Tanzania: Wanne waliombaka na kumlawiti binti mmoja wahukumiwa maisha jela

Na Ronald Sonyo akiwa Dodoma &

Yusuf Jumah akiwa Nairobi

TH

Chanzo cha picha, Ronaldo Sonyo

Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma imewahukumu kifungo cha maisha jela watuhumiwa wanne kwa kesi ya ubakaji na ulawiti kwa kundi dhidi ya binti wa Yombo Dovya jijini Dar es salaam

Nje ya Mahakama hiyo wakili anayetetea watuhumiwa , Godfrey Wasonga amesema hawakuridhishwa na hukumu hiyo kwani kuna baadhi ya vifungu vimekiukwa.

Hata hivyo, licha ya wanne hao kuhukumiwa pia wametakiwa kulipa kiasi cha shilingi milioni moja kwa kila mmoja kwa muathiriwa wa tukio hilo.

Uamuzi huo ulitolewa katika Kesi ya Jinai namba 23476 ya mwaka 2024, ambapo watu waliohukumiwa walitambuliwa kuwa MT 140105 Clinton Damas, anayejulikana pia kama "Nyundo," askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ); C.1693 Askari Magereza Praygod Mushi; Nickson Jackson, anayejulikana pia kama "Machuche"; na Amin Lema, anayejulikana kwa jina la "Kindamba."

Kisa kilichozua hasira mitandaoni

th

Chanzo cha picha, Tanzania Police

Kisa cha binti huyo kilisababisha Kamanda wa polisi katika mji mkuu wa Tanzania, Dodoma, kuondolewa kwenye wadhifa wake kufuatia matamshi ya kutatanisha ambapo alimhusisha mwathiriwa anayedaiwa kubakwa na genge na biashara ya ngono.

Mapema mwezi Agosti, video iliyokuwa ikionyesha msichana akishambuliwa ilisambaa, na kusababisha kilio katika taifa hilo la Afrika Mashariki.

Baadaye jeshi la polisi nchini humo lililazimika kuomba radhi kuhusu matamshi ya kamanda huyo na kuahidi uchunguzi wa kina .

"Jeshi la polisi linapenda kuomba radhi kwa kila mtu ambaye aliguswa na kukerwa na taarifa hiyo inayosambazwa kwenye vyombo vya habari wakati ufuatiliaji ukifanyika ili kupata usahihi wake," msemaji wa polisi wa taifa David Misime alisema wakati huo .

Bw Msime aliongeza kuwa katika maoni yake kwa gazeti la ndani la Mwananchi, Kamanda wa Mkoa wa Dodoma, Theopista Mallya alisema hata kama mwanamke huyo alikuwa mfanyabiashara ya ngono, "hakustahili kutendewa hivyo".

Maneno hayo hata hivyo hayakuonekana kwenye ripoti ya Mwananchi- BBC iliwasiliana na gazeti hilo kwa ufafanuzi.

Akijibu ripoti ya Mwananchi, wakili Peter Madeleka alisema kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba maoni ya Bi Mallya yalikuwa ni "ushahidi wa ukatili wa polisi kwa haki za wanawake".

Fatma Karume, mwanasheria na mwanaharakati maarufu, naye alionyesha kukerwa na kuandika kwenye X: "Wanaojiuza hawawezi kubakwa katika nchi hii");