Je, waliokatiza masomo kutokana na ujauzito ujasiriamali ndio suluhu?

Hawa ni baadhi ya wasichana waliopata mimba za utotoni na watoto wao siku ya mahafali
Maelezo ya picha, Hawa ni baadhi ya wasichana waliopata mimba za utotoni na watoto wao siku ya mahafali

Wasichana 23 waliokatiza masomo yao kutokana na mimba za utotoni hatimaye wamehitimu mafunzo mbalimbali ya ujasiriamali huko Mkoani Arusha, nchini Tanzania.

Baadhi ya wasichana hao wamejifunza upishi, huku wengine wakipata mafunzo ya ushonaji na kusuka nywele baada ya kupata msaada wakiwa na watoto wao katika kituo cha Faraja kilichopo mjini humo.

Lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wa kujiajiri na kujikimu kimaisha.

Wakiwa wamevalia mavazi yao mapya, tabasamu waliokuwa nayo ilionyesha ishara ya matumaini katika maisha yao ya baadaye.

Kulingana na Debra - ambaye ni mama wa watoto wawili - alipata pigo mara mbili alipopata uja uzito akiwa shule.

Mzazi akiwa na mtoto wake siku ya kufuzu kwa mahafali
Maelezo ya picha, Mzazi akiwa na mtoto wake siku ya kufuzu kwa mahafali

Mbali na kulazimika kukatiza masomo yake shule alifukuzwa nyumbani na wazazi wake waliokata tamaa.

Lakini baada ya kumaliza mafunzo imekuwa fahari kubwa kwake kwa kuwa mafunzo hayo aliyopata yatamsaidia kupiga hatua kubwa za kimaisha.

Anasema kwamba mafunzo hayo yatamsaidia kupata fedha za kujikimu yeye na watoto wake kupitia kuwalipia ada ya shule.

Maelezo ya video, Kituo cha Faraja: Waliokatiza masomo kutokana na ujauzito wahitimu Tanzania

Lakini kwa kuwa mabinti hao wana watoto wanawezaje kugawanya majukumu ya ulezi na kuendelea na masomo ya kawaida?

Debra mwenye umri wa miaka 23 anasema kwamba wao hulazimika kuwapeleka watoto katika kituo cha malezi ili kupata fursa ya kuendelea na shughuli zao bila usumbufu.

Lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wa kujiajiri na kujikimu kimaisha.
Maelezo ya picha, Wanafunzi waakiendelea na masomo ya kupika keki na kuirembesha

Hatahivyo mwanamke huyo anasema kwamba bado ni changamoto kuchanganya malezi na masomo huku mara nyengine akiwa na mda mchache kukaa na watoto.

"Ni changamoto kulea na kusoma. Wakati mwengine natamani kukaa na watoto lakini nakosa muda kwa sababu nakuwa darasani au nafanya homework.

Katika kituo hicho ni wachache tu waliobahatika kupata mafunzo hayo huku maelfu ya wasichana waliokatiza masomo yao wakisalia majumbani mwao bila msaada wowote.

Lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wa kujiajiri na kujikimu kimaisha.
Maelezo ya picha, Pia wanafunzi hao hufunzwa kushona nguo

Mikoa inayoripotiwa kuwa na kiwango kikubwa cha wasichana waliopata mimba za utotoni nchini Tanzania ni kama vile Singida, Manyara and Arusha inaripotiwa kuwa na kiwango kikubwa cha mimba za utotoni.

Kwa baadhi ya wazazi hao ni vigumu kuchanganya masomo na ulezi
Maelezo ya picha, Kwa baadhi ya wazazi hao ni vigumu kuchanganya masomo na ulezi

Kulingana na afisa wa maendeleo ya jamii katika mkoa wa Arusha Blandina Nkini baadhi ya wazazi hao waliingia katika ndoa bila wenyewe kujua jinsi ya kulea watoto.

Hivyobasi, Blandini anasema kwamba afisi yake imeanza kutoa mafunzo kwa wazazi hao ili kujua wajibu wao kwa lengo la kupunguza idadi ya mimba za utotoni.

Anaongezea kwamba afisi yake pia imefungua kituo ambacho kitatoa huduma zote za kijinsia kwa waathiriwa.

Hawa wanaonyesha vitu walivyotengeza ikiwemo keki
Maelezo ya picha, Hawa wanaonyesha vitu walivyotengeza ikiwemo keki

"Tumegundu baadhi ya wazazi wameingia katika ndoa bila wenyewe kujua jinsi ya kulea watoto , kwa hivyo tumeanza kuwapatia mafunzo wazazi ili wawajibike''.

''Katika kituo hicho kuna daktari, mwanasheria, na dawati la unyanyasaji wa kijinsia ambapo mhanga haitajiki kuzunguka sehemu nyingi na mwishowe kupoteza ushahidi kotini."

Jitihada hizo zilifanywa na mwalimu mstaafu Martina Simon Siara mwenye umri wa miaka 72 ambaye kwa sasa anahisi wakati umefika kwa serikali kupitia tena uamuzi wake.

Martina Simon Siara
Maelezo ya picha, Mama Martina Simon Siara mwanzilishi wa kituo cha Faraja

Mwalimu huyo anasema kwamba kwa sasa kituo cha Faraja kimeshindwa kukabiliana na idadi kubwa ya matatizo kama hayo kutokana na nafasi chache zilizopo.

Martina Simon Siara: Sifa za kituo hiki zimevuma mbali na kuvuka milima na mabonde. Sasa hivi imekuwa ni ndoto ya kila aliyepatwa na matatizo haya, kujiunga na kituo cha Faraja, licha ya nafasi kuwa chache. Wakati kundi hili likimaliza. Tayari kundi jingine linaingia likijawa na shauku ya kutaka kuiona siku kama hii.

Mwaka 2017, Rais wa Tanzania John Magufuli alipiga marufuku kwa wasichana kurudi katika shule rasmi za serikali baada ya kupata ujauzito kwa madai kwamba watakuwa na ushawishi kwa wenzao.

Hata hivyo, kumekuwa na malalamiko tangu agizo hilo litolewe.