Amenorrhoea: Sababu 8 za kukosa hedhi mbali na ujauzito

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, BBC 100 Women
- Nafasi,
Kukosa hedhi kwa wanawake wa umri wa kuzaa huitwa amenorrhea, na ingawa sababu inayojulikana zaidi ni ujauzito, kuna sababu nyingi kwa nini hedhi inaweza kuchelewa au kukosekana.
Kwa kawaida, wanawake wa umri wa uzazi huwa na hedhi kila baada ya siku 28, ingawa ni kawaida kuwa na mzunguko mfupi au mrefu zaidi, kati ya siku 24 na 35.
Kukosa hedhi mara kwa mara hakuchukuliwi kuwa tatizo kubwa, lakini ikiwa ni suala linalojirudia, inaweza kuashiria suala la msingi.
"Lazima ujitambue na jinsi mwili wako unavyofanya kazi, ili ujue wakati kitu kiko sawa. Na kila mwanamke hufanya kazi kwa njia tofauti; hakuna wanawake wawili wanaofanana," daktari wa magonjwa ya wanawake Dk Amira Alkourdin Martinez aliiambia BBC.
Huduma ya Kitaifa ya Afya ya Uingereza (NHS), inapendekeza kushauriana na daktari ikiwa umekosa hedhi kwa miezi mitatu mfululizo na huna mimba, au ikiwa kipindi chako kitakoma kabla ya umri wa miaka 45.
Kliniki ya Mayo nchini Marekani pia inapendekeza mashauriano ya tiba kwa wasichana ambao hawajaanza kupata hedhi kufikia umri wa miaka 15.
Hizi ndizo sababu nane za kawaida, ukiondoa ujauzito, ambazo mwanamke anaweza kupata amenorrhea, kulingana na taasisi zote mbili.
1. Msongo wa mawazo
"Msongo wa mawazo ndio sababu kubwa zaidi na janga la kweli la wakati wetu," anasema Dk Amira Alkourdin Martinez.
Msongo huchochea utengenezaji wa homoni kama vile adrenaline, na kuuweka mwili katika hali ya tahadhari kama njia ya ulinzi katika hali hatari.
Kukaribiana kwa muda mrefu kwa homoni hizi kunaweza kuvuruga hedhi, kufanya mzunguko kuwa mrefu au mfupi, na kusababisha kukosa hedhi, au kufanya hedhi kuwa ya maumivu zaidi.
Katika baadhi ya matukio, inaweza kusababisha mwanamke kupata hedhi mbili ndani ya mzunguko wa kawaida wa wiki nne.
Ikiwa msongo wa mawazo ndio chanzo cha kuchelewa au kukosa hedhi, NHS inapendekeza kuchukua hatua kama vile mazoezi ya kawaida au mbinu za kupumua.
Ikiwa hatua hizi hazifanyi kazi, kuna matibabu ya utambuzi-tabia (CBT) ambayo yanaweza kuwasaidia watu kukabiliana na matatizo na wasiwasi.
2. Kupunguza uzito kupita kiasi au ghafla
Kuzuia sana kalori zinazotumiwa kunaweza kuzuia mwili kutoa homoni zinazohitajika wakati wa utengenezaji mayai.
Wakati kupoteza uzito kunasababishwa na shida ya kula, kama vile anorexia, msaada wa daktari wa akili ni muhimu.

Chanzo cha picha, Getty Images
3. Uzani wa mwili kupita kiasi
Uzito mkubwa unaweza kusababisha mwili kutoa oestrogen iliyozidi, mojawapo ya homoni zinazodhibiti mfumo wa uzazi wa mwanamke.
Kuongezeka kwa viwango vya estrojeni kunaweza kuathiri mzunguko wa hedhi na, katika hali nyingine, kusababisha vipindi kukoma kabisa.
Kwa wanawake walio na amenorrhoea ambao wana uzito kupita kiasi au wana BMI zaidi ya 30, mara nyingi madaktari huwaelekeza kwa mtaalamu wa lishe ili kupata usaidizi katika kufikia uzito wenye afya.
4. Kufanya mazoezi kupita kiasi
Mazoezi makali yanaweza pia kuathiri viwango vya homoni vinavyodhibiti hedhi, na kupoteza kwa mafuta mengi ya mwili kunaweza kuzuia utengenezaji yai.
Kwa wanariadha wa kitaalamu, wataalam wa dawa za michezo wanaweza kushauri juu ya kiasi cha mazoezi kinachoweza kufanywa.

Chanzo cha picha, Getty Images
5. Polycystic Ovary Syndrome (PCOS)
Ovari ya polycystic ina idadi kubwa ya follicles ambayo ni mifuko ambayo mayai hukua. Katika wanawake wenye hali hii, mifuko hii mara nyingi haiwezi kutolewa mayai, na kwa hiyo mchakato huo hautokei.
Nchini Uingereza, NHS inakadiria kuwa PCOS huathiri mwanamke mmoja kati ya 10.

6. Kukoma kwa hedhi
Pamoja na ujauzito na kunyonyesha, kukoma kwa hedhi ni moja ya sababu za asili za amenorrhea.
Wanawake wanapokaribia kukoma hedhi, viwango vya estrojeni huanza kupungua, na uzalishaji wa mayai unakuwa chini ya kiasi cha kawaida.
Kukoma hedhi kwa kawaida hutokea kati ya umri wa miaka 45 na 55.
Hata hivyo, tafiti za kimatibabu zinakadiria kuwa mwanamke mmoja kati ya 100 hupatwa na kukoma hedhi kabla ya kufikia umri wa miaka 40, hali inayojulikana kama kukoma hedhi kabla ya wakati au kushindwa kwa ovari kabla ya wakati.
7. Dawa za kupanga uzazi
Baadhi ya vidonge vya kupanga uzazi, sindano, vipandikizi na vifaa vya ndani ya uterasi vinaweza pia kusababisha amenorrhea.
Hata baada ya kusimamisha uzazi wa mpango, inaweza kuchukua muda kabla ya mwili kuzalisha mayai tena.
8.Hali nyingine za kiafya na dawa za muda mrefu
Hedhi inaweza pia kukosekana kutokana na hali za kiafya za muda mrefu kama vile kisukari au matatizo ya homoni kama vile hyperthyroidism au hypothyroidism.
Amenorrhea inaweza kusababishwa na baadhi ya dawa, kama vile dawa za maradhi ya akili, tiba ya mionzi na matibabu ya shinikizo la damu na mizio, kulingana na Kliniki ya Mayo.
