Waokoaji walivyokutana na miili iliyooza ya wachimba migodi walionasa Afrika Kusini

Wafanyakazi wa kujitolea Mzwandile Mkwayi (kulia) na Mandla Charles (kushoto) walilakiwa kama mashujaa baada ya kushuka kwenye shimo la kuchimba madini.
  • Author, Mayeni Jones na Khanyisile Ngcobo
  • Nafasi, BBC London na Johannesburg

Mzwandile Mkwayi alipokuwa akishushwa ndani ya mgodi wa Afrika Kusini ndani ya kizimba chekundu cha chuma kilichofungwa kwenye mashine ya kupandisha juu ya ardhi, kitu cha kwanza kilichompata ni harufu.

"Acha nikuambie kitu," anaiambia BBC, "miili hiyo ilikuwa na harufu mbaya".

Alipofika nyumbani baadaye siku hiyo, alimwambia mkewe hawezi kula nyama aliyoipika.

"Ni kwa sababu nilipozungumza na wachimbaji hao, waliniambia baadhi yao walilazimika kula [watu] wengine ndani ya mgodi kwa sababu hawakuweza kupata chakula. Na pia walikuwa wanakula mende," alisema kwenye simu kutoka nyumbani kwake.

Madai kuwa wachimbaji hao waliamua kula nyama ya binadamu ili kujinusuru pia yalitolewa na wachimba migodi wengine waliookolewa mwezi Disemba, katika taarifa zilizowasilishwa mahakama kuu.

Mkwayi, mfungwa wa zamani, anayejulikana kwa jina jingine Shasha, anaishi katika kitongoji cha Khuma ambacho kilikuwa karibu na mgodi ambao ulikuwa hautumiki huko Stilfontein. Kijana huyo mwenye umri wa miaka 36, ​​ambaye alikuwa ametumikia kifungo cha miaka saba jela kwa wizi, alijitolea kwenda chini ili kusaidia juhudi za uokoaji.

"Ninarekebishwa na huduma za urekebishaji na nilijitolea kwa sababu watu katika jamii yetu walikuwa wakitafuta msaada kwa watoto na kaka zao.

"Kampuni ya uokoaji ilisema haikuwa na mtu yeyote ambaye alitaka kushuka. Kwa hiyo mimi na rafiki yangu Mandla tulikubali kujitolea ili tuweze kuwasaidia ndugu zetu."

Lakini ingawa alitaka kusaidia, safari ya dakika 25 chini ya shimo lenye kina cha kilomita 2 (maili 1.2) ilimjaa hofu.

Unaweza kusoma
Mkwayi alishushwa shimoni kwenye kizimba

Chanzo cha picha, AFP

Mashine ya kushushia mara kwa mara ilisimama na kuanza, ikimwacha akining'inia gizani. Mara baada ya kushuka ndani ya mgodi, alishtushwa na alichokiona.

"Kulikuwa na miili mingi, zaidi ya miili 70, na karibu watu 200 ambao walikuwa wamepungukiwa na maji.

"Nilijihisi mnyonge sana nilipowaona, lilikuwa jambo la uchungu kuona. Lakini mimi na Mandla tuliona kuwa tulihitaji kuwa na nguvu na kutowaonesha jinsi tulivyohisi ili tuweze kuwatia moyo."

Wachimbaji madini ambao walikuwa wakingojea msaada kwa miezi kadhaa, waliwakaribisha kwa shangwe.

"Walikuwa na furaha sana," anasema.

Wachimbaji hao walikuwa wamekwama hapo kufuatia operesheni ya polisi nchini kote kukomesha uchimbaji haramu wa madini katika maeneo ambayo hayatumiki ambayo yalikuwa yamefungwa, kwani sekta hiyo, ambayo ilikuwa uti wa mgongo wa uchumi wa nchi, ilikuwa ikididimia.

Haikuwa na faida tena kwa makampuni ya kimataifa ya uchimbaji madini kufanya kazi katika maeneo mengi, lakini kupatikana kwa amana za dhahabu iliwavutia watu wengi waliokata tamaa, hasa wahamiaji wasio na vibali.

Maelfu ya mashimo yaliachwa.

Mnamo Novemba, polisi waliongeza juhudi katika mgodi wa Buffelsfontein huko Stilfontein, kuzunguka mlango wa shimoni na kukataa kuruhusu chakula na maji kushuka.

Kabla ya shughuli ya uokoaji kuanza Jumatatu, jamii katika eneo hilo ilikuwa imejaribu kuchukua hatua mikononi mwao kwa kushusha kamba chini ya shimo ili kujaribu kuwatoa baadhi ya watu.

Pia walituma ujumbe na kuwaambia wachimbaji mgodi kwamba msaada unakuja.

"Kwa hiyo tulipofika pale tayari walikuwa wanasubiri kreni. Sasa wakituona wanatuona sisi ni marais wao, sisi ni masiha wao: watu waliotoka nje kuingia shimoni kuwasaidia kutoka kwenye shimo hilo."

Polisi wanasema wachimbaji hao haramu walihimizwa kutoka nje lakini wenyewe walikuwa wakikataa kufanya hivyo kwa sababu walihofia kukamatwa.

Lakini Mkwayi hakubaliani na hilo: "Ni uwongo kwamba watu hawakutaka kujitokeza. Watu hao walikuwa wakihitaji msaada, walikuwa wanakufa."

Wakiwa katika eneo la mgodi siku ya Jumanne, BBC iliona makumi ya watu waliookolewa.

Walionekana wamedhoofika, mifupa yao ikionekana kupitia nguo zao. Wengine hawakuweza kutembea na ilibidi wasaidiwe na wafanyakazi wa afya.

Katika taarifa zilizowasilishwa kwa mahakama kuu, wachimba migodi hao haramu wanaelezea kwa undani vifo vya polepole na vya uchungu vya wenzao. Wanasema wengi walikufa kwa njaa.

Mkwayi anasema watu aliowaokoa walikuwa dhaifu kiasi kwamba kizimba cha uokoaji ambacho kilikusudiwa kubeba watu wazima saba wenye afya nzuri kiliweza kuchukua watu 13 kati yao.

"Walikuwa wamepungukiwa sana na maji na walikuwa wamepungua uzito hivyo tulifanikiwa kuingia zaidi kwenye kizimba, kwa sababu wasingebaki siku mbili tena chini kwenye shimo. Wangekufa tusingewatoa haraka iwezekanavyo. ."

Wafanyakazi wa kujitolea pia walikuwa na jukumu la kuleta maiti.

"Wahudumu wa uokoaji walitupa mabegi na kutuambia tuweke miili hiyo ndani na kuileta nje jambo ambalo tulifanya kwa msaada wa baadhi ya wachimbaji.

Operesheni ya uokoaji ilikusudiwa kudumu kwa takribani wiki moja, lakini baada ya siku tatu tu, waliojitolea walisema hakuna mtu aliyeachwa chini ya ardhi.

Mamlaka ilituma kamera chini ya shimo kufanya ukaguzi wa mwisho. Wanasema mgodi huo sasa utafungwa kabisa.

Lakini aliyoyapitia yamemuathiri sana Mkwayi.

Wakati fulani wakati wa mazungumzo ya simu alitaka swali lirudiwe, akieleza kuwa usikivu wake umeathiriwa tangu aingie shimoni mgodini, labda kwa sababu ya shinikizo.

Lakini athari mbaya zaidi imekuwa kutokana na kile alichoshuhudia.

"Lazima nikwambie, nina kiwewe. Sitasahau macho ya watu hawa katika maisha yangu yote."

Kwa wanaharakati na vyama vya wafanyakazi vinavyosaidia jamii, vifo vya watu 87 katika mgodi huo ni sawa na "mauaji" yaliyofanywa na mamlaka.

Matumizi ya neno hilo ya kusisimua yamelinganishwa na mauaji ya polisi ya wachimba migodi 34 waliokuwa wakigoma kupigwa risasi huko Marikana, umbali wa kilomita 150 kutoka Stilfontein, mwaka 2012.

Lakini wakati inaonekana wengi walikufa kwa njaa.

Mamlaka inakana kuhusika.

Jamii Imekuwa ikiandamana karibu na mgodi huo

Chanzo cha picha, Getty Images

Serikali ilianzisha msako dhidi ya wachimbaji madini haramu mnamo Desemba 2023 kupitia Operesheni Vala Umgodi (maana yake "funga shimo" kwa Zulu)

Migodi iliyotelekezwa ilikuwa imechukuliwa na magenge, mara nyingi yakiongozwa na wafanyakazi wa zamani, ambayo yaliuza kile kilichopatikana kwenye soko la biashara.

Watu walishirikishwa katika biashara hii haramu, ama kwa nguvu au kwa hiari, na kulazimishwa kutumia miezi kadhaa chini ya ardhi kuchimba madini. Serikali inasema uchimbaji madini haramu uligharimu uchumi wa Afrika Kusini $3.2bn (£2.6bn) mwaka 2024 pekee.

Kama sehemu ya oparesheni ya polisi, maeneo ya kuingilia katika migodi mbalimbali ambayo hayatumiki yalizuiwa, pamoja na chakula na maji, katika jitihada za kuwaondoa wachimbaji haramu, wanaojulikana kienyeji kama zama zama (ambayo inatafsiriwa kama "chukua nafasi").

Wakati Vala Umgodi ilifanikiwa kwa kiasi kikubwa katika majimbo mengine, mgodi wa dhahabu wa Buffelsfontein ulitoa changamoto ya kipekee.

Kabla ya operesheni ya polisi, wachimbaji wengi waliweza tu kuingia chini ya ardhi kupitia mfumo wa puli wa muda unaoendeshwa na watu juu ya ardhi.

Lakini kisha waliachana na sehemu ya juu ya shimo wakati maafisa wa usalama walifika kwa wingi mwezi Agosti, na kuwaacha wale waliokuwa kwenye mgodi huo wakiwa wamekwama.

Wanajamii kisha wakaingia kusaidia, wakiwavuta watu wachache juu kwa kutumia kamba, lakini huu ulikuwa mchakato mrefu na mgumu.

Njia nyingine ngumu na hatari za kutoka zilipatikana na kwa jumla karibu 2,000 ziliibuka tena, wengi walikamatwa na kusalia chini ya ulinzi wa polisi.

Kwa nini wengine hawakutoka haijulikani, wanaweza kuwa walikuwa dhaifu sana au walikuwa wakitishiwa na wafuasi wa genge katika mgodi, lakini waliachwa katika mazingira ya kukata tamaa.

Polisi wametetea operesheni hiyo huko Stilfontein, wakisema ilihusu kukabiliana na uhalifu

Chanzo cha picha, Getty Images

Kati ya 87 waliofariki, ni wawili tu ndio wametambuliwa, polisi walisema Alhamisi, wakieleza kwamba ukweli kwamba wengi walikuwa wahamiaji wasio na vibali ulifanya mchakato huo kuwa mgumu.

"Tunaona kwamba serikali ina damu mikononi mwake," Magnificent Mndebele kutoka kikundi cha Mining Affected Communities United in Action (Macua), aliiambia BBC.

Alisema kuwa wachimbaji hao hawakupewa onyo lolote kuhusu yale yaliyokuwa karibu kutokea kabla ya operesheni ya polisi kuanza.

Katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, Macua imekuwa mstari wa mbele katika makabiliano mbalimbali ya mahakama yaliyoanzishwa ili kuishinikiza serikali kwanza kuruhusu vifaa na kisha kufanya shughuli ya uokoaji.

Lawama zake kwa serikali zinaangazia kauli za awali kutoka kwa familia ambazo zilisema kwamba mamlaka imewaua wapendwa wao.

Walikuwa wamechukua hatua kali tangu operesheni ilipozidi. Mnamo Novemba, waziri mmoja, Khumbudzo Ntshavheni, alitoa kauli hiyo ambayo sasa ni mbaya wakati wa mkutano na waandishi wa habari kwamba wangeenda "kuwavuta".

Jimbo lilikataa kuruhusu chakula kutumwa au mtu yeyote kusaidia kuwapata wachimbaji hao, lakini iliambulia patupu baada ya maombi kadhaa ya mahakama kufanikiwa.

Mnamo Novemba, sehemu ndogo ya mahindi na maji ya papo hapo yalifikishwa shimoni, lakini katika taarifa ya mahakama, mmoja wa wachimbaji alisema haitoshi kwa mamia ya wanaume walio chini, ambao wengi wao walikuwa dhaifu sana hata kutafuna na kumeza.

Chakula zaidi kilitolewa mwezi Desemba, lakini tena hakikuweza kuwakimu.

Ikizingatiwa kuwa oparesheni ya kuwatoa watu hao na miili yao ilichukua siku tatu tu, jambo ambalo ni gumu kwa Mndebele kuelewa ni kwa nini jambo hilo lisingefanyika mapema, wakati ilionekana wazi kulikuwa na tatizo.

"Tumesikitishwa na serikali yetu, kusema ukweli, kwa sababu msaada huu umechelewa sana."

Wakati serikali bado haijajibu rasmi tuhuma hizo, polisi wameapa kuendelea na operesheni kubwa zaidi ya kusafisha migodi ambayo haijatumika hadi Mei mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Stilfontein siku ya Jumanne, Waziri wa Madini Gwede Mantashe alikuwa hakuomba radhi. Alisema serikali itaimarisha vita dhidi ya uchimbaji haramu wa madini, ambao aliutaja kuwa uhalifu na "mashambulizi dhidi ya uchumi".

Siku ya Alhamisi, Waziri wa Polisi Senzo Mchunu alikuwa na maridhiano zaidi.

"Ninaelewa na kukubali kuwa hili ni suala la kihisia. Kila mtu anataka kuhukumu... lakini itatusaidia sisi sote kama Waafrika Kusini watasubiri hadi wataalamu wa magonjwa wawe wamekamilisha kazi yao," alisema.

Polisi wametetea hatua yao, wakisema kuwapa wachimba migodi hao chakula "kungeruhusu uhalifu kushamiri".

Wachimbaji madini haramu wameshutumiwa kwa kuendeleza uhalifu katika jamii wanamofanyia kazi.

Hadithi kadhaa zimechapishwa katika vyombo vya habari vya ndani zikihusisha zama na ubakaji na mauaji mbalimbali.

Lakini kwa Mkwayi, ambaye aliweka usalama wake kwenye hatari kuwasaidia wachimbaji hao, wanaume wa mgodi wa Stilfontein walikuwa wakijaribu kujikimu kimaisha.

"Watu walishuka kilomita 2 wakiwa na kamba na kuhatarisha maisha yao kuweka chakula mezani kwa ajili ya familia zao."

Alisema anaitaka serikali kutoa leseni kwa wachimbaji wadogo ambao wanalazimika kwenda kwenye migodi ambayo haijatumika kutokana na kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira nchini Afrika Kusini.

"Ikiwa watoto wako wana njaa, hutafikiria mara mbili juu ya kwenda huko kwa sababu unapaswa kuwalisha. Utahatarisha maisha yako kuweka chakula mezani."

Unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Lizzy Masinga na kuhaririwa na Maryam Abdalla