Fahamu virusi hatari vinavyotokana na kinyesi cha panya

Chanzo cha picha, Getty Images
Maafisa nchini Marekani wamethibitisha kuwa mkewe muigizaji maarufu wa Marekani mshindi wa tuzo ya Oscar, Gene Hackman alifariki kutokana na matatizo ya kupumua yanayohusishwa na Hantavirus.
Huu ni ugonjwa adimu unaoambukizwa na panya.
Inaamika kuwa Betsy Arakawa alifariki wiki moja kabla ya mumewe, ambaye naye alikuwa akiugua ugonjwa wa Alzheimer. Maafisa waliigundua miili ya wawili hao nyumbani kwao New Mexico mwezi uliopita.
Maafisa wa afya wanaeleza kuwa ugonjwa huo unaweza kusababisha muathirika kuwa na dalili kama za homa anapokaribia kinyesi cha panya, na kwa wakati mwingine hali ikiwa mbaya sana muathirika anaweza kuishia kuugua Hantavirus Pulmonary Syndrome (HPS), ugonjwa wa mapafu unaoweza kusababisha mtu kufariki dunia.

Chanzo cha picha, Getty Images
Hantavirus ni nini?
Huu ni mkusanyiko wa virusi unaotokana na panya, na unaosambazwa kwa binaadamu kwa kupumua chembechembe za kinyesi cha panya kilichokauka.
Maambukizi hutokea wakati virusi hivyo vinaposambaa hewanikutoka kwenye mkojo au kinyesi au mate ya panya kwa mujibu wa taasisi ya kudhibiti magonjwa (CDC).
Licha ya kwamba ni ugonjwa adimu, virusi hivyo vinaweza kusambaa baada ya kugwaruzwa au kung'atwa na panya.
Virusi hivyo vinaweza kusababisha magonjwa mawili hatari. Kwanza, Hantavirus Pulmonary Syndrome – hii ni aina ya ugonjwa inayoshuhudiwa pakubwa nchini Marekani – na ndio uliosababisha kufariki dunia kwa Bi Arakawa kwa mujibu wa maafisa.
Mara nyingi dalili huanza kwa uchofu, homa na maumivu ya misuli, hii hufuatwa kwa maumivu ya kichwa, kisunzi, baridi mwilini na matatizo ya tumbo.
Pili ni ugonjwa wa kuvuja damu na ndio hatari zaidi na kimsingi huathiri figo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Ugonjwa huu unatibiwa vipi?
Hakuna matibabu maalum kwa maambukizi ya virusi vya ugonjwa huu.
Taasisi ya kudhibiti magonjwa CDC inapendekeza kujaribu kuhimili dalili za ugonjwa huo.
Wagonjwa walio na dalili kali, huenda wakalazimika kulazwa hospitalini katika kitengo cha wagonjwa mahututi.
Wengine wanalazimika kupewa usaidizi wa kupumua.
CDC inashauri kudhibiti uwepo wa panya katika sehemu za makazi, kazini ili kupunguza maambukizi ya virusi hivyo.
Kadhalika, inashauriwa pia kuvaa mavazi ya kujikinga wakati wa kusafisha kinyesi cha panya ili kuepuka kupumua hewa ilioathirika na kinyesi hicho.