'Mtoto wangu mpendwa alifariki kwa njaa'

.

Chanzo cha picha, Family photo

Jamal alikuwa mtoto anayevutia zaidi hospitalini, Abeer al-Kaferna anasema, akikumbuka kuzaliwa kwake huku akipitia picha kwenye simu yake.

"Tazama jinsi anavyovutia. Mtoto wangu mpendwa."

Ndicho alichobaki nacho kwa mtoto wake wa pekee.

Jamal alifariki tarehe 18 Januari.

Alikuwa na umri wa miezi mitatu alipoanza kuugua.

Ilikuwa mwezi mmoja baada ya vita na familia yake ilikuwa imefurushwa mara kadhaa, ikikaribia kufariki baada ya shambulio la anga la Israel kwenye kambi walimokuwa wakiishi.

Alipatikana na maambukizi kwenye utumbo wake na kupewa dawa. Lakini hakupata nafuu.

Pia unaweza kusoma:

Mapema mwezi Desemba, asilimia 90 ya familia kaskazini mwa Gaza zilikuwa zikikosa chakula kwa siku nzima, kulingana na Mpango wa Chakula wa Umoja wa Mataifa.

Abeer alikuwa akihangaika kumnyonyesha mtoto wake.

Akiwa na lishe duni na upungufu wa maji mwilini, hakuwa akitoa maziwa ya mama ya kutosha na ilikuwa vigumu kupa maziwa ya unga ya mtoto.

Mnamo Novemba, Jamal alikuwa na uzito wa kilo 7 lakini alipungua uzani haraka.

Ndani ya wiki, alikuwa na kilo 3.5 tu.

Kufikia Januari, bibi yake Esmahan anasema alionekana "kama mifupa".

"Hatukuweza kumtafutia maziwa," babake Mahmoud al-Kaferna anasema.

"Tulijaribu kumpa maji lakini hata maji yalikuwa machafu."

.

Chanzo cha picha, Family photo

Waliandikiwa dawa lakini hawakuweza kuipata. Hatimaye walilazwa hospitalini lakini Jamal alipoanza kupata nafuu ilibidi waondoke.

"Hospitali ilisema hawana la kumfanyia zaidi na kuna watoto wengine wanapaswa kuhudumiwa pia," babake anasema.

Usiku wa tarehe 17 Januari, joto la Jamal lilianza kushuka na alikuwa akikohoa. Kitu cheupe kilikuwa kinamtoka puani.

"Tulikimbia hospitalini usiku mabomu yakiwa yanarushwa," Mahmoud anasema.

"Walijaribu kumuokoa kwa muda wa nusu saa lakini hawakuweza. Ukosefu wa chakula, maji na matibabu sahihi vilimuua mwanangu.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limekuwa likijaribu kupata msaada zaidi wa matibabu kaskazini.

Ni safari tatu pekee kati ya 16 zilizopewa idhini ya kuondoka na Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF) mnamo mwezi Januari.

Mnamo Februari, hakuna safariiliyopewa idhini ya kufikia eneo hilo.

Wakati WHO hatimaye ilifika kaskazini mwa Gaza mapema mwezi Machi, timu yake iligundua kuwa watoto 10 walikuwa wamefariki kutokana na "ukosefu wa chakula" katika hospitali moja.

Wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas inasema watoto 27 wamefariki kutokana na utapiamlo na upungufu wa maji mwilini huko Gaza tangu kuanza kwa vita.

Idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka.

Takriban Wapalestina 300,000 wanadhaniwa kusalia kaskazini mwa Gaza.

The UN and its humanitarian partners planned 61 missions to the north in January. The IDF facilitated nine of them.

Umoja wa Mataifa na washirika wake wa kutoa misaada ya kibinadamu walipanga safari 61 za upande wa kaskazini mwezi Januari.

IDF iliruhusu tisa kati ya hizo.

Baada ya msafara wa chakula cha Umoja wa Mataifa kutiwa moto wa jeshi la wanamaji la Israel ulipokuwa ukingoja karibu na kituo cha ukaguzi, Umoja wa Mataifa ulipanga safari chache. Kati ya 24 walizopanga mnamo Februari, IDF iliruhusu sita.

"Uwezo wa Umoja wa Mataifa kufika eneo la kaskazini ni jambo ambalo halipaswi kutiliwa shaka kama tuko tayari na kuweza kufika huko," anasema Tess Ingram, afisa wa mawasiliano wa Unicef, ambaye alikaa kwa wiki moja huko Gaza mwezi Januari na alijaribu kufikia eneo la kaskazini mara kadhaa.

Israel inasema hakuna kikomo kwa kiasi cha misaada inayoweza kutolewa na inalaumu mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa kushindwa kusambaza vifaa.

Imewaacha watu wa kaskazini wakiwa na kidogo au hawana chochote.

Khalid anajihifadhi katika jiji la Jabalia na watoto wake watano na watu 90 wa familia yake kubwa.

Aliambia BBC kwamba familia yake imekuwa ikiishi kwa magugu na chakula cha mifugo.

"Ni kama kula kokoto," anasema.

Baada ya kula chakula hicho, alikuta damu kwenye kinyesi chake na tumbo linamuuma.

Kisha familia yake ikapata bahati; walikuta mfuko wa mchele, umejaa uchafu na mawe, kwenye kifusi cha jengo. Pia walitafuta mmea unaoweza kuliwa ambao ulikua kwenye bustani ya jengo lililolipuliwa baada ya mvua kunyesha.

Lakini chakula cha mifugo, mchele na hata magugu yameisha.

Kwa wiki moja mwanzoni mwa Machi, familia ya Khalid haikuwa na chochote. Nchi za Kiarabu na Magharibi sasa zinaratibu kutoa chakula kwa njia ya anga huko Gaza.

Khalid na familia yake walipata bahati tena walipokamata pakiti za mchele na nyama zilizokuwa zikidondoshwa kwa njia ya anga.

Lakini mashirika ya misaada yanasema hii ni njia isiyofaa na ya gharama kubwa ya kupeleka chakula katika eneo hilo.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Aseel, ambaye pia yuko kaskazini mwa Gaza, aliambia BBC kwamba misaada mingi ilianguka baharini na watu walilazimika kupigana ili kuifikia.

Kaka yake alienda mahali pa kudondoshea ndege saa 06:00 lakini akarudi na mkebe wa dagaa.

Siku iliyofuata, alifanikiwa kupata chupa mbili ndogo za maji.

Baadhi ya misaada hiyo pia ilitua katika maeneo ya karibu na mpaka wa Israel ambayo IDF imewaonya wakazi kutokaribia.

"Kila mtu anakimbia, kwa kufuata mwelekeo wa parachuti, hadi mwisho tunakata tamaa na kurudi bila chochote," Aseel anasema.

Watu watatu huko Gaza waliambia BBC kwamba misaada iliyodondoshwa ilinufaisha wachache tu kati ya maelfu wanaojaribu kuipata. Waliobaki walirudi wakiwa wamechoka na mikono mitupu.

Umoja wa Mataifa unasema takriban Wapalestina 576,000 huko Gaza - robo moja ya watu - wako hatua moja kutoka kukabiliana na njaa.

Inaonya kuwa muda unakwenda kwa watu wa kaskazini wenye chakula kidogo au maji safi.

Ili njaa itangazwe, 20% ya idadi ya watu lazima wawe wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, 30% ya watoto lazima wawe na utapiamlo mkali na watu wawili kati ya kila 10,000 wanafariki kila siku kwa njaa, au kutokana na utapiamlo na magonjwa.

Mwezi Januari, wastani wa malori 150 ya misaada yaliingia Gaza kila siku - sehemu ya lori 500 za misaada na vifaa vya kibiashara ambavyo vilivuka mpaka kabla ya vita.

Hata katika maeneo ya kusini mwa Gaza ambayo yanapata misaada zaidi, familia nyingi zinaishi kwa mlo mmoja kwa siku.

Matunda, mboga mboga, mayai na nyama ni vigumu kupata na vikipatikana ni hadi mara 10 ya bei iliyokuwa kabla ya vita.

"Ninahitaji mkopo wa kimataifa kulisha familia yangu," anatania Muhammad al-Najjar, ambaye alilazimika kuhama kutoka eneo la Jabalia hadi Rafah kusini na watu 11 wa familia yake.

Makopo manne ya maharagwe, makopo matatu ya chickpeas na masanduku 11 ya biskuti kawaida hulazimika kudumu kwa wiki.

Wanakula pale wanapoweza, kwa gharama kubwa.

Nagham Mazid anafanya kazi kama daktari wa kujitolea katika Hospitali ya Martyrs ya Al-Aqsa katikati mwa Gaza.

Ameona idadi inayoongezeka ya wagonjwa wanaougua upungufu mkubwa wa maji mwilini na magonjwa ya njia ya utumbo kutokana na kula vyakula vingi vya makopo.

Kumekuwa na visa vya sumu kwenye chakula kutoka kwa chakula kilichochafuliwa.

Hospitali pia inashuhudia ongezeko kubwa la visa vya homa ya ini na upungufu wa damu.

WHO inasema visa vya kuhara na magonjwa ya kupumua kwa papo hapo vimeongezeka, haswa kwa watoto.

Familia ambayo mtoto Jamal aliiacha haina chakula kwa sasa. Binamu zake wanane na wazazi wao wana njaa.

Wanatumai kuwa watakuwa na bahati ya kupata baadhi ya usaidizi kupitia msaada unaodondoshwa kwa njia ya anga, baharini au nchi kavu.

Pia unaweza kusoma:

Imefasiriwa na Asha Juma na kuhaririwa na Ambia Hirsi