini mwaka 2015, polisi waliamriwa kuchunguza tena kesi hiyo.
Ushahidi Mpya

Chanzo cha picha, PAGE FAMILY
Polisi walichunguza tena kesi hiyo na kukusanya ushahidi kutoka katika nyumba ya Brenda Page. Doa la manii lilipatikana kwenye blanketi. Mbegu hizo zililinganishwa na DNA ya Harrison.
Katika uchunguzi ya awali, Harrison alisema hakufanya mapenzi na Brenda. Katika uchunguzi wa pili polisi waliamua kuna ushahidi mkubwa kwamba manii ni yake.
Machi 27, 2020, Harrison alikamatwa tena na kuhukumiwa.
Harrison alishikilia kwamba hahusiki na mauaji ya mke wake wa zamani. Kwa vile ushahidi ulikuwa na nguvu, kesi ya mauaji ilisajiliwa dhidi yake.
Hatimaye, Machi 2023 baada ya kesi ya siku 10. Harrison alipatikana na hatia ya kumuua mke wake wa zamani, Brenda Page. Mahakama ilimhukumu kifungo cha maisha jela. Harrison anaweza kuomba msamaha baada ya kutumikia kifungo cha miaka 20 jela.
Afisa wa polisi aliyechunguza kisa hicho Callender alizungumza na BBC na kusema, ''hakutarajia kwamba Harrison angekamatwa na kufungwa kwa mauaji ya mke wake wa zamani, Brenda Page.''
“Ukiona jinsi polisi walivyomhoji mbele ya kamera za video, utaelewa yeye mwenyewe anakiri kosa, ndiye anayehusika na mauaji hayo,” alisema.
Maisha ya Harrison na Brenda

Harrison na Brenda Page, walioana 1972. Brenda alikuwa akiwaambia marafiki zake wa karibu kuwa hana furaha katika maisha yake ya ndoa. Akisema kuwa anaogopa kuonana na mumewe.
Baada ya miaka minne, waliachana. Brenda Page alinunua nyumba yake mwenyewe katika jumba la ghorofa.
Wanafamilia wa Brenda Page walisema Harrison aliendelea kumnyanyasa Brenda hata baada ya talaka. Wanafamilia wa Brenda walisema Brenda aliwaambia kuwa Harrison anamtuhumu kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wanaume wengine.
Mwanafamilia wa Brenda mwenye umri wa miaka 59, Chris Ling, alikuwa akienda mahakamani kila siku wakati wa kesi hiyo.
"Ni hisia za ajabu sana. Mwanaume anayetuhumiwa kumuua shangazi yangu amekuwa nasi kwa miaka mingi. Alikuwa mbele ya macho yetu," Ling aliiambia BBC.
Alielezea furaha kuwa kutokana na maendeleo ya teknolojia ya DNA, mshtakiwa sasa anaweza kutambuliwa.
Tangu kuanza kwa uchunguzi wa kesi hii, polisi waliwahoji mashahidi 4000. Takriban taarifa 500 zilirekodiwa za kesi hiyo.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah