Nenda hospitali ukiona mambo haya kwenye sikio lako

edf

Chanzo cha picha, Getty Images

  • Author, Michael Ilediagu
  • Nafasi, BBC

Kupoteza usikivu au uziwi ni hali inayoweza kumuathiri mtu yeyote, kutoka watoto wachanga hadi watu wazima.

Mtaalamu wa masikio, koo na pua Moses Ayodele Akinola kutoka Nigeria, anazungumzia mambo mbalimbali yanayoathiri masikio na kusababisha upotevu wa kusikia.

Akinolati ameyasema hayo wakati dunia imetoka kuadhimisha Siku ya Usikivu Duniani ambayo hufanyika Machi 3 kila mwaka.

Pia unaweza kusoma

Dalili za tatizo la kusikia

df

Chanzo cha picha, Getty Images

Akinola anataja mambo kadhaa ambayo yanaweza kuashiria kuwa mtu ameanza kuwa na matatizo ya kusikia.

  • Kuanza kupata shida kuelewa kile ambacho mtu mwingine anasema wakati wa mazungumzo.
  • Kuanza kuwaambia watu warudie yale waliyoyasema.
  • Kuanza kusikia vizuri mzungumzaji anapozungumza kwa sauti kubwa.
  • Mtu anapotazama televisheni au anaposikiliza redio kwa sauti ya juu.
  • Kuhisi sauti ya mlio masikioni.
  • Sauti fulani huonekana kuwa kubwa kupita kiasi katika sikio moja.

Ishara kwa watoto wadogo:

  • Kutoshtushwa na kelele kubwa.
  • Kutogeukia chanzo cha sauti akiwa chini ya umri wa miezi 4.
  • Kutosema hata neno moja kufikia umri wa mwaka 1.
  • Kukugundua anapokuona, lakini sio unapoita jina lake.
  • Kusikia sauti fulani lakini sio zingine.
  • Kutoiga sauti au maneno rahisi kufikia umri wa miezi 12.

Sababu za matatizo ya kusikia

gf

Chanzo cha picha, Michael Ilediagu

Maelezo ya picha, Moses Ayodele Akinola

Matatizo ya kusikia, au kupoteza kusikia, yanaweza kusababishwa na mambo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuzeeka, kuathiriwa na kelele kubwa, maambukizo ya sikio, majeraha, dawa fulani, na vinasaba.

Kadiri watu wanavyozeeka, uchakavu wa asili kwenye sikio la ndani na mishipa ya fahamu vinaweza kusababisha upotevu wa kusikia.

Kelele za muda mrefu au kujirudia rudia kwa sauti kubwa kunaweza kuharibu seli za dhaifu kwenye sikio la ndani, na kusababisha upotezaji wa kusikia.

Maambukizi kwenye sehemu ya ndani ya sikio au kati yanaweza kusababisha uvimbe, mkusanyiko wa majimaji, na uchafu unaoweza kuzuia mawimbi ya sauti kufika kwenye sehemu ya ndani ya sikio.

Moses Ayodele Akinola anasema kinachotokea wakati mtu akiwa mjamzito kinaweza kuathiri usikivu wa mtoto na kuathiri ngoma za masikio.

Mfano, ikiwa mama wa mtoto huyo alikuwa akitumia dawa au mtoto huyo alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa usio wa kawaida na kusababisha upotevu wa kusikia.

Sababu nyingine ni mtoto aliyezaliwa na homa ya manjano. Anasema ni vyema kuokoa maisha ya mtoto huyo ili ugonjwa huo usisambae kwenye ubongo wake.

Watu wengine huzaliwa na tatizo la kusikia kwa sababu ya mabadiliko ya jeni, au wanaweza kuwa na tatizo la kutosikia baadaye maishani kwa sababu ya jeni.

Nta wa sikio kuwa mwingi kupita kiasi unaweza kuziba mfereji wa sikio na kuzuia sauti kufikia katika sehemu ya ndani ya sikio.

Katika baadhi ya matukio, kupoteza kusikia kunaweza kuwepo wakati wa kuzaliwa kutokana na uharibifu katika sikio au mishipa.

Hali fulani za kiafya, kama vile kisukari, shinikizo la damu, na kiharusi, zinaweza pia kuchangia kupoteza uwezo wa kusikia.

Jinsi ya kulinda masikio yako

fg

Chanzo cha picha, Getty Images

Ili kulinda masikio yako, epuka kelele nyingi, kaa mbali na kelele nyingi, kama vile matamasha, maeneo ya ujenzi, au maeneo yenye mashine kubwa.

Tumia kinga kuzuia kelele kama vile viziba masikioni inapohitajika. Unaposikiliza muziki au kutazama TV, weka sauti katika kiwango salama.

Pumzika kutoka katika mazingira yenye sauti kubwa. Ikiwa uko katika mazingira yenye kelele, ondoka mara kwa mara ili kuyapa masikio yako nafasi ya kupumzika.

Linda masikio yako kutokana na maji. Epuka kuogelea kwenye maji machafu na kausha masikio yako vizuri baada ya kuogelea.

Usiweke chochote masikioni mwako. Kuwa na tahadhari unapotumia pamba au vitu vingine kusafisha masikio yako, kwani vinaweza kuharibu kiwambo cha sikio.

Dhibiti viwango vya msongo wa mawazo. Viwango vya juu vya mfadhaiko wakati mwingine vinaweza kuchangia matatizo ya kusikia.

Akinola anaendelea kusema ni vyema kwa yeyote mwenye matatizo ya kusikia kwenda hospitali kuonana na daktari. Pata kipimo cha kusikia ikiwa unashuku kuwa unaweza kuwa na matatizo ya kusikia.

Anasema kwa watoto wanaozaliwa wanapaswa kufuatiliwa kwa karibu na kupewa chanjo kwa wakati, kuwakinga na magonjwa.