Je, Chadema inajijenga au inajimega?

g

Chanzo cha picha, Mwananchi

Maelezo ya picha, Waliokuwa wanachama wa ngazi ya juu wa Chadema ambao wamejiuzulu hivi karibuni

Tuanzie usiku wa kuamkia Jumatano, Januari 22, 2025, pale Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kilipopata Mwenyekiti mpya, Tundu Antiphas Mughwai Lissu baada ya kumshinda Freeman Aikaeli Mbowe, aliyekuwa ameshika wadhifa huo kwa miongo mwili na ushei, tangu 2003.

Tangu uchaguzi huo kuisha, kumekuwa na vute ni kuvute kwa Chadema. Mosi, vuta ni kuvute na utawala, ambayo sio mpya, ni muendelezo wa harakati za Chadema dhidi ya kile wanachoamini ni kukosekana haki katika vyombo vya kusimamia uchaguzi. Ili kuwepo haki, wanataka mabadiliko, ambayo yatatokana na katiba mpya.

Pili, kuna vute nikuvute ndani ya chama iliyoanza wakati wa uchaguzi wa kumtafuta Mwenyekiti uliofanyika Januari, 2025. Maneno mengi yalinenwa, kauli nyingi zikatolewa, vijembe na ngonjera zikaghaniwa. Wengi waliamini hayo yangemaliza baada ya uchaguzi kuhitimika. La hasha! Hali haionekani kubadilika. Mchafukoge ndani ya Chadema unaendelea.

Mivutano yote mwili ina athari kwa Chadema: Huo wa kwanza, umepelekea Tundu Lissu kuwekwa ndani kwa kesi ya uhaini. Viongozi wengine na wanachama pia wamekamatwa kwa nyakati tofauti na kuachiwa. Lakini hilo hilo si jambo jipya, lilitarajiwa.

Na mvutano huu wa pili, umepelekea baadhi ya wanachama wa Chadema kukiacha mkono chama hicho. Ni ukweli ulio wazi kwamba, kuondoka chamani ni haki ya mwanachama yeyote wa chama chochote, ila uamuzi huo unaweza usiwe wa afya kwa chama.

Chadema wana vita mbili wanavyopigana sasa kwa wakati mmoja. Wao kwa wao na wao dhidi ya utawala. Sina hakika ikiwa wana uwezo wa kushinda vita vyote kwa wakati mmoja, hasa ukizingatia ile sehemu ya msemo wa Waswahili "utengano ni udhaifu."

Katika nyakati za harakati za kudai mabadiliko ya kisiasa hasa mbele ya utawala, watu ni mtaji muhimu sana. Ingawa swali la watu hao wawe wa aina gani, litaibuka. Mwongozaji wa harakati hizo ndio atakuwa na jawabu ya swali hilo.

Pia unaweza kusoma

Mzozo mpya Chadema?

Kuna jambo la tatu, ambalo ni jipya kabisa kwa Chadema. Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa wiki hii imetengua uteuzi wa wajumbe wanane wa sekretarieti na kamati kuu ya Chadema, ambao walithibitishwa na Baraza Kuu la chama hicho, ofisi hiyo inasema ni kutokana na kutokuwepo kwa akidi halali ya kikao hicho.

Miongoni mwa waliotenguliwa ni vigogo wa chama akiwemo John Mnyika – Katibu Mkuu, Amani Golugwa – Naibu Katibu Mkuu (Bara) na Ally Ibrahim Juma – Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar), Godbless Lema – kuwataja kwa uchache.

Chadema kupitia Makamu Mwenyekiti Bara, John Heche, imejibu kwa kusema, inaendelea kuwatambua viongozi hao na hawatabadili chochote. Heche amesema akiwa mkoani Mara, "mimi nakwambia Msajili wewe huhitaji kumtambua Katibu Mkuu wa chama chetu sisi tunamtambua."

Katika hili, hali ikibaki kama ilivyo sasa, itakuwa nafuu kwa Chadema, lakini ikiwa Msajili ataamua kuchukua hatua kubwa zaidi, huenda hilo likazusha shida nyingine ndani ya chama hicho.

Mwanasheria na mchambuzi wa masuala ya Katiba na Sera, Edson Kilatu akihojiwa na moja ya vyombo vya habari vya ndani anasema Msajili hana mamlaka ya kufanya ilichofanya.

"Maamuzi ambayo Msajili ameyafanya ni batili, kisheria wako sahihi, sema kisiasa hiyo naiona ni changamoto, ila kisheria mimi sioni shida Chadema wasipozingatia hayo maagizo ambayo kimsingi yamekiuka katiba ya nchi", anasema Kilatu.

Maelezo ya Kilatu anayelekeza kwenye Katiba ya Chadema Ibara ya 6.2.2 ya mwaka 2016 toleo la mwaka 2019 ambayo inasema kwenye vikao vingine vyote akidi ni 50% isipokuwa kama kikao kinahusu mabadiliko ya katiba ambayo akidi yake ni 75%. Kwa mujibu wa Chadema akidi ya zaidi ya 50% ilikuwepo.

Huu huenda ukawa ni mzozo mpya unaokwenda kuanza sasa. Mzozo ambao utaiweka Chadema kwenye kaa la moto zaidi, kutokana na mamlaka na nguvu kubwa aliyopewa Msajili wa vyama kisheria.

Nani kaondoka Chadema?

Kuanzia Juma lililopita kumekuwa na msururu wa wanachama wakiwemo viongozi wa kipindi kilichopita chini ya Mbowe, wanaoojiita G-55 kutangaza kwa mafungu kuondoka Chadema.

Msururu huo ulianza rasmi Jumatano ya Mei 7, 2025 Iliyokuwa sekretarieti ya Chama hicho kutangaza kuondoka, wakieleza kwa vyombo vya habari na umma sababu za wao kutimka.

Hao ni aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Bara, Benson Kigaila, aliyekuwa Mkurugenzi wa Itifaki, Uenezi na Mambo ya Nje John Mrema, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalim, aliyekuwa katibu wa sekretarieti, Julisu Mwita, na aliyekuwa Katibu wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Catherine Ruge.

Kigaila alisema kuna 'ubaguzi dhidi ya wanaohusishwa na upande wa Mbowe na wamekuwa wakitengwa katika ngazi zote.' Mwalim yeye alisema 'kama sio mrengo wa no reform, no election unatengwa na ushauri wao kutosikilizwa juu ya hoja ya No reform, no election.' Ruge ameeleza, 'hawezi kuwa kwenye chama ambacho haamini katika ajenda na msimamo wao.'

Aman Golugwa, amejibu kwamba 'kuondoka kwao hakuna pengo lolote waliloliacha ndani ya chama hicho' ambacho ni kikuu cha upinzani. Naye Heche amesema 'yaliyosemwa na waliondoka hayana ukweli, bali wamefikia bei na ana taarifa kuwa wengine pia watafuata.'

Kwa hakika, jawabu ya swali la nani anasema kweli kati ya makundi haya, huenda lisiwe la muhimu miongoni mwa wafuasi wa chama hicho. Bila ya shaka, lilo muhimu ni kutokiona chama hicho kikiporomoka na kuishia kwenye kaburi la sahau.

Chadema bado ina ushawishi na yaonekana Tundu Lissu amekuja na mikakati mipya ili kufanikisha kile wanachotaka kukifanikisha; matokeo ya mwisho yatakayozaliwa kutokana na mikakati hiyo, ndiyo yataamua ikiwa uongozi wake umefanikiwa au umefeli.

Inajijenga au inajimega?

f

Chanzo cha picha, CHADEMA

Maelezo ya picha, Tundu Lissu baada na Freeman Mbowe (kulia)

Kujiuzulu au kuondoka chamani sio jambo jipya, itakumbukwa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2020 vyama vya upinzani hasa Chadema, vilipoteza wanachama kadhaa waliokuwa Wabunge na Madiwani ambao walihamia Chama cha Mapinduzi (CCM), kwa hoja ya kuunga mkono juhudi za maendeleo za raia wa wakati huo hayati John Pombe Magufuli.

Chadema waliwatuhumu walioondoka kuwa wananunuliwa na kuahidiwa kupewa viti katika uchaguzi mkuu. Wabunge walioondoka Chadema na kufanikiwa kurudi katika nafasi hizo kupitia CCM, walikuwa ni pamoja na Mwita Waitara, Julius Kalanga, Chacha Ryoba, Godwin Mollen, James Ole Millya, Puline Gekul na Joseph Mkundi.

Licha ya kundi kubwa kuondoka, Chadema bado ilifanikiwa kubaki kuwa chama kikuu cha upinzani – ingawa ilikosa viti vingi vya Ubunge kama vyama vingine vya upinzani, kutokana na kile ambacho wengi walikiona kuwa ni mbinu chafu zilizotumika wakati wa uchaguzi wa 2020.

Turudi sasa kwenye swali kuu: Je, Chadema inajijenga au inajimega? Ionekanavyo ni kwamba mambo yote mawili kwa sasa yanatokea kwa wakati mmoja; uongozi mpya uko katika harakati ya kukijenga chama na wakati huo huo kuna makundi yanameguka ndani ya chama.