Je, mashambulizi ya makombora ya Iran na Israel yameibadilisha Mashariki ya Kati?
Na James Landale,
BBC News, Jerusalem

Chanzo cha picha, AFP/Getty
Habari za Mashariki ya Kati hubadilika haraka. Wakati mmoja ni kuhusu mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani kati ya Iran na Israel. Kichwa cha habari kinachofuata kinarejea tena kwenye mapigano na mateso huko Gaza.
Lakini watunga sera, wachambuzi na viongozi wa kijeshi bado wanatafakari hatua makabiliano yaliyo ya kawaida siku chache zilizopita kati yya mahasimu wawili wa zamani, ambayo bila shaka yalikaribia kusababisha mzozo mbaya wa kimataifa.
Inafaa kuzingatia jinsi walivyokaribia kupigana . Hii ilikuwa mara ya kwanza Iran na Israel kushambuliana moja kwa moja.
Baadhi ya wachambuzi wanasema shambulio hilo la Iran lilikuwa shambulio kubwa zaidi la kombora na ndege zisizo na rubani kuwahi kutokea - kubwa kuliko shambulio lolote ambalo Urusi imewahi kulifanya dhidi ya Ukraine. Hakika lilikuwa ni shambulio la kwanza la nje la Israel tangu yalipofanyika makombora ya Scud ya Saddam Hussein mwaka 1991.
Nyingi za ndege zisizo na rubani 300 pamoja na makombora ya Iran yaliangushwa au kukomea njiani.
Lakini nilitazama nikiwa ofisini kwetu Jerusalem jinsi anga usiku ule lilivyowashwa na walinzi wa anga wa Israel wakijaribu kuangusha makombora ya balestiki yaliyokuwa yakipaa juu angani.
Haya yote yalitekelezwa na mfumo mmoja wa GPS ambao uliweza kuzuia kombora kutua katika eneo la mjini na kusababisha hasara kubwa kwa raia.
"Sidhani kama watu walitambua jinsi tulivyokuwa karibu na wikendi ," afisa mmoja mkuu wa usalama wa Magharibi aliniambia. "Inaweza kuwa hadithi tofauti sana."

Bado baadhi ya nchi za Magharibi bado zinahisi kuwa kuna masuala chanya yanayoweza kupatikana kutokana na shambulio la Aprili 13 na ulipizaji kisasi wa kiwango kidogo wa Israeli wiki iliyopita.
Wanasema kuwa yalikuwa mafanikio makubwa ya kiintelijensia kutabiri shambulio la Iran, kwamba ulinzi wa Israel ulikuwa mfano bora wa ushirikiano wa kijeshi wa washirika, na kwamba Iran na Israel zilijifunza jinsi ya kuchochea na kuzuia mapigano.
Wacha tuchukue operesheni ya ujasusi kwanza.
Nimeambiwa Marekani ilifahamu kuhusu mipango ya Iran siku ya Jumatano asubuhi kabla ya shambulio la Jumamosi jioni. Na muhimu zaidi, waligundua ukubwa wa azma ya Iran.
"Tulipata taarifa kwamba jibu la Iran lingekuwa kinyume cha matarajio," kilisema chanzo kimoja cha ngazi ya juu cha Magharibi. " Ilisababisha mshituko kidogo. Lakini ilisaidia kuratibu mwitikio wa kimataifa."
Kwa bahati mbaya, ilisaidia Marekani kuzishawishi baadhi ya nchi za Ghuba kujiunga na ulinzi wa Israel, zikiwemo Jordan na Saudi Arabia.
Hofu yao - mara tu walipofahamu ukubwa wa mipango ya Iran - ilikuwa hatari ya vita vya kikanda vilivyozidi ikiwa Israeli haikuwa na chaguo ila kulipiza kisasi vikali. Kwa hivyo mchanganyiko wa mkusanyiko mzuri wa ujasusi na ishara ya kibinafsi iliyotolewa na Iran iliipa Israeli na washirika wake wakati wa kujiandaa.
Majukumu ya Jordan na Saudi Arabia bado hayako wazi kabisa. Jordan imekiri kudungua ndege zisizo na rubani za Iran katika kujilinda ili kulinda mamlaka yake. Inaeleweka Jordan pia iliruhusu baadhi ya ndege za kivita za Israel kulifikia anga lale.
Wasaudia hao wanadhaniwa kutoa taarifa kwa Marekani na kufuatilia kwa karibu tisho lolote kutoka kwa makundi yenye silaha yanayoungwa mkono na Iran nchini Yemen.
Suala kuu ni kwamba hili lilifanikiwa. Wanajeshi wa Marekani, Uingereza, Ufaransa, Jordan na Saudia walionyesha kuwa wanaweza kufanya kazi pamoja katika ulinzi wa anga wa pamoja.
"Ilikuwa operesheni ya mbinu iliyofanikiwa sana," kilisema chanzo cha usalama. "Taarifa za kijasusi zilidhibiti, tuliona eneo lote na tulifanya kazi pamoja. Hakuna kundi lingine la mataifa linaweza kufanya hivyo duniani." Wengine pia wamedai kuwa huu unaweza kuwa mwanzo wa muungano mpya wa kikanda dhidi ya Iran. Ingawa kwa wengine, huo ni mtazamo tu wa kawaida wa usalama na wa kijeshi, unaosherehekea mafanikio ya kiteknolojia huku ukikosa taswira kuu ya kisiasa.
Wachambuzi walio na matumaini zaidi wanasema kwamba ikiwa Iran ilitaka kusababisha maafa makubwa kwa Israeli, ingeweza kujizuia kutoa onyo la mapema, kupanua malengo yake, kuanzisha wimbi la pili la mashambulizi - au hata kuwaamuru Hezbollah kufanya mashambulizi makubwa kutoka Lebanon.
Emile Hokayem kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Mafunzo ya Kimkakati alisema operesheni hiyo ilifichua ni kiasi gani Israel ilipaswa kutegemea washirika kwa ajili ya ulinzi wake. Pia alijiuliza ikiwa Israel itakuwa na makombora ya kutosha ya ulinzi wa anga yanayohitajika kwa mzozo wa hali ya juu zaidi.
"Kama tulivyoona katika vita kati ya Ukraine na Urusi, katika ni muhimu kufahamu ni kiasi gani cha vitu vizuri ulivyo navyo," alisema.

Chanzo cha picha, Reuters
Bw Hokayem pia alipuuzilia mbali wazo kwamba mgogoro huu uliashiria mwanzo wa muungano mpya wa kijeshi wa kikanda.
"Hatuko kwenye kilele cha enzi mpya," alisema. "Mataifa ya Kiarabu yameshirikiana kwa sababu kimsingi yanataka kuepusha makabiliano ya kikanda. Na yanataka kuonyesha kwamba wao ni washirika wazuri kwa washirika wao wa magharibi. Pia ni suala la uhuru wa kitaifa.
Hawataki vitu kupaa na kulipuka katika anga za nchi zao."
Madai ya pili ya watu wenye matumaini ni kwamba Iran na Israel wamejifunza kutokana na uzoefu huu.
Iran iliweza kuishambulia Israel lakini iliwaonya washirika wake kuhusu nia yake na kuashiria mapema kuwa ilikuwa ni ya moja kwa moja.
Israel ilionyesha inaweza kulipiza kisasi kwa unyenyekevu, ikilenga ulinzi wa anga katikati mwa Iran na kutumia shambulio dogo kuashiria uwezo mkubwa zaidi, yaani kwamba inaweza kuipiga Iran wapi na wakati inapotaka.
Nimeambiwa Iran inaweza kuwa hata ilidokezewa kuhusu kulipiza kisasi kwa Israeli. Kwa hakika Iran iliashiria mapema sana kuwa haikukusudia kujibu mashambulizi ya Israel.
Pande zote mbili hakika zitakuwa zimejifunza masomo ya kijeshi. "Huenda shambulio hilo liliisaidia Iran kutambua nguvu na udhaifu wa mfumo wa ulinzi wa anga wa Israeli," Taasisi ya Utafiti wa Vita ilisema. Israel na Marekani pia zitakuwa na uelewa mkubwa wa mikakati ya kimbinu ya Iran.
Hoja ya inayoweza kupingwa ni kwamba Iran na Israel zinafahamu kwamba mashambulizi ya moja kwa moja sasa ni chaguo rahisi.
Katika insha ya Masuala ya Kigeni, Afshon Ostovar kutoka Taasisi ya Utafiti wa Sera za Kigeni anasema ukubwa wa mashambulizi ya Iran unaonyesha kuwa haiwezi kubana na sera ya kujizuia kufanya mashambulizi iwapo ingetaka kuyafanya.
"Wazo kwamba Iran ilianzisha mashambulizi dhaifu kimakusudi sio la halihitaji kuchunguzwa ," anaandika. "Iran ilitarajia Israel ipate kipigo kikubwa."
Bw Hokayem anapinga wazo ambalo Iran na Israel zimejifunza kuelewana. Anatoa mfano wa Israel wa kushindwa kutambua matokeo ya uamuzi wake wa kuwaua makamanda kadhaa wakubwa wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran (IRGC) katika ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus.
Labda somo muhimu walilojifunza na wengi katika mzozo huu lilikuwa ni jinsi eneo hilo lilikaribia kuingia katika vita kamili.
"Ilikuwa kitulizo kikubwa," mwanadiplomasia mmoja wa Magharibi aliniambia. "Mambo yangekuwa tofauti."
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Yusuf Jumah