Je, maji yaliyochujwa ni bora kuliko maji ya bomba?

Chanzo cha picha, Alamy
Vichujio vya maji vinaweza kuondoa uchafu kutoka kwa maji ya bomba - lakini ni muhimu kiasi gani na je, vinaweza kusababisha madhara bila kukusudia?
Ikiwa inawezekana, Shima Chin-See ataepuka kunywa maji moja kwa moja kutoka kwenye bomba. Jokofu lake nyumbani ambapo anaishi na familia yake, ina chujio ya maji ambayo imeunganishwa na kichungi kwa ajili ya kusafisha maji kupitia chipu ya urujuanimno iliyopachikwa kwa juu.
"Maji yaliyochujwa yana ladha nzuri," anasema Chin-See. "Kuna harufu ya kemikali kwenye maji ya bomba na hata ukinywa unaweza kusikia."
Hata hivyo, baadhi ya watu wanamuona wa ajabu akisema hivyo akiwemo mume wake.
Likini imejitokeza kuwa Chin-See hayuko peke yake. Shirika lisilo la serikali la Mazingira lilikusanya watu 2,800 wanaoishi kote nchini Marekani na nusu ya idadi hiyo walisema kuwa maji ya bomba sio salama kwa kunywa huku karibu asilimia 35 ya idadi hiyo wakiwa wanachuja maji yao.
Kulingana na utafiti uliofanywa mwaka 2023 kwa zaidi ya watu 500 nchini Uingereza na Shirika la Sweden linalochuja maji maji ya bomba, asilimia 42 hawaamini au wanapenda ladha ya maji ya bombani.
Robo ya idadi hiyo waliamini kuwa maji yao ya bombani sio safi, yana kemikali na hata bakteria. Matokeo yake ni kwamba, zaidi ya nusu ya wakaazi wa London walisema kuwa wanatumia maji yaliyochujwa.
Watetezi wanasema kuwa kuchuja maji kunaweza kuleta faida nyingi, kuanzia kuondoa sumu na vimelea vya magonjwa hadi kupunguza ugumu na kuboresha harufu na ladha.
Lakini je, maji yaliyochujwa ni bora kwako kuliko maji kutoka kwenye bomba?
Aina za kuchuja
Kwa wale wanaopendelea kuchuja maji yao, kuna aina nyingi za kuchuja maji.
Vichungi pia hutofautiana katika aina ya nyenzo ambazo zimetengenezwa na hutumia teknolojia tofauti – kwa mfano, ubadilishanaji wa ioni, ‘Reverse Osmosis’ yaani teknolojia ambayo hutumiwa kuondoa idadi kubwa ya uchafu kutoka kwa maji kwa kusukuma maji chini kwa shinikizo kupitia utando unaoweza kupenyeza nusu, na kutenganisha kemikali ndio maarufu zaidi - kuondoa maji kutoka kwa molekuli zingine.
"Vichungi tofauti vinaweza kutimiza malengo tofauti," anasema Detlef Knappe, profesa wa uhandisi wa kiraia, ujenzi, na mazingira katika Chuo Kikuu cha Jimbo la North Carolina.
Muhimu ni kuelewa kilicho ndani ya maji yako na kama kinahitaji kuondolewa, kisha utafute kichujio kinachofaa kufanya hivyo.
Njia za kuzuia sumu na kemikali kwenye maji
Bila shaka, manufaa ya kuchuja maji ya bomba hutegemea mahali unapoishi duniani.
Katika nchi zinazoendelea ambapo jamii zinatatizika kupata maji safi ya kunywa, "tatizo kuu ambalo tunahofia ni bakteria kama E.coli na Legionella," anasema Brent Krueger, profesa wa kemia na mkurugenzi mwenza wa Global Water Research, taasisi katika Chuo cha Hope cha Michigan.
Maji chafu yanaweza kusababisha ugonjwa wa kuhara, ugonjwa unaozuilika ambao unaua takriban watu milioni moja kila mwaka, karibu nusu yao wakiwa watoto chini ya miaka mitano.
Vichungi vya maji, hata hivyo, vinaweza "kuwa vizuri sana katika kuzuia bakteria," anasema Krueger, ambaye timu yake imeongoza juhudi hizo katika eneo la Amerika ya Kusini.
Katika jaribio moja, waliweka vichungi katika nyumba kwenye vijiji 16 vya Jamhuri ya Dominika.
Hii ilisababisha matukio ya kuhara kupungua kutoka asilimia 25.6 hadi chini ya asilimia 10, na kusababisha athari zingine. "Watoto hukosa Kwenda shule kidogo, na watu wazima hukosa kufanya kazi kwa siku kadhaa zenye kusaidia kuleta kipato kwa familia pia," anasema Krueger.

Chanzo cha picha, Getty Images
Suala jingine ni madini ya risasi yanayoruhusiwa katika mabomba, lakini mara nyingi hali huwa mbaya hasa katika nyumba za kitambo na inaweza kuwa tatizo.
"Mabomba yenye kutu ni tatizo kubwa. Ninaona sumu nyingi ya madini ya risasi kutoka kwa mabomba ya maji ya zamani," anasema Nirusa Kumaran, daktari huko London na mkurugenzi wa matibabu wa kituo cha ustawi HUM2N.
Katika hali hizi, vichungi vinaweza kusaidia kuondoa madini ya risasi kutoka kwa maji.
Zaidi ya hayo, Kumaran anasema inaweza kuwa njia ya kipekee kuzuia sumu na kemikali zingine zilizopo kwenye maji.
Sumu moja katika maji ya bomba ambayo inatia wasiwasi baadhi ya wataalam ni kundi la zaidi ya kemikali 15,000 zinazotengenezwa na binadamu zinazoitwa PFAS.
Pia huitwa "kemikali za milele" kwa sababu zinaendelea kuwepo katika mazingira bila kuharibika, PFAS inahusishwa na maswala mengi ya kiafya, pamoja na saratani, uharibifu wa ini na kupungua kwa uzazi.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Tuna wasiwasi juu ya viwango vya chini sana vya kemikali kwa sababu PFAS fulani inaweza kujilimbikiza katika mwili wa binadamu kwa njia ya kushangaza," anasema Knappe.
"Kuna viwango vya chini vya PFAS katika karibu vyanzo vyote vya maji kote ulimwenguni kwa sasa."
Kwa mfano, angalau PFAS moja iligunduliwa katika sampuli za maji ya kunywa zilizochukuliwa kutoka kwa makampuni 17 kati ya 18 ya maji ya Uingereza mwaka wa 2023.
Nchini Marekani, PFAS inapatikana katika asilimia 45 ya maji ya bomba, na sita katika kila watu 10 wanaaminika kuathiriwa na kemikali.
Kwa bahati nzuri, vichungi vya maji vinaweza kusaidia kuondoa kemikali hizi hatari.
Madini muhimu yanayoweza kuondolewa kwa kuchuja
Ingawa vichungi vinaweza kusaidia katika kuondoa kemikali hatari kutoka kwa maji, wakati mwingine huondoa madini yenye faida pia.
Hizi ni pamoja na magnesiamu na kalsiamu, madini ya chuma na manganese, ambayo huondolewa ili kufanya maji kuwa laini na kuzuia kubadilika kwa rangi.
Vichungi vinaweza pia kuondoa madini ya floraidi, ambayo baadhi ya manispaa huongeza kwenye maji ya bomba ili kusaidia kukabiliana na kuoza kwa meno.
Baadhi ya watu hunyunyiza chumvi kidogo ya bahari kwenye maji yao yaliyochujwa, hata hivyo kwa sasa hakuna ushahidi kwamba hatua hii ni nzuri katika kuongeza madini yaliyopotea.
Lakini kwa kweli, ni muhimu zaidi kupata madini haya muhimu kwa lishe yako, Kumaran anasema. "Hatupaswi kutegemea maji yetu ya kunywa kama chanzo kikuu cha madini."
Mwisho wa siku, kuamua kutumia kichujio cha maji au kutotumia inatokana na kuelewa aina ya maji katika eneo lako, pamoja na unavyotaka mwenyewe na kiwango cha kukubalika cha kile kilicho ndani ya maji hayo.