Wakimbizi wa Afghan wanahisi 'kusalitiwa' na agizo la Trump la kuwazuia kuingia Marekani

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Azadeh Moshiri
- Nafasi, BBC News
- Akiripoti kutoka Islamabad
"Ni kama Marekani haielewi kile nilichofanya kwa ajili ya nchi hii, ni kutoaminiana," anasema Abdullah katika mahojiano na BBC.
Alikimbia Afghanistan pamoja na wazazi wake wakati wa kujiondoa kwa Marekani Agosti 2021 na sasa ni mwanajeshi wa angani (paratrooper) katika jeshi la Marekani.
Anahofia kuwa hataweza kuwasaidia dada yake na mumewe kutoroka pia, kutokana na amri ya Rais Donald Trump ya kusitisha mpango wa kuhamisha wakimbizi.
Amri hiyo inafuta ndege zote na maombi ya wakimbizi kutoka Afghanistan, bila kutoa kinga kwa familia za wanajeshi wa Marekani.
Trump anasema uamuzi huo unalenga kushughulikia "viwango vya rekodi vya uhamiaji" vinavyotishia "upatikanaji wa rasilimali kwa Wamarekani".
Hata hivyo, Abdullah na wakimbizi wengine kadhaa kutoka Afghanistan wamesema kwa BBC kuwa wanahisi Marekani "imewaacha" licha ya miaka mingi ya kushirikiana na maafisa wa Marekani, wanajeshi, na mashirika yasiyo ya kiserikali nchini Afghanistan.
Hatuwatumii majina yao halisi, kwani wanahofia kuwa kufanya hivyo kunaweza kuathiri kesi zao au kuleta hatari kwa familia zao.
Haraka aliposikia kuhusu amri hiyo, Abdullah alimpigia simu dada yake.
"Alikuwa analia, ameanza kupoteza matumaini yote," alisema. Anaamini kuwa kazi yake imemfanya dada yake kulengwa na serikali ya Taliban iliyoingia madarakani mwaka 2021.
"Msongo wa mawazo , hauwezi kuelezeka. Anafikiri hatutakuwa na nafasi ya kuonana tena," anasema.
Wakati wa vita, Abdullah anasema alifanya kazi kama mtafsiri kwa jeshi la Marekani.
Alipokuwa akiondoka Afghanistan, dada yake na mumewe hawakuweza kupata paspoti kwa wakati ili kuweza kupanda ndege.
Suhail Shaheen, msemaji wa serikali ya Taliban, aliiambia BBC kwamba kuna msamaha kwa yeyote aliye shiriki na vikosi vya kimataifa na kwamba Wafghani wote wanaweza "kuishi nchini bila hofu". Anadai kuwa wakimbizi hawa ni "wahamiaji wa kiuchumi".
Hata hivyo, ripoti ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2023 ilitilia shaka kuhusu ahadi kutoka kwa serikali ya Taliban.
Ripoti hiyo iligundua kwamba mamia ya maafisa wa zamani wa serikali na wanajeshi walikuwa wameuawa licha ya kuwa na msamaha wa jumla kutoka kwa serikali ya Taliban.
Dada yake Abdullah akiwa na mumewe wamekamilisha mitihani na usaili unaohitajika kabla ya kuhamia Marekani.
BBC imeonyeshwa nakala kutoka idara ya ulinzi ya Marekani ikiidhinisha kuingia kwao Marekani.
Abdullah anasema Trump kudai kuwa idadi ya wakimbizi imeongezeka haingii maanani yeye kunyimwa kuungana na familia yake.
Anasema sasa kupata lepe la usingizi ni nadra na inamtatiza katika shughuli zake za kutoa ulinzi akitumikia taifa la Marekani.
Babak, aliyekuwa mshauri wa sheria kwa wanajeshi wa anga wa Afghan, bado amejificha nchini Afghanistan.
''Hawavunji ahadi tuliokuwa nayo - wanatuvunja pia kiwiliwili chetu.'' anasema.

Chanzo cha picha, Getty Images
Babak anashindwa kuelewa uamuzi wa rais wa Marekani, kwani alifanya kazi bega kwa bega na wanajeshi wa Marekani.
Anasema walikuwa wakitolea maisha yao kwa ajili ya misheni, lakini sasa wako katika hatari kubwa.
Amehamisha familia yake kwa siri na anadai ndugu yake aliteswa kwa sababu ya kutafuta taarifa kuhusu yeye, ingawa BBC haiwezi kuthibitisha madai haya.
Babak anamsihi Trump na Mike Waltz kubadili maamuzi yao, akisema kuwa matumaini yao ya mwisho sasa yamezimika.
Ahmad alifanikiwa kuondoka na kuelekea Marekani katikati ya machafuko ya kujiondoa, lakini sasa ametengana na familia yake.
Alijisikia hana chaguo lingine isipokuwa kuacha baba yake, mama yake, na ndugu zake wa kike na wa kiume waliokuwa vijana.
Anasema kama yeye na baba yake wangekuwa hawakufanya kazi na Marekani, familia yake isingekuwa lengo la serikali ya Taliban.
"Siwezi kulala nikijua kwamba mimi ni miongoni mwa sababu zinazowafanya wawe katika hali hii," anaongeza.
Kabla ya kuchukuliwa madarakani na Taliban, Ahmad alifanya kazi kwa shirika lisilo la kiserikali linaloitwa Open Government Partnership (OGP), lililoanzishwa na Marekani miaka 13 iliyopita na lenye makao yake makuu Washington.
Anasema kazi anayojivunia zaidi ni kuanzisha mahakama maalum kushughulikia ukiukaji wa haki za wanawake.
Lakini anadai kuwa kazi yake katika shirika la OGP na utetezi wake kwa wanawake ulimfanya kuwa lengo la mashambulizi, na a;liwahi kupigwa risasi na wapiganaji wa Taliban mwaka 2021 kabla ya Taliban kuchukua madaraka nchini Afghanistan.
BBC imeshuhudia barua kutoka hospitali moja huko Pennsylvania inayoelezea "ushahidi wa jeraha la risasi na vipande vya risasi" ambavyo wanasema vinakubaliana na maelezo yake kuhusu kilichomtokea Kabul.

Chanzo cha picha, Getty Images
Ahmad anasema familia yake iko hatarini kwa sababu baba yake alikuwa kanali katika jeshi la Afghanistan na alisaidia CIA.
Familia yake ilikimbilia Pakistan baada ya kunyanyaswa na serikali ya Taliban.
BBC imeshuhudia picha za baba na ndugu yake wakitibiwa hospitalini kutokana na majeraha yaliyodaiwa kutokana na mashambulizi ya Taliban.
Familia yake ilikuwa imekamilisha hatua za mpango wa kuhamisha wakimbizi, na Ahmad alitoa ushahidi wa fedha za kutosha kusaidia familia yake bila msaada wa serikali.
Hali ni tete sasa kwani familia yake iko Pakistan kwa visa zitakazomalizika, na IOM imemwambia kuwa "akuwe mvumilivu".
Shirika la #AfghanEvac linakadiria kuwa watu 10,000 hadi 15,000 wako kwenye hatua za mwisho za maombi yao ya kuruhusiwa kuingia Marekani.
Mina, ambaye ni mjamzito, amekuwa akingojea ndege kutoka Islamabad kwa miezi sita. Ana uoga kwamba hofu yake inaweza kuhatarisha mtoto aliye tumboni. "Nikimpoteza mtoto, nitajiua," alisema kwa BBC.
Anasema alikua akipinga kwa ajili ya haki za wanawake, hata baada ya Taliban kuchukua madaraka nchini Afghanistan.
Alidai alikamatwa mwaka 2023 na kuzuiliwa usiku mmoja.
"Hata wakati huo sikutaka kuondoka Afghanistan. Nilijificha baada ya kuachiliwa, lakini waliniita na kusema kuwa wakiniona tena, wataniua," anasema.
Mina ana hofu kuwa serikali ya Pakistan itamrudisha Afghanistan. Hii ni kwa sababu Pakistan haitatoa hifadhi kwa wakimbizi wa Afghanistan milele.
Nchi hiyo imewapokea maelfu ya wakimbizi kutoka Afghanistan kutokana na machafuko ya muda mrefu katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, Pakistan inawahifadhi Wafghani milioni 3, ambapo milioni 1.4 wanahifadhiwa kwa nyaraka.
Huku mvutano mpakani mwa Pakistan na Afghanistan ukizidi kutokota kumekuwa na wasiwasi wafghani wanaohifadhiwa Pakistaniwapo watasalia nchini humo kwa muda mrefu.
Serikali ya Pakistan inasema inawarudisha raia wa kigeni walioko nchini kinyume cha sheria na kuthibitisha kuwa oparesheni za msako zilifanyika Januari.
Kwa mujibu wa IOM, zaidi ya Wafghani 795,000 wamerudishwa kutoka Pakistan tangu mwezi Septemba mwaka jana.
Wakimbizi wa Afghanistan tuliozungumza nao wanahisi wako katika njia panda ambapo kwa nchi yao maisha yako hatarini, na nchi inayowahifadhi ambapo uvumilivu unakwisha hasa baada ya agizo la Trump.
Walikuwa wakitegemea Marekani, lakini kile kilichokuwa kivutio cha usalama sasa kimefungwa na rais mpya hadi taarifa zaidi au kubatilishwa kwa sheria hiyo.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na Ambia Hirsi