Wanasayansi wagundua mfumo mpya wa kinga ya mwili

f

Chanzo cha picha, AS

  • Author, James Gallagher
  • Nafasi, BBC News

Mfumo mpya wa kinga ya mwili imegunduliwa. Upo katika sehemu ya mwili inayojulikana kwa kusaga protini na mfumo huo una muundo wa siri ambao unaweza kutapika kemikali zinazoua bakteria.

Watafiti kutoka Israel wanasema ugunduzi huu - utabadilisha uelewa wetu wa jinsi mwili unavyolindwa dhidi ya maambukizi.

Utafiti huu unatoa nafasi mpya ya kutafuta dawa mpya za antibiotiki ili kukabiliana na tatizo linaloongezeka la wadudu ambao ni sugu kwa dawa zetu za sasa.

Mfumo huu upo katika proteasome – eneo dogo ambalo lipo katika kila seli ya mwili. Kazi yake kuu ni kukata protini kongwe na kuzifanya vipande vidogo ili ziweze kuchakatwa na kutengenezwa kuwa protini mpya.

Pia unaweza kusoma
tf

Chanzo cha picha, Weizmann Institute of Science

Maelezo ya picha, Bakteria aina ya Staphylococcus, mmoja akiwa na afya njema upande wa kushoto na mwingine akiharibiwa baada ya gamba lake la juu kupasuliwa na kinga ya mwili iliyotengenezwa na proteasome.

Mfululizo wa majaribio ya maabara, yanayoelezwa katika jarida la Nature, yanaonyesha proteasome ina uwezo wa kutambua seli inapoambukizwa na bakteria.

Ndiposa proteasome hubadilisha muundo na kazi zake. Huanza kuibadilisha protini za zamani kuwa silaha zinazoweza kupasua gamba la nje ya bakteria ili kuwaua.

Prof Yifat Merbl, kutoka Taasisi ya Sayansi ya Weizmann, anasema: "Ugunduzi huu unafurahisha sana, kwa sababu hatukujua kamwe kuwa haya yanatokea.

"Tumegundua mfumo mpya wa kinga ya mwili, ambao unaruhusu kuwa na ulinzi dhidi ya maambukizi ya bakteria.

"Ulinzi huo hutokea katika miili yetu zote na katika seli zote, na huzalisha aina mpya kabisa ya kinga ya asili ya mwili."

Watafiti waliijaribu kinga hii kwa bakteria waliokuwa kwenye maabara na kwenye panya wenye nimonia na wenye sumu katika damu (sepsis). Watafiti wanasema walikuwa wakipata matokeo kama yale ya baadhi ya dawa za antibiotiki zinazopambana na bakteria.

Watafiti walipozichukua seli na kwenda nazo kwenye maabara na kuiondoa proteasome, ilikuwa rahisi sana kwa seli hiyo kuambukizwa bakteria kama Salmonella.

Prof Daniel Davis, mkuu kitivo cha sayansi ya maisha na mtaalamu wa chanjo katika Chuo cha Imperial London, anasema matokeo hayo "yanavutia sana" kwani yamebadilisha uelewa wetu wa jinsi mwili unavyopambana na maambukizi.

"Kinachosisimua sana kuhusu utafiti huu, ni ugunduzi wa mchakato wa kinga ya mwili ambao haukuwa umegunduliwa kabisa, ambapo molekuli za kupambana na bakteria huundwa ndani ya seli zetu, inashangaza sana."

Lakini alionya kuwa kuugeuza mfumo huu wa kinga ya mwili kuwa chanzo kipya cha dawa za kuua bakteria ni wazo ambalo "bado linahitaji kupimwa" na hilo litachukua muda.

fg

Chanzo cha picha, Weizmann Institute of Science

Maelezo ya picha, Prof Yifat Merbl, katikati mwenye nguo nyeusi, pamoja na timu yake ya maabara

Zaidi ya watu milioni moja kwa mwaka wanakadiriwa kufa kutokana na maambukizo ambayo ni sugu kwa dawa kama vile dawa za antibiotiki.

Licha ya hitaji hilo, kumekuwa na ukosefu wa utafiti katika kutengeneza antibiotiki ili kuendana na mahitaji. Kutokana na hali hiyo, ugunduzi huu umetoa mahali papya pa kutafuta antibiotiki.

Dk Lindsey Edwards, mhadhiri wa biolojia katika Chuo cha King's College London, ameiambia BBC: "Ni mgodi wa dhahabu kwa antibiotiki mpya, na hilo linasisimua sana.

"Katika miaka ya nyuma tumekuwa tukichimba sana kutafuta antibiotiki, ni jambo la ajabu kwamba kumbe ni kitu kilicho ndani miili yetu, lakini ilihitajika teknolojia kuweza kugundua vitu hivi."

Pia anasema huenda kusiwe na tatizo kubwa kuifanya kinga hii ya mwili kuwa kuwa dawa ya antibiotiki kwa sababu tayari inatokana na mwili wa binadamu, hivyo inaweza kuwa salama zaidi.