Wafungwa waliosusia kula chakula kwa muda mrefu zaidi duniani

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Na Asha Juma

BBC Nairobi

Mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda Kizza Besigye alirejeshwa gerezani baada ya kulazwa katika hospitali moja mjini Kampala kwa muda mfupi alipougua kutokana na hatua yake ya kususia kula chakula.

.

Chanzo cha picha, Reuters

Hayo yalijiri baada ya familia ya Besigye kuibua wasiwasi kufuatia kupokea ujumbe kutoka idara ya magereza Uganda iikiitaka familia hiyo itume daktari binafsi wa Besigye.

Mara ya mwisho kwa Besigye kufika mahakamani, alionekana kudhoofika kiafya.

Lakini unajua kuwa kuna wafungwa wengine waliowahi kugoma kula chakula dunia. Je walifanikiwa kufanya hivyo kwa muda gani na kipi kilichowachochea?

Irom Sharmila – aligoma kula kwa miaka 16

.

Chanzo cha picha, AFP

Irom Sharmila alianza mgomo wake wa kususia kula mnamo mwaka 2000 kupinga sheria yenye utata katika jimbo la kaskazini-mashariki la Manipur, ambayo iliipa nguvu zaidi jeshi la India.

Sheria hiyo inaruhusu wanajeshi wa India ambao wamepelekwa katika maeneo ambayo serikali inayachukulia kuwa "yenye vurugu" kukamata watu bila vibali na hata kupiga risasi kukusudia kuua katika hali fulani.

Mnamo mwezi Novemba 10, 2000, raia 10 waliokuwa wamesimama kwenye kituo cha mabasi katika Jimbo la Sharmila la Manipur walidaiwa kupigwa risasi na kuuawa na wanajeshi wa India ambao walidai walikuwa wakiwarushia risasi.

Tukio hilo, lililopewa jina la "mauaji ya Malom" na raia waliokuwa na hasira, na kuwa chanzo cha Sharmila kuanza mgomo wa kutokula. Aliapa kuendeleza mgomo huo hadi sheria hiyo itakapofutwa.

Bi Sharmila alipoanza tu mgomo huo, alikamatwa na kuwa hospitalini kwa miaka 16, akizungukwa na walinzi wenye silaha na timu ya madaktari na wauguzi ambao walimlazimisha kula virutubishi vya kioevu na dawa kwa njia ya bomba, wakati mwingine hadi mara tatu kwa siku.

Wakati huo wote, Sharmila alipata uungwaji mkono mkubwa ulimwenguni na hata alishinda tuzo bora kutoka kwa Tume ya Kutetea Haki za Binadamu ya Asia.

Pia unaweza kusoma:

Mwisho wa kususia kula

.

Chanzo cha picha, AP

Mnamo tarehe 26 Julai 2016, Irom Sharmila, ambaye alikuwa kwenye mgomo wa kula tangu 2000, alitangaza kwamba atamaliza mgomo huo mnamo 9 Agosti 2017.

Na pia, alitangaza kuwa atagombea uchaguzi ujao wa serikali huko Manipur. Kusudi la kujitosa siasani haraka ilikiwa kupigania kuondolewa kwa sheria hiyo tata. Sharmila alisema "nitajiunga na siasa na jitihada zangu za kupinga sheri hili zitaendelea."

Bhagat Singh – aligoma kula chakula kwa siku 116

.

Chanzo cha picha, NO RIGHTS

Bhagat Singh alikuwa raia wa India aliyezaliwa katika wilaya ambayo ilikuwa inamilikiwa na Dola ya Wakoloni wa Uingereza.

Bhagat Singh, alijitahidi kusaidia kupatikana kwa uhuru wa India kutoka kwa Waingereza kupitia mgomo wa kususia kula.

Bhagat Singh na wafungwa wenzake walitangaza mgomo wa kususia kula chakula usio na mwisho kupinga ubaguzi kati ya wafungwa wazungu na weusi na kudai watambuliwe kama 'wafungwa wa kisiasa'.

Mgomo wao ulifuatiliwa na wengi kuanzia vyombo vya habari na kupata uungwaji mkubwa kutoka kwa umma wakitaka matakwa yao yatimizwe.

Singh alipata umaarufu kiasi kwamba serikali ya Uingereza ilijaribu kuzima azma yake kwa kuweka mabakuli ya chakula kwenye seli yake, lakini alikuwa amedhamiria na hakuwahi kugusa chochote.

Mwishowe Singh aliamua kumaliza mgomo wake wa kutokula wa siku 116 mnamo tarehe 5 Oktoba 1929, wakati huo alikuwa amekonda sana.

Mnamo Machi 23, 1931, pamoja na wengine, Bhagat Singh aliuawa kwa kunyongwa.

Bobby Sands – Siku 66

.

Chanzo cha picha, PA Media

Miaka arobaini iliyopita, mnamo Mei 5, 1981, Bobby Sands mwenye umri wa miaka 27, kiongozi wa chama cha IRA katika gereza la Maze nje ya Belfast, mji mkuu wa Kaskazini mwa Ireland alisusia kula hadi akafa.

Chanzo cha mgomo wa kutokula ni wakati serikali ya Labour ya Harold Wilson ilipoondoa haki ya "watu maalum" ambayo iliwaruhusu wafungwa wa IRA, mambo mengi miongoni mwayo, kuvaa nguo zao za nyumbani.

Wengi waliitikia hatua ya serikali ya Wilson ya kuondoa haki ya kuvaa nguo zao gerezani, kwa kubaki uchi.

Mwaka mwaka 1980 mgomo wa kususia kula ulianza wakati wafungwa saba walikataa kula chakula. Walimaliza mgomo huo baada ya siku 53 kwa sababu mmoja wao alikuwa anakaribia kufa.

Waliamini kwamba karibuni wangeruhusiwa kuvaa nguo zao lakini hilo halikutokea.

Mwaka 1981 Machi, Bobby Sands, kiongozi wa IRA gerezani, alianza tena mgomo wa kususia kula, na kuweka wazi kuwa kusudi lake ni kukaa hivyo hadi kufa kwa njaa.

Wafungwa wengine tisa wa Republican walijiunga naye. Na mnamo mwezi Mei, Sands alifariki baada ya siku 66 za kuwa kwenye mgomo wa kususia chakula.

Karibu waombolezaji 100,000 walihudhuria mazishi yake.

Mgomo uliisha baada ya kufikiwa kwa makubaliano na wafungwa wakaruhusiwa kuanza tena kuvaa nguo zao na polepole wakarejeshewa haki zingine.

Solange Fernex – Siku 40

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Alizaliwa mwaka 1934 nchini Ufaransa, Solange Fernex alikua mmoja wa wanasiasa wenye ushawishi mkubwa.

Sera yake kuu ilikuwa kuongeza ufahamu wa athari ya nguvu ya nyuklia katika mazingira, na vile vile uharibifu unaoweza kusababishwa na vinu vya nyuklia.

Kuongeza uhamasishaji juu ya hilo, Solange ilishiriki katika mgomo wa kususia chakula kwa siku 40 akiwa na matumaini kwamba umma utapiga kura kuunga mkono kuachana kabisa na nyuklia.

Cha kusikitisha, hali haikuwa hivyo, lakini hadi leo Solange ameingia katika vitabu vya historia kwa juhudi zake za kishujaa kama mwanaharakati.

Mnamo mwaka 2001 alipewa tuzo ya 'Kuondokana na Nyuklia siku za usoni'.

Na mwezi Novemba 2006 alifariki dunia kwa sababu ya ugonjwa wa saratani.

Cesar Chavez – Siku 36

,

Chanzo cha picha, Getty Images

Cesar Chavez alizaliwa huko Arizona na wazazi waliozaliwa Mexico na alikulia California.

Aliacha shule kwenda kufanya kazi katika tasnia ya kilimo ili kutoa msaada wa kifedha kwa familia yake.

Alianzisha chama cha wafanyikazi wa shamba la kitaifa mnamo 1962. Kusudi lake lilikuwa kuleta mabadiliko ya kuhakikisha mazingira bora ya kazi na kulipa wafanyikazi wa kilimo ambao walijiunga na chama chake.

Alipata uungwaji mkono mkubwa lakini kusudi lake halikutumia.

Chavez alishiriki migomo ya kususia kula mara nyingi lakini iliyokuwa na siku nyingi zaidi ni 36 na kusababisha yeye kupoteza pauni 30.

Chavez alifariki mnamo mwaka 1993, na hukumbukwa kama shujaa kwa kuangazia maswala yanayowakabili wafanyikazi wahamiaji.

Pia unaweza kusoma:

Imehaririwa na Ambia Hirsi