Kwanini Kapteni Ibrahim Traoré ni maarufu miongoni mwa vijana wa Afrika?

nmn

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kiongozi wa sasa wa mpito wa Burkina Faso aliingia madarakani kupitia mapinduzi ya Septemba.

Maelfu ya watu walikusanyika katika Uwanja wa Mapinduzi mjini Ouagadougou siku ya Jumatano tarehe 30 Aprili kumuunga mkono Rais wa mpito, Kapteni Ibrahim Traoré.

Maandamano hayo yalifanyika baada ya Kamanda wa AFRICOM wa Marekani, Jenerali Michael Langley, kusema mbele ya Kamati ya Kijeshi ya Seneti ya Marekani mapema mwezi Aprili kwamba utawala wa kijeshi unaotawala Burkina Faso unatumia rasilimali za nchi hiyo, hasa akiba ya dhahabu, kwa ajili ya kujilinda wao wenyewe badala ya kuwalinda raia.

Kauli hiyo ya Jenerali Langley ilisababisha hasira na mshtuko miongoni mwa watu wa Burkina Faso na nchi nyingine za Afrika ya Kati na Magharibi na hata nje ya ukanda huo.

Serikali ya Burkina Faso ililaani kauli hiyo iliyotolewa na uongozi wa kijeshi wa Marekani, ikisema inalenga "kuharibu taswira ya nchi."

Tazama hapa
Maelezo ya video, Traoré 'chupuchupu' kupinduliwa Burkina Faso
Unaweza pia kusoma

Mamia ya ujumbe na machapisho ya kumuunga mkono Kapteni Traoré yamejaa kwenye mitandao ya kijamii katika kipindi cha hivi karibuni.

Kupitia jukwaa la X (zamani Twitter), wasanii, wanaharakati, viongozi vijana wa Kiafrika na hata Wamarekani Weusi walionesha hasira zao kutokana na kauli aliyoitoa Jenerali Langley wa Marekani.

Uungaji mkono huu mkubwa kwa kiongozi wa kijeshi wa Burkina Faso, Kapteni Ibrahim Traoré, unakuja wakati wa mvutano unaoongezeka kati ya nchi hiyo na mataifa ya Magharibi.

Shutuma za ufisadi alizotoa Jenerali Langley dhidi ya Rais wa mpito, Kapteni Ibrahim Traoré, badala ya kudhoofisha utawala wa kijeshi wa Burkina Faso, zimeimarisha hadhi na mvuto wa kiongozi huyo wa kijeshi, ambaye umaarufu wake umevuka mipaka ya kitaifa.

Kwa miaka kadhaa, Burkina Faso imekumbwa na mashambulizi ya wapiganaji wa kijihadi yaliyosababisha vifo vya maelfu ya watu na kuwafikisha zaidi ya watu milioni mbili kuwa wakimbizi wa ndani.

Alipochukua madaraka mnamo Septemba 2022, Kapteni Ibrahim Traoré aliahidi kuwa mapambano dhidi ya ugaidi yatakuwa kipaumbele chake kikuu.

Alianzisha kampeni kubwa za ajira za kujitolea katika shughuli za ulinzi wa taifa (VDP), akaongeza operesheni za kijeshi, na kuimarisha uwezo wa vikosi vya ulinzi.

Mtazamo wake wa kishujaa dhidi ya makundi yenye silaha ulimletea uungwaji mkono mkubwa kutoka katika kundi kubwa la wananchi.

Hata hivyo, umaarufu wa Traoré unazidi tu kuongezeka miongoni mwa utawala wa kijeshi na raia. Amefanya mageuzi makubwa ya msingi yanayovutia sehemu kubwa ya jamii.

nmn

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wafuasi wa Kapteni Ibrahim Traore wakiwa wamebeba bendera za Burkina Faso na Urusi kuonesha mshikamano na Traore , Ouagadougou, 30 Aprili 2025.

Sauti ya uhuru na ya wazi

Traoré aliimarisha msimamo wa kupinga ubeberu, ambapo alikosoa vikali uingiliaji wa madola ya Magharibi, hasa Ufaransa.

Uamuzi wake wa kujielekeza kwa washirika wapya kama Urusi na Iran, na kujiondoa kwenye baadhi ya miungano ya ushirikiano wa kikanda (kama vile G5 Sahel na ECOWAS), umeonekana kama njia ya kudhihirisha mamlaka kamili ya taifa.

Mabadiliko haya ya kiusawa wa dunia yamewapendeza sana vijana wanaotafuta uhuru wa kisiasa na kiuchumi.

Umaarufu wa Rais Ibrahim Traoré miongoni mwa vijana unachangiwa zaidi na msimamo wake wa kupinga ubeberu na hotuba zake za kutetea mamlaka ya taifa, kwa mujibu wa mwandishi wa habari na mwandishi Seidik Abba, mtafiti mshiriki na Rais wa Kituo cha Kimataifa cha Tafakari na Tafiti kuhusu Sahel (CIRES).

"Kwanza kabisa, ni msimamo wake wa kupinga ubeberu. Jinsi anavyopinga mataifa ya kigeni kuingilia mambo ya nchi yake inaendana na matarajio ya vijana wengi wa Kiafrika waliokata tamaa na mfumo wa zamani ambapo mataifa ya Afrika yalikuwa yakipokea maagizo kutoka kwa wakoloni wao wa zamani au kutoka kwa mfumo wa kimataifa.

Huu msimamo wa kizalendo na wa kupinga ubeberu umemfanya kuwa maarufu sana kwa vijana," alisema Abba.

Katika hotuba zake nyingi, huwa anasisitiza dhamira yake ya "kurejesha mamlaka na fahari kwa watu wa Burkina Faso".

Alionya tarehe 1 Aprili 2025, wakati wa hafla ya kitaifa, kwamba "hatutakuwa na huruma wala msamaha kwa watu wanaotaka kuzuia maendeleo ya taifa letu."

Msimamo huu umewagusa vijana wengi ambao sasa wanajitambulisha na kauli hii ya kupinga mataifa ya Magharibi, kama anavyoeleza Seidik Abba.

Mwandishi huyu wa habari kutoka Nigeria alisema, "pia ni kuhusu namna anavyoongea,anavyotoa matamko yake waziwazi, bila kuzingatia sana tahadhari za kidiplomasia, akiwashambulia Ufaransa na vyombo vya habari anavyovishutumu kuwa karibu na nchi za Magharibi – yeye ni kijana."

Lakini Daniel Eizenga, mtafiti kutoka Kituo cha Mafunzo ya Kimkakati kwa Afrika kilichoko Washington DC, Marekani, anasisitiza kuwa umaarufu wa Traoré kwa wananchi wa kawaida unapaswa kuangaliwa kwa makini katika muktadha wa kurudisha nyuma demokrasia na ukosefu wa uhuru wa kujieleza.

Alisema, "baada ya kufanya mapinduzi mwaka 2022, Kapteni Traoré alitumia hotuba za kupinga ubeberu kuchochea uungwaji mkono wa kisiasa. Hatua hii inaonekana kuwa maarufu miongoni mwa kizazi kipya kilicho na ufuasi mkubwa katika mitandao ya kijamii. Lakini umaarufu wa Traoré kwa wananchi wa kawaida una kasoro. Traoré anahusishwa na ongezeko la ukandamizaji dhidi ya wakosoaji wake. Akiwa kiongozi wa jeshi lililochukua mamlaka, amekandamiza vikali sauti huru."

"Waandishi wa habari, viongozi wa asasi za kiraia, viongozi wa vyama vya siasa, na hata majaji wamekuwa wakilengwa na utawala wake kwa kutumia nguvu na ukandamizaji wa kimabavu."

"Wananchi waliotoa wito wa mabadiliko wamekuwa wakitekwa, kuzuiliwa, kupotezwa, na kupelekwa mstari wa mbele baada ya kulazimishwa kujiunga na wanamgambo wa taifa."

nmn

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kapteni Ibrahim Traoré, Rais wa Mpito, akimpokea Rais wa Senegal Bassirou Diomaye Faye tarehe 30 Mei 2024

Je ni Sankara mpya?

Kapteni Traoré amekuwa ishara ya upinzani dhidi ya ushawishi wa Mataifa ya Magharibi, hasa Ufaransa, na jambo hili limepokelewa vyema na idadi kubwa ya vijana.

Msimamo wake wa kimapinduzi na kujizatiti katika umoja wa Afrika unavutia wengi wa watu wa Burkina Faso, hasa vijana.

"Kuna kipengele cha tatu kwangu: ukweli kwamba ujana wa Ibrahim Traoré, ujasiri wake wa kusema mambo wazi na msimamo wake dhidi ya ubeberu vinafanana na rais mwingine wa Burkina Faso, Kapteni Thomas Sankara, ambaye umaarufu wake karibu miaka 40 baada ya kifo chake hauwezi kutiliwa shaka," alisema Seidik Abba, Rais wa Kituo cha Kimataifa cha Tafiti kuhusu Sahel (CIRES).

Utawala wa kijeshi ulio madarakani nchini Burkina Faso umeendelea kufanya kwa vitendo ili kuimarisha sura yake kwa umma. Uamuzi wa Kapteni Traoré kuachana na mshahara wa rais na kuchukua mapato ya kawaida kama kiongozi wa jeshi pia umemletea umaarufu.

Kwa Daniel Eizenga, mtafiti kutoka Kituo cha Mafunzo ya Kimkakati kwa Afrika kilichoko Washington D.C., Marekani, kufanya ulinganifu baina ya Traoré na Sankara kunatokana na baadhi ya sifa, zaidi ni hisia tu.

"Ni kweli kwamba wote walichukua madaraka wakiwa na umri wa miaka 34. Lakini kufanana kwao kunafikia kikomo kwa vyeo na umri wao.

Sankara alipata madaraka miaka ya 1980, katika kipindi cha mwisho wa Vita Baridi na migawanyiko ya kiitikadi ndani ya jeshi. Maafisa waliomuunga mkono waliongoza mapinduzi mwaka 1983. Sankara alionekana kama mpinduzi wa Kijamaa.

Alijaribu kutekeleza mageuzi ya kisiasa: kuongeza ushiriki wa kisiasa, kuwawezesha wanawake, kupambana na ukataji miti hovyo, na kupunguza pengo la kijamii."

"Traoré, kwa upande mwingine, anatawala katika mazingira hatari zaidi ambapo uwezekano wa kupinduliwa ni mkubwa. Mapinduzi yake, kama ya Damiba, yanaonyesha kuwa jeshi lina makundi tofauti: maafisa wengi wa kijeshi hawakuhusika moja kwa moja katika mapinduzi hayo."

Kwa mujibu wa serikali yenyewe, utawala wa kijeshi umekumbwa na majaribio kadhaa ya kutaka kuudhoofisha. Hili linaonyesha jinsi mabadiliko ya madaraka yalivyokuwa ya ghafla na jinsi hali ya kisiasa isivyo imara chini ya utawala wa kijeshi.

Tangu alipopata madaraka mwaka 2022, Kapteni Ibrahim Traoré amechukua hatua mbalimbali za kurejesha udhibiti wa serikali juu ya rasilimali za madini, hasa dhahabu, ambayo ndiyo bidhaa kuu ambayo huuzwa nje na taifa hilo.

Mwezi Oktoba 2024, alitangaza kufuta baadhi ya leseni za uchimbaji madini zilizotolewa kwa makampuni ya kigeni, na kusema: "Tunajua kuchimba dhahabu yetu, na sielewi kwa nini tunawaachia makampuni ya kimataifa kazi hiyo."

Uamuzi huu ni sehemu ya juhudi kubwa ya kurudisha sekta ya madini mikononi mwa wananchi wa nchi hiyo ili kuhakikisha kuwa watu wa kawaida wananufaika zaidi na rasilimali za taifa.

Serikali pia ilichukua usimamizi wa migodi miwili ya dhahabu, Boungou na Wahgnion, kwa gharama ya takriban dola milioni 90, na hivyo kukomesha mgogoro kati ya makampuni ya uchimbaji madini Endeavour Mining na Lilium Mining.

Lakini kwa mujibu wa Daniel Eizenga wa Kituo cha Mafunzo ya Kimkakati kwa Afrika, hatua za Traoré hazijaboresha hali ya usalama – bali zimeifanya kuwa mbaya zaidi tangu achukue madaraka mwezi Oktoba 2022.

"Mamlaka ya kijeshi ya Burkina Faso iko chini ya shinikizo kubwa. Hali ya usalama imezorota sana tangu Traoré achukue madaraka, na idadi ya vifo vinavyotokana na mashambulizi ya wanamgambo wa Kiislamu imekaribia kuongezeka mara mbili katika kipindi chake cha uongozi.

Jeshi limepata hasara kubwa, mamia ya wanajeshi wameuawa katika mashambulizi mwaka 2024.

Idadi ya watu waliolazimika kuhama kutokana na ukosefu wa usalama imeongezeka hadi zaidi ya 10% ya idadi ya watu.

Maelfu ya shule zimelazimika kufungwa kutokana na hali hiyo, na hivyo kizazi kizima cha watoto kimeachwa bila elimu."

Mwelekeo huu umetokea katika kipindi ambacho mamalaka ya kijeshi yameimarishwa kwa karibu 70% katika miaka miwili iliyopita hadi kufikia karibu dola bilioni moja – sawa na takriban 18% ya matumizi ya serikali.

Hii ni ongezeko la zaidi ya 10% katika matumizi ya serikali tangu mapinduzi ya kijeshi ya Traoré mwaka 2022.

"Kwa hiyo, ni vigumu kuelewa jinsi bajeti ya ulinzi ilivyoongezeka kiasi hicho bila mafanikio ya kuridhisha kwenye uwanja wa mapambano au maboresho ya hali ya kibinadamu. Maelezo rahisi zaidi ni kwamba Traoré ametumia fedha hizi kulinda utawala wake mwenyewe."

"Kujitenga na mataifa ya magharibi na kuhuisha msimamo wa kijiografia"

Kapteni Ibrahim Traoré mara kwa mara ameeleza wasiwasi wake kuhusu juhudi za mataifa ya kigeni kuingilia mambo ya ndani ya Burkina Faso.

Hasa, amezishutumu baadhi ya nguvu za kibeberu kwa kutaka kunufaika na utajiri wa nchi hiyo kwa kutumia ugaidi kama chombo cha kuleta machafuko. Alisema:

"Sisi ni waathirika wa utajiri wetu, utajiri ambao mabeberu wanataka kuuchukua kwa gharama yoyote ili kutuweka katika utumwa."

"Nchi za ESA zimejikita katika mchakato wa kurejesha mamlaka yao kamili," alisema katika mkutano wa kilele wa nchi za ESA mwezi Julai 2024.

Katika muktadha huu, Burkina Faso imeimarisha mahusiano na washirika wake wasio wa Magharibi, kama Urusi, huku ikijiondoa kutoka kwa baadhi ya washirika wa jadi.

Alianza kwa kugeuka dhidi ya Ufaransa, koloni la zamani, ambapo aliwaambia wanajeshi wa Ufaransa waliokuwa nchini humo kuondoka mwanzoni mwa mwaka 2023 na pia kuwaamuru wanadiplomasia waondoke.

Mwelekeo huu mpya wa kijiografia unaakisi shauku ya kutanua ushirikiano wa kimataifa na kuimarisha mamlaka ya kitaifa.

Hata hivyo, kwa mchambuzi Daniel Eizenga, kuna upande wa hasara kwa mkakati huu wa kidiplomasia kwa upande wa serikali ya mpito ya kijeshi, ambayo inazidi kukabiliwa na shinikizo kubwa.

"Traoré ameacha ushirikiano wa usalama na mataifa mengi ya Magharibi.

Ushirikiano huu wa kiusalama haukuwa na gharama yoyote ya kifedha kwa wananchi wa Burkina Faso.

Hali ni tofauti na Urusi. Juhudi za Bwana Traoré kuimarisha uhusiano na Urusi zimemfanya atoe mikataba ya uchimbaji madini kwa makampuni ya Kirusi."

Vivyo hivyo, kuna mazungumzo mengi kuhusu jinsi ushirikiano mkubwa zaidi na Urusi unaweza kusaidia kutatua hali ya usalama na kibinadamu inayozidi kuwa mbaya nchini humo.

Hata hivyo, mwaka 2024, Burkina Faso ilishuhudia mashambulizi mabaya zaidi kuwahi kutokea kutoka kwa wanamgambo wenye msimamo mkali dhidi ya wanajeshi na raia.

Zaidi ya wanajeshi 100 waliuawa katika shambulio moja kwenye kambi ya kijeshi huko Mansila mwezi Juni 2024.

Mamia ya raia waliuawa katika shambulio jingine karibu na mji wa Barsalogho mwezi Agosti 2024.

Tangu Traoré achukue madaraka na kuimarisha mahusiano na Urusi, tumeona pia jinsi vikosi vya usalama vinavyolenga raia.