'Meneja wa benki yangu aliiba $1.9m kutoka kwa akaunti yangu'

Chanzo cha picha, SHVETA SHARMA
Na Geeta Pandey
BBC News, Delhi
Mwanamke mmoja wa Kihindi amemshutumu meneja katika mojawapo ya benki kubwa nchini humo kwa kumlaghai rupia 160m ($1.9m; £1.5m) kutoka kwenye akaunti yake.
Shveta Sharma anasema alikuwa amehamisha pesa kwa benki ya ICICI kutoka kwa akaunti yake ya Marekani, akitarajia kuwekezwa katika amana za kudumu.
Lakini anadai kuwa afisa wa benki aliunda "akaunti bandia, akaghushi saini yake, akatoa kadi za benki na vitabu vya hundi kwa jina lake" ili kutoa pesa kutoka kwa akaunti yake.
"Alinipa taarifa ghushi, akaunda kitambulisho ghushi cha barua pepe kwa jina langu na akabadilisha nambari yangu ya simu kwenye rekodi za benki ili nisipate arifa zozote za utoaji fedha," aliambia BBC.
Msemaji wa benki hiyo aliambia BBC kwamba "hakika ulaghai huo ulifanyika" lakini akasema kwamba ICICI "ni benki yenye sifa ambayo inaweka matrilioni ya amana kutoka kwa mamilioni ya wateja".
“Yeyote atakayehusika ataadhibiwa,” aliongeza.
Bi Sharma na mumewe, ambao walirejea India mwaka 2016 baada ya kuishi kwa miongo kadhaa Marekani na Hong Kong, walikutana na mfanyakazi wa benki kupitia rafiki yake.
Kwa vile kiwango cha riba cha amana za benki nchini Marekani kilikuwa kidogo, alimshauri Bi Sharma kuhamisha pesa zake hadi India ambako amana za kudumu zilikuwa zikitoa riba ya 5.5% hadi 6%.
Alifungua akaunti ya NRE iliyokusudiwa Wahindi wasio wakaaji kwa ushauri wake baada ya kutembelea tawi la ICICI huko Gurugram karibu na mji mkuu, Delhi, na mnamo 2019, alianza kuhamisha pesa kutoka kwa akaunti yake ya Marekani.
"Katika kipindi cha miaka minne kuanzia Septemba 2019 hadi Desemba 2023, tuliweka akiba yetu yote ya maisha ya karibu rupia milioni 135 kwenye benki," alisema, na kuongeza kuwa "pamoja na riba, jumla hiyo ingekua zaidi ya rupia 160m".
Alisema hakuwahi kushuku kuwa kuna kitu kibaya kwa sababu meneja wa tawi "alikuwa akinipa stakabadhi sahihi za amana zote za benki, mara kwa mara kunitumia taarifa za barua pepe kutoka kwa akaunti yake ya ICICI na wakati mwingine hata kuja na makabrasha ya risiti".
Ulaghai huo ulikuja kujulikana mapema Januari wakati mfanyakazi mpya katika benki hiyo alipojitolea kumpatia Bi Sharma kiasi bora zaidi cha riba kwa fedha zake.
Hapo ndipo alipogundua kuwa amana zake zote za kudumu zimetoweka. Pia kulikuwa na mkopo wa rupia 25m zilizochukuliwa kwenye moja ya amana.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Mimi na mume wangu tulishtuka. Ninaugua ugonjwa wa autoimmune na niliumia sana hivi kwamba sikuweza kuamka kutoka kitandani kwa wiki nzima," aliniambia. "Maisha yako yanaharibiwa mbele ya macho yako na huwezi kufanya chochote juu yake."
Bi Sharma anasema ameshiriki habari zote na benki hiyo na kufanya mikutano kadhaa na maafisa wakuu.
"Katika mkutano wetu wa kwanza tarehe 16 Januari, tulikutana na wakuu wa benki wa mikoa na kanda na mkuu wa kitengo cha ulinzi wa ndani wa benki ambaye alitoka Mumbai kwa ndege, walituambia walikubali kuwa ni kosa lao kwamba meneja wa tawi alitudanganya .
"Walituhakikishia kwamba tutarejeshewa pesa zetu zote. Lakini kwanza, walisema, walihitaji msaada wangu katika kubaini miamala ya ulaghai."
Bi Sharma na timu yake ya wahasibu walitumia siku nzima kupitia taarifa kwa miaka minne iliyopita. Wahasibu wake kisha walikaa na timu ya uangalizi kuashiria miamala ambayo "walikuwa na uhakika wa 100%" ilikuwa ya ulaghai.
"Ilishangaza kugundua jinsi pesa zilivyochukuliwa kutoka kwa akaunti yangu na zilitumika wapi."
Bi Sharma anasema licha ya hakikisho la benki hiyo kwamba suala hilo litasuluhishwa ndani ya wiki mbili, zaidi ya wiki sita baadaye, bado anangoja kuona pesa zake zikirejeshwa.
Wakati huo huo, ametuma barua kwa Afisa Mkuu Mtendaji na naibu wake katika benki ya ICICI na kuwasilisha malalamiko kwa Benki Kuu ya India - na Kitengo cha Kuchunguza Makosa ya Kiuchumi (EOW) pamoja na polisi wa Delhi, ambayo inashughulikia kesi hiyo.
Katika taarifa iliyotumwa kwa BBC, benki hiyo ilisema imejitolea kuweka rupia 92.7m kwenye akaunti yake kwa njia ya malipo, ikisubiri matokeo ya uchunguzi.
Lakini Bi Sharma amekataa ofa hiyo: "Ni kiasi kidogo sana kuliko rupia 160m ninazowadai na hatua hiyo itamaanisha kwamba akaunti hiyo itafungiwa hadi kesi hiyo ifungwe na polisi, ambayo inaweza kuchukua miaka."
"Kwa nini ninaadhibiwa kwa kosa lisilo langu? Maisha yangu yamebadilika- Siwezi kulala. Nina ndoto mbaya kila siku," aliongeza.

Chanzo cha picha, Getty Images
Srikanth L, ambaye anaendesha shirika la uangalizi wa fintech liitwalo Cashless Consumer, anasema visa kama hivyo si vya kawaida sana na benki hutumia ukaguzi ili kuhakikisha mambo kama haya hayafanyiki.
Lakini meneja wako wa benki akiamua kukulaghai, anasema, kuna mambo machache unayoweza kufanya.
"Kwa kuwa alikuwa meneja wa benki, alimuamini kabisa. Lakini wateja lazima wawe waangalifu zaidi. Ni lazima wafuatilie uhamisho wa pesa kutoka kwa akaunti zao kila wakati.
"Kukosekana kwa njia ya kuthibitisha mara mbili kwa upande wa mteja kunaweza kusababisha aina hii ya udanganyifu," anaongeza.
Hii ni mara ya pili mwezi huu kwa benki ya ICICI kujipata ikiangaziwa kwenye vyombo vya habari kwa sababu zisizo nzuri.
Mapema mwezi huu, polisi katika jimbo la Rajasthan walisema meneja wa tawi na wasaidizi wake walidanganya waweka amana na kuwaibia mabilioni ya rupia kwa miaka ili kufikia malengo yaliyowekwa na benki.
Polisi walisema walitoa pesa kutoka kwa akaunti za wateja na kuzitumia kufungua akaunti mpya na za akiba na kuweka amana za kudumu.
Msemaji wa ICICI alisema katika kesi hiyo, benki ilichukua hatua haraka na kuchukua hatua dhidi ya meneja aliyehusika. Aliongeza kuwa hakuna mteja aliyepoteza pesa.
Katika kesi ya Bi Sharma, alisema ilikuwa "inastaajabisha" kwamba alibaki "hajui kuhusu miamala hii na salio katika akaunti yake katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, na hivi majuzi tu aligundua hitilafu katika salio la akaunti yake".
Meneja wa tawi anayetuhumiwa "amesimamishwa kazi, akisubiri uchunguzi", alisema, na kuongeza "pia tumetapeliwa".
"Pia tumepeleka malalamiko kwa EOW na inabidi tusubiri mpaka upelelezi wa polisi ukamilike. Atarejeshewa fedha zake zote pamoja na riba, mara baada ya kuthibitishwa kuwa madai yake ni ya kweli. Lakini kwa bahati mbaya anatakiwa subiri."
BBC haikuweza kuwasiliana na meneja kwa maoni.