Mvutano wa Marekani - China: Fahamu nguvu za kijeshi kati ya mataifa haya mawili

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Ramani inayoonyesha uwezo wa kijeshi kati ya Marekani na China

Wiki chache baada ya Rais wa Marekani kutuma onyo kwa China kuhusu Taiwan, serikali ya Beijing ilitoa jibu kali zaidi kuwahi kutokea.

Taarifa iliyotolewa na serikali ya China ilisema kwamba "itashinda jaribio lolote" la kutafuta uhuru kutoka kwa Taiwan.

Waziri wa Ulinzi wa China, Jenerali Wei Feng, pia wiki hii aliishutumu Marekani kwa kurudisha nyuma uhuru wa kisiwa hicho, akisema kuwa Marekani "ilivunja ahadi yake kwa Taiwan" na "inaingilia" masuala ya China.

“Niseme wazi, iwapo mtu yeyote atajaribu kutenganisha Taiwan na China, hatutasita kuingia vitani,” alisema Jenerali Wei Fenge, alipozungumza kwenye Mkutano wa Usalama wa Asia huko Singapore.

"Tutaingia kwenye vita ambapo kila kitu kitapotea na tutapigana hadi mwisho. Hiyo ndiyo njia pekee iliyo wazi kwa China," aliendelea.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rais wa Marekani Joe Biden

Maoni hayo makali ya Waziri wa Ulinzi wa China yalifuatia ujumbe wa hivi karibuni wa Rais wa Marekani, Joe Biden, kwa China, ambapo alisema kuwa "inacheza mchezo hatari" inaporusha ndege zake za kivita katika anga karibu na Taiwan.

Biden aliapa wakati huo kwamba Marekani italinda kisiwa hicho kijeshi ikiwa kitashambuliwa.

Ni kutokana na cheche hizo za maneno katika ya viongozi hao kutoka mataifa yenye uwezo mkubwa duniani ndiposa tunalinganisha uwezo wa kijeshi wa Marekani na China.

Marekani

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Jeshi la Marekani

Marekani ina jumla ya wanajeshi milioni 1.4. Wakati jeshi la wanamaji linasemekana kuwa na wanajeshi 346,200.

Jeshi la Wanamaji la Marekani lina nyambizi 51 zinazobeba vichwa vya nyuklia na 11 za kubeba ndege. Kwa jumla, Jeshi la Wanamaji la Marekani lina meli za kivita 296.

Wanaanga wa Marekani ni tawi la huduma za Jeshi la Wanajeshi ambao wana utaalamu wa hali ya juu wa vita vya angani . Lilianzishwa mnamo Septemba 1947, chini ya Sheria ya Usalama wa Kitaifa ya 1947, na wakati huo ilikuwa moja ya matawi mapya ya jeshi la Marekani

Ndege nyingi za Jeshi la Anga ni F-16C Falcons, ambazo idade yake ni 783.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Silaha za kijshi za Marekani

Jeshi la angani la Marekani lilikuwa na ndege 4,100 zilizo tayari kupambana. Kwa kuongezea, Jeshi hilo lina makombora 400 ya balestiki yanayoweza kurushwa kutoka bara moja hadi jingine .

Idadi ya wafanyikazi wa akiba katika Idara ya Ulinzi ya Marekani imesalia thabiti tangu 1995. Mnamo 2020, kikosi cha akiba kilikuwa 795,955.

China

.

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Uchina ndio nchi yenye wanajeshi wengi zaidi duniani

Tathmini iliyofanywa na gazeti la Business insider linalonukuu tovuti ya Statista mwaka 2022 ilisema kuwa China ndiyo nchi yenye wanajeshi wengi zaidi duniani, huku wanajeshi wake wakifikia milioni 2.18.

Mnamo Oktoba 2019, China ilifanya mazoezi yake ya hivi karibuni ya kijeshi.

Iliwakilishwa na jeshi la askari 15,000, zana za kijeshi 580 na ndege 160 za kivita.

China ni nchi ya pili kwa matumizi makubwa ya kijeshi, inatumia dola bilioni 261 kila mwaka, kulingana na Taasisi ya Utafiti wa Amani ya Kimataifa ya Stockholm.

China ni nchi ya tatu kwa ukubwa kwa uwezo wa ndege za kivita, ikiwa na ndege 3,210.

China ina vifaru 3,200 na magari 33,000 ya kivita, kulingana na data iliyochapishwa na Global Firepower, tovuti ambayo inalinganisha nguvu za kijeshi za nchi duniani kote.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, China ni nchi ya tatu kwa ukubwa kwa uwezo wa ndege za kivita, ikiwa na ndege 3,210.

China ina magari 2,650 ya kufyatua makombora . Kwa upande wa nguvu za majini, China ina vyombo vya majini 777 vya aina mbalimbali. China ina manowari 74. Pia ina meli 36 za kivita maarufu Destroyer.