Watoto wa Gaza walio na utapia mlo walivyojeruhiwa katika shambulizi la Israel

  • Author, Fergal Keane
  • Nafasi, BBC News
  • Akiripoti kutoka Amman

Vitisho vya vita vinaongezeka. Viungo vya watu waliofariki vilivyotapakaa mitaani. Watu ambao kifo kinawakodolea macho. Watu ambao wanakabiliwa na njaa. Hali inazidi kuwa mbaya – uzito wote wa mateso ya binadamu yaliyoshuhudiwa na wanahabari wenzangu wajasiri huko Gaza.

Wazo la kuangalia kando unapoona picha ya kusikitisha linaweza kukujia. Lakini wapiga picha wanaofanyia kazi BBC hawawezi kufanya hivyo na Siku Jumanne mmoja wao akajeruhiwa. Kwa usalama wao hatutaji majina ya wenzetu huko Gaza.

Mpiga picha wetu hakujeruhiwa sana, lakini hilo lilikuwa jambo la bahati. Mabomu hayo ya Israel yalirushwa kwenye eneo la maegesho ya magari ya Hospitali ya Ulaya huko Khan Younis na kuua na kujeruhi makumi.

Waisrael wanasema kiongozi wa Hamas alikuwa amejificha katika boma la amri na udhibiti chini ya hospitali hiyo. Jeshi lilisema lilifanya "shambulio maalum" - na kuilaumu Hamas kwa "kuwatumia raia walio ndani na karibu na hospitali kama ngao". Hamas inakanusha madai hayo.

Pia unaweza kusoma:

Wakati wa shambulio hilo, familia ambazo watoto wao wagonjwa walitarajiwa kuhamishwa kutoka Gaza zilikuwa zikikusanyika hospitalini. Pia kulikuwa na familia zinazosubiri kukutana na watoto wanaorejea kutoka kwa matibabu nje ya nchi.

Baba mmoja alikuwa na waandishi wa BBC na alijeruhiwa na mabomu hayo. Sasa ameruhusiwa kutoka hospitalini. Picha za kutisha zinaonyesha mwanahabari wetu akijaribu kuwafariji watoto wa mwanamume huyo waliokuwa na hofu kubwa.

Tahadhari: Taarifa hii ina picha za kusikitisha.

Waandishi wenzangu kwa kiwango kikubwa katika siku za hivi karibuni wamekuwa ya wakiangazia hali mbaya ya watoto wanaokabiliwa na utapiamlo.

Muda mfupi kabla ya mlipuko huo, nilitumia ujumbe mpiga picha wetu kumshukuru kwa jinsi alivyonasa kwa uweledi mkubwa video ya taarifa ya Siwar Ashour. Hili lilikuwa jibu lake:

"Hadithi ya Siwar ilitugusa sote, na kuifanyia kazi ilikuwa jambo la kuumiza sana ambalo nimewahi kufanya. Lakini nilijua hali yake ilipaswa kuangaziwa - ilipaswa kusikilizwa."

Siwar ana umri wa miezi mitano na hana lishe bora, mtoto ambaye macho yake makubwa yametawala umbo lake lililodumaa. Wanafuata kila hatua ya mama yake Najwa. Siku ya Jumanne Najwa alitutumia ujumbe wa video kutoka chumba chake cha Hospitali ya Nasser kusini mwa Gaza.

Alitaka ulimwengu ujue jinsi anavyompenda mtoto wake. "Natamani angepokea matibabu anayohitaji, apone kikamilifu, na kurudi kama alivyokuwa hapo awali - kucheza kama watoto wengine, kukua na kunenepa kama watoto wengine. Yeye ni mtoto wangu wa kwanza, na kama mama yake, ninasononeka moyoni."

Siwar Ashoura ana utampya mlo mbaya na hawezi hata kutumia maziwa
Maelezo ya picha, Siwar Ashoura ana utampya mlo mbaya na hawezi hata kutumia maziwa

Katika siku chache zilizopita Siwar amepata maambukizi ya ngozi. Vidonda vinaonekana kwenye mikono yake. Pia anaumwa vibaya na utumbo. Changamoto kubwa ni kuhakikisha lishe anayopata inamsaidia. Mfumo wake wa kinga unapambana na kunyimwa kulikosababishwa na kizuizi cha Israeli.

Kilio cha mtoto ni hafifu, lakini kimejaa maumivu, sauti ya mahangaiko. Siwar anaweza tu kunywa mchanganyiko maalum wa maziwa kutokana na mizio kali.

Siku ya Jumanne kulikuwa na habari nzuri zaidi. Madaktari katika Hospitali iliyo karibu ya Jordanian Field walifanikiwa kupata baadhi ya mchanganyiko wa maziwa anayohitaji. Ni kiasi kidogo lakini wanapanga kumuagizia mengine zaidi.

Watoto wa Asma Al-Nashash wamekwama Gaza
Maelezo ya picha, Watoto wa Asma Al-Nashash wamekwama Gaza

Siku chache zijazo kuna mipango ya kuwapeleka watoto wagonjwa katika mataifa ya Umoja wa Falme za Kiarabu na Jordan. Hapa Amman tayari kuna familia kadhaa za Wagaza ambazo zina watoto wanaotibiwa magonjwa au majeraha ya vita katika hospitali za ndani. Uhamisho huu unaratibiwa na Waisrael ambao hufanya ukaguzi wa kina wa wazazi wanaosafiri na watoto wao.

Mnamo Januari tulishuhudia kuwasili kwa Abdelrahman al-Nashash na mama yake Asma. Abdelrahman alipoteza mguu wake katika shambulio la bomu la Israel.

Kwa muda wa miezi minne wameishi mahali wanapata chakula na malazi. Mahali salama.

Tulipowatembelea Jumanne Asma aliwapigia simu watoto wake na bibi yao huko Gaza.

Watoto walio kwenye picha gii wamekwama mjini Gaza na bibi yao Najwa
Maelezo ya picha, Watoto walio kwenye picha gii wamekwama mjini Gaza na bibi yao Najwa

Bibi yao Najwa alielezea jinsi walivyozungukwa na mashambulizi. "Roketi zinarushwa kutoka kila upande, zinapita juu ya vichwa vyetu. Hakuna chakula Chakula. Maisha ni mabaya sana. Bei ya bidhaa iko juu sana."

Watoto walimpungia mkono mama yao kwa ishara ya mabusu.

Baadaye, Asma alituambia: "Sijui niseme nini. Ninamshukuru sana mama yangu kwa yote anayonifanyia. Natumai nikirudi nyumbani nitawakuta wakiwa salama na wenye afya njema." Alijawa na hisia na kukaa kimya.

Ni mama tu anayeweza kuwa na nia ya kurudi Gaza baada ya kumuona mtoto wake aliyekwama katika mashambulizi hatari akiwa na hofu na njaa.

Taarifa ya ziada na Alice Doyard, Suha Kawar and Nik Millard.