Bilionea mwendazake Mohamed Al Fayed anatuhumiwa kwa ubakaji na wafanyakazi wake wa zamani

zx
  • Author, Cassie Cornish-Trestrail, Keaton Stone, Erica Gornall & Sarah Bell
  • Nafasi, BBC

Onyo: Makala hii ina maelezo ambayo baadhi ya watu yanaweza kuwahuzunisha.

Wanawake watano wanasema walibakwa na mmiliki wa zamani wa duka kubwa la kifahari la Harrods, Mohamed Al Fayed walipokuwa wakifanya kazi katika duka la London.

BBC imesikia kauli kutoka kwa wanawake zaidi ya 20 waliokuwa wafanyakazi, ambao wanasema bilionea huyo, aliyefariki mwaka jana akiwa na umri wa miaka 94, aliwanyanyasa kingono - ikiwa ni pamoja na ubakaji.

BBC imekusanya ushahidi kwamba wakati wa umiliki wa Fayed, Harrods sio tu ilishindwa kuingilia kati, pia ilisaidia kuficha madai ya unyanyasaji.

Wamiliki wa sasa wa Harrods wanasema "wanasikitishwa na matukio hayo na kukosa kupata haki waathiriwa wake – na duka hilo linaomba radhi.”

Matukio hayo yametokea London, Paris, St Tropez na Abu Dhabi.

“Niliweka wazi kwamba sitaki. Sikutoa ruhusa,” anasema mmoja wa wanawake hao, ambaye anasema Fayed alimbaka katika nyumba yake ya Park Lane.

Mwanamke mwingine anasema alikuwa msichana alipobakwa huko Mayfair.

"Mohamed Al Fayed alikuwa mnyama, mnyanyasaji wa kingono asiye na maadili," anasema, akiongeza kuwa wafanyakazi wote wa Harrods walikuwa kama "vitu vyake vya kuchezea."

“Sote tulimuogopa. Alitujaza hofu.”

Fayed alikabiliwa na madai ya unyanyasaji wa kingono alipokuwa hai, lakini madai haya ya sasa ni ya ukubwa na uzito ambao haujawahi kushuhudiwa.

Pia unaweza kusoma

'Fayed alikuwa mwovu’

xc

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mtoto wa Fayed alikuwa amechumbiana na Familia ya Kifalme

Kazi ya ujasiriamali ya Fayed ilianza katika mitaa ya Alexandria, Misri, ambapo aliuza vinywaji vikali kwa wapita njia. Lakini ndoa yake na dada wa milionea, mchuuzi wa silaha wa Saudia ndiyo iliyomsaidia kuunda uhusiano mpya na kujenga himaya ya biashara.

Alihamia Uingereza 1974 na tayari alikuwa mtu mashuhuri alipoichukua Harrods mwaka 1985. Katika miaka ya 1990 na 2000, alionekana mara kwa mara kama mgeni kwenye vipindi vya TV na vipindi vya burudani.

Fayed ndiye baba wa Dodi aliyefariki katika ajali ya gari akiwa pamoja na Princess Diana wa Wales, mwaka 1997.

Kwa wanawake ambao tumezungumza nao, wanasema taswira yake ya kupendeza na ya urafiki ilikuwa mbali na uhalisia.

"Alikuwa mwovu," anasema mmoja wa wanawake hao, Sophia, ambaye alifanya kazi kama msaidizi wake binafsi kutoka 1988 hadi 1991. Anasema alijaribu kumbaka zaidi ya mara moja.

Fayed alikuwa na tabia ya kukagua mara kwa mara ghorofa ya chini ili kuwatambua wafanyakazi wasichana wanaomvutia, ambao baadaye angewapandisha cheo kufanya kazi katika ofisi zake za ya juu - wafanyakazi wa zamani, wanaume na wanawake, walituambia.

Unyanyasaji wake aliufanya katika ofisi za Harrods, katika nyumba yake ya London, au katika safari za nje - mara nyingi huko Paris katika hoteli ya Ritz, ambayo pia anaimiliki, au katika jengo lake la Villa Windsor.

'Alinibaka'

Rachel, sio jina lake halisi, alifanya kazi kama msaidizi wake binafsi katika duka la Harrods katika miaka ya 1990.

Usiku mmoja baada ya kazi, anasema alimwita kwenye nyumba yake ya kifahari, huko Park Lane. Jengo hilo lilikuwa likilindwa na wafanyakazi wa usalama.

Rachel anasema Fayed alimtaka aketi kwenye kitanda chake kisha akaweka mkono wake mguuni, akiweka wazi anachotaka.

"Nakumbuka nilihisi mwili wake juu yangu, uzito wake. Alinibaka."

BBC imezungumza na wanawake 13 ambao wanasema Fayed aliwanyanyasa kingono katika nyumba ya 60 Park Lane. Wanne kati yao, akiwemo Rachel, wanasema walibakwa.

Sophia anasema alinyanyaswa kingono: “Sikuweza kuondoka. Sikuwa na familia ya kurudi, nilitakiwa kulipa kodi,” anasema.

Gemma, aliyefanya kazi kama mmoja wa wasaidizi wa binafsi wa Fayed kati ya 2007-09, anasema tabia yake ilitisha zaidi wakati wa safari za kikazi nje ya nchi.

Anasema alibakwa katika nyumba Villa Windsor huko Bois de Boulogne mjini Paris - nyumba ya zamani ya Mfalme Edward VIII na mkewe Wallis Simpson.

Anasema baada ya Fayed kumbaka alilia. Fayed alinyanyuka na kumwambia kwa ukali akaoge na Dettol.

"Ni wazi alitaka nifute ushahidi wowote wa yeye kuwa karibu nami," anaeleza.

Wanawake wengine wanane pia wametuambia walinyanyaswa kingono na Fayed huko Paris. Wanawake watano walitaja unyanyasaji huo kama jaribio la ubakaji.

‘Siri iliyo wazi’

"Unyanyasaji wa wanawake, niliufahamu nilipokuwa dukani," anasema Tony Leeming, meneja wa Harrods kutoka 1994 hadi 2004. "Haikuwa siri,” Lakini anasema hakujua kuhusu madai mazito ya ubakaji.

Kauli ya Leeming unaungwa mkono na wanachama wa zamani wa timu ya usalama ya Fayed.

"Tulifahamu alikuwa akipenda sana wasichana wadogo," anasema Eamon Coyle, ambaye alijiunga na Harrods mwaka 1979 kama mpelelezi wa duka, kisha akawa naibu mkurugenzi wa usalama kuanzia 1989-95.

Steve, ambaye hataki tutumie jina lake la ukoo, alifanya kazi kwa bilionea huyo kati ya 1994-95. Alituambia wafanyakazi wa usalama "walijua mambo fulani yalikuwa yakitokea kwa wafanyakazi fulani wa kike huko Harrods na Park Lane."

Wanawake wengi walituambia walipoanza kufanya kazi kwa Fayed walipitia vipimo vya afya vilivyofanywa na madaktari.

Lakini hawakuona matokeo ya vipimo hivyo - ingawa yalitumwa kwa Fayed.

"Utamaduni wa hofu"

Wanawake wote tuliozungumza nao walieleza kuwa hofu ndiyo ilifanya iwe vigumu kwao kuzungumza.

Sarah, si jina lake halisi, anasema: “Hakika kulikuwa na utamaduni wa hofu katika duka zima - kutoka watu wa hali ya chini, hadi wakuu.”

Wengine walituambia wanaamini kuwa simu katika duka la Harrods zilikuwa zikifuatiliwa - na wanawake walikuwa wakiogopa kuzungumza wao kwa wao kuhusu unyanyasaji wa Fayed, wakihofia kuwa walikuwa wakirekodiwa na kamera zilizofichwa.

Aliyekuwa naibu mkurugenzi wa usalama, Eamon Coyle, alithibitisha hili – anasema miongoni mwa majukumu yake ilikuwa ni kusikiliza kanda za mazungumzo ya simu yaliyorekodiwa. Kamera ambazo zinaweza kurekodi pia ziliwekwa kwenye duka lote, alisema, pamoja na vyumba vya watendaji.

Harrods inasema katika taarifa yake kwa BBC kuwa haya yalikuwa ni matendo ya mtu "mwenye nia ya kutumia vibaya mamlaka yake" na inalaani vikali.

"The Harrods ya leo ni shirika tofauti sana na lile lililomilikiwa na kudhibitiwa na Al Fayed kati ya 1985 na 2010, ni shirika ambalo linaweka ustawi wa wafanyakazi wake katika kila kitu inachofanya."

Majaribio ya kufichua matendo yake

z

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wamiliki wapya wa Harrods walianza kusuluhisha madai ya waathiriwa wa Fayed mnamo 2023

Kulikuwa na majaribio kadhaa ya kufichua tuhuma dhidi ya Fayed kabla ya kifo chake – moja kupitia jarida la Vanity Fair mwaka 1995 - katika makala iliyoeleza kuhusu ubaguzi wa rangi, ufuatiliaji wa wafanyakazi na tabia mbaya za ngono. Lakini Fayed alifungua kesi ya kashfa.

Mohamed Al Fayed baadaye alikubali kufuta kesi hiyo ikiwa ushahidi uliokusanywa na gazeti hilo kuhusu utovu wake wa kingono utafutwa.

Mwaka 1997, The Big Story ya ITV iliripoti madai mengine mazito ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa kijinsia na kupapasa.

Mmoja wa wanawake katika uchunguzi wa BBC, Ellie, sio jina lake halisi, alikuwa na umri wa miaka 15 mwaka 2008 aliporipoti unyanyasaji kwa polisi - madai ambayo yalichukua vichwa vya habari - lakini haikusababisha mashtaka yoyote.

Mwaka 2017, Channel 4 iliripoti madai ya kupapasa, kushambulia na kunyanyasa, mwanamke huyo alikuja hadharani na iliwapa wanawake wengine ujasiri wa kujitokeza - na uchunguzi wa 2018 kwenye Channel 4 News ulifanyika.

Lakini tangu Mohamed Al Fayed kufariki mwaka jana, wanawake wengi zaidi wameweza kuzungumza hadharani kuhusu ubakaji na jaribio la ubakaji.

Fedha na makubaliano

Makala ya BBC inafichua kwamba, sehemu ya suluhu ya mwaka 2009, ilimbidi Germma kutia saini makubaliano ya kutofichua tuhuma hizo, mkataba unaomzuia kisheria na unaohakikisha habari inabaki kuwa siri.

Anasema baada ya kubakwa, aliwasiliana na wakili ambaye alimwambia kuwa anaacha kazi kwa sababu za unyanyasaji wa kijinsia.

Harrods ilikubali, anaweza kuondoka na itamlipa kiasi cha pesa, lakini asivujishe ushahidi na badala yake asaini makubaliano hayo. Gemma anasema mfanyakazi wa ofisi ya rasilimali watu (HR) kutoka Harrods alikuwepo wakati makubaliano yakifanyika.

BBC imeelezwa na wanawake waliotishwa na mkurugenzi wa usalama wa wakati huo wa Harrods, John Macnamara, ili kuwazuia wasizungumze.

Wanawake kumi na wanne tuliozungumza nao wamefungua mashitaka dhidi ya Harrods wakitaka fidia. Wamiliki wa sasa wa duka, walianza kusuluhisha kesi hizi mwezi Julai 2023.

Ilimchukua Sophia na Harrods miaka mitano kufikia makubaliano. Wanawake wengi zaidi sasa wanatarajia kuchua hatua za kisheria dhidi ya Harrods.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah