Ugonjwa usio na tiba unaowatatiza Watanzania wengi

.

Chanzo cha picha, Hajjrat Mohammed

Maelezo ya picha, Hajjrat Mohammed
  • Author, Na Leonard Mubali
  • Nafasi, BBC Swahili Dar es Salaam
  • Akiripoti kutoka Tanzania

Katika orodha ya magonjwa yapo baadhi ambayo hata majina yake yakitajwa katika kundi la watu, swali la kwanza linalojitokeza huwa ni ugonjwa gani huo?

Ugonjwa wa Lupus ni miongoni mwa magonjwa ambayo hayafahamiki kwa wengi pamoja na kwamba yana athari katika kuharibu mfumo wa kinga za mwili.

Daktari Magreth Angelus kutoka Hospitali ya Shree akizungumza na BBC amekiri kwamba ni kweli watu wengi hawana uelewa na taarifa sahihi za ugonjwa huo na kwa wachache waliobainika baadaye kuwa na ugonjwa huo iliwachukua muda mrefu kujua kwamba wana maradhi ya Lupus.

Katika Makala hii tunaiangazia safari ya mateso na panda shuka ya maisha, na ndoto zake kupotea kabisa msichana Hajjrat Mohammed ambaye baada ya kushindwa kujua anasumbuliwa na ugonjwa gani hatimaye ilibainika anasumbuliwa na Lupus.

Hajjrat katika mahojiano maalum na BBC alianza kuelezea historia ya kuanza kuugua na namna alivyoweza kugundulika baadaye kuwa ana Lupus.

''Nilianza kuguua mwaka 2006, kipindi hicho nilihangaika sana, kwani ilikuwa haifahamiki naugua maradhi gani, nilienda hospitali ya taifa ya Muhimbili kwa mara ya kwanza lakini hawakugundua tatizo langu licha ya maumivu niliohisi mwilini '' alisema.

Dalili alizopitia hadi kubainika wazi kuwa ana ugonjwa wa Lupus, anazikumbuka akisimulia huku uso wake ukionyesha uchungu mkubwa.

Anazipanga moja baada ya nyingine mbali na mabadiliko aliyoanza kuyaona katika mwili wake.

''Kwa upande wangu, mimi nilianza kudondoka nywele, nikiwa na umri kama wa miaka 13, huku vidonda na vipele vinavyotoa damu na usaha vikijitokeza. Vidonda hivyo viliongezeka vikasambaa usoni, shingoni, ndani ya mwili, mikononi, ( hadi sehemu za siri '', alisema mwanadada huyo.

Dalili nyingine alizozitaja ni pamoja na uchovu, maumivu ya mwili - tatizo lililomfanya kulala mara kwa mara ,huku wazazi wake wakilalamika kwamba ni mvivu licha ya kuhisi maumivu makali mwilini .

Hajrat anasema kwamba ugonjwa huu pia ulimsababishia tatizo jingine la kusahau na homa za mara kwa mara.

''Mfano, kama hapa, tunopoongea, si unaiona mzima?, ukinifanyia vipimo utaona naugua UTI . Kwa hiyo, najikuta ni mtu wa kumeza dawa kila siku maana UTI na Lupus ni magonjwa ya maisha na matibabu yake kwa mwezi ni laki saba. Baba alipata kiharusi kwasababu ya mahangaiko yangu. Kufikia sasa nadhani ameuza kila kitu kunitibu tangu nikiwa umri mdogo hadi sasa '', Hajjrat aliongezea.

.

Chanzo cha picha, Hajjrat Mohammed

Ushiriki wa familia katika maradhi ya Hajrat

'Kwa upande wa familia, walipopokea habari za maradhi yaliokuwa yakiniathiri , waliweza kuishi na mimi kwa upendo na kuhangaika na mimi, wameuza vitu vya thamani na sasa sote hatuelewi nini itakuwa hatima yangu '', aliongezea Hajjrat

Hata hivyo Hajrat anasema mchango wake kwa familia hata baada ya kuwa mkubwa kwa sasa ni mdogo, kwa sababu hawezi kufanya kazi yoyote hata zile anazoziweza sababu ya unyanyapaa na kubaguliwa hali ambayo ilimshinikiza kukatisha masomo yake ya sekondari.

Vipimo hadi kugundulika ana Lupus

.

Chanzo cha picha, Hajrat Mohammed

Anasema aliendelea kuhangaika huku na kule kujaribu kubaini nini tatizo kabla ya, kushauriwa tena kurejea hospitali ya taifa Muhimbili kwa mara ya pili.

''Mwaka 2013 tulirudi tena kufanya vipimo. Ugonjwa haukufahamika wakati huo,na kulazimika kuendelea na hatua nyingine zikiwemo za mimi kutumia dawa mbalimbali'' alisema msichana huyo.

Alieleza kuwa walipokwenda tena hospitali ya taifa Muhimbili kwa mara nyingine ndipo ilipobainika kuwa ana ugonjwa unaoitwa Lupus na ndipo hapo wakaomba kibali cha kwenda India kwa vipimo zaidi na kusaka matibabu.

Nchini India, ugonjwa huo ambao ni aina ya DLE ulibainika hatua iliowafanya madaktari kumpatia dawa za mwezi mzima na kisha wakarejea nchini Tanzania.

Hajjrat anasema alipata nafuu kubwa aliporejea kutoka India lakini ghafla bin vuu mambo yakabadilika .

''Ngozi iliharibika, nywele zikaanza kudondoka na kusababisha vidonda kichwani vilivyokuwa vikitoa usaha'', anasema Hajrat.

Aliongeza: Nahisi maumivu makali katika viungo vyangu vya mwili, mifupa yangu na misuli na wakati mwingine nashindwa kusimama, kukaa.

Baada ya kuelezewa na daktari kwamba maradhi aliyokuwa anagua hayana tiba ,aliamua kuingia mtandaoni kuwasaka watu wenye maradhi kama yake ama taasisi yoyote inayojishughulisha na kampeni ama ushauri wowote kuhusu Lupus, lakini ilikuwa vigumu kuwapata.

''Niligundua kuwa hakuna taarifa za watu wenye matatizo kama yangu na nikalazimika kuanzisha taasisi kwa jina Lupus Awareness Organization.''

Baada ya kuhojiwa na chombo fulani cha habari na kuwacha nambari zangu za simu nilipata wenzangu 16 na hao wakawa wanachama wenza wa taasisi hiyo hadi leo'' anasema Hajrat.

Ili kujua kwa kina kuhusu maradhi hayo BBC, ilifanya mahojiano na Daktari Magreth Angelus kutoka Hospitali ya Shree Hindu Mandar jijini Dar es Salaam ambaye alisema kwamba ugonjwa huo ulitokana na hitilafu kwenye mfumo wa kinga za mwili.

''Aina ya ugonjwa huu inayojulikana zaidi ni Systemic Lupus Erythematous SLE, ambao unashambulia kinga za mwili na kuathiri viungo mbalimbali,'' alisema Dkt.Magreth,

Dkt.Magreth alivitaja baadhi ya viungo vya mwili ambavyo hushambuliwa zaidi na ugonjwa huo kuwa ni ngozi, ,mapafu na figo.

Hata hivyo alisisitiza kuwa ugonjwa huo unawapata sana wanawake kuliko wanaume.

.

Chanzo cha picha, Hajrat Mohammed

Kwanini Lupus ni vigumu kugundulika?

Dkt. Magreth alisema: Unajua ni vigumu kuzigundua dalili za Lupus kwa sababu zinafanana na magonjwa mengine mengi.

Je, ugonjwa wa Lupus unatibika?

Kwa mujibu wa Dkt. huyo maradhi hayo hayajapata tiba na wagonjwa wengi wamekuwa wakipatiwa dawa za kupunguza maumivu tu. Daktari huyo ameongezea kwamba ipo haja ya jamii kuendelea kufuatilia taarifa za ugonjwa huu ili zinapotokea dalili waweze kuwahi kuwafanyia wagonjwa vipimo.

Imehaririwa na Abdalla Dzungu