Kilitokea nini kwa IS mwaka 2023?

Islamic State/Iraq/Syria

Chanzo cha picha, Getty Images

  • Author, Mina al-Lami
  • Nafasi, BBC Monitoring

Kundi la Islamic State (IS), ambalo liliwahi kushikilia eneo kubwa kutoka kaskazini-mashariki mwa Syria hadi kaskazini mwa Iraq, limeonesha dalili za kupungua kwa kiasi kikubwa kwa mashambulizi yake mwaka 2023, kwa mujibu wa data iliyokusanywa na BBC Monitoring.

Shughuli za IS zilikuwa chini kwa zaidi ya nusu ikilinganishwa na mwaka jana, na uongozi wa kundi hilo pia ulipata hasara.

Muungano wa kundi hilo la Misri ulinyamaza mwaka huu, na kuungana na matawi mengine yaliyolala huko Libya na Yemen. Wakati huo huo, mshirika wake wa Afghanistan alidai kuhusika na sehemu ndogo ya idadi ya mashambulizi ambayo ilidai kutekeleza mwaka jana.

Operesheni za kundi hilo barani Afrika pia zilitekeleza mashambulizi machache, isipokuwa tawi la Sahel, ambalo lilipanuka mashariki mwa Mali, lilifanya mashambulizi makubwa nchini Niger, na kulenga shughuli za propaganda.

Idadi hii inaashiria nini?

IS ilitekeleza jumla ya mashambulizi 838 duniani kote mwaka 2023, ukiondoa Desemba, ikilinganishwa na 1,811 kwa kipindi kama hicho mwaka jana, na kuashiria kushuka kwa 53%.

Uchambuzi na matokeo ya takwimu za mashambulizi yanatokana na madai rasmi ya IS yenyewe, ujumbe na propaganda na juu ya wafuasi wake. Kwa hivyo, takwimu zinaweza kutiwa chumvi au wakati fulani kupunguzwa.

Takwimu zote zilizotajwa za 2023 zinawakilisha mashambulizi yaliyofanywa kati ya 1 Januari na 30 Novemba.

Tunafahamu nini kuhusu mashambulizi ya IS ?

Kundi hilo lilidhibiti sehemu kubwa za Syria na Iraq, lakini kufikia 2017, lilikuwa limepoteza 95% ya eneo lake.

Mnamo mwaka wa 2019, muungano wa kimataifa unaoongozwa na Marekani na wanamgambo wa Kikurdi walichukua udhibiti wa kijiji cha Baghuz, ngome ya mwisho ya IS nchini Syria na kufuatiwa na kushindwa kwa kundi hilo ambalo lilisababisha kupungua kwa kundi hilo.

Tangu wakati huo, IS imejikita katika kujenga matawi yake ya Afrika, kwani ilitaka kugeuza mawazo kutokana na kushindwa kwake Mashariki ya Kati.

Kundi hilo bado linaendesha operesheni za waasi nchini Iraq na Syria na kusimamia mtandao wa washirika wasiopungua kumi na wawili katika Asia, Afrika na Mashariki ya Kati, lakini kupungua kwa kiasi kikubwa kwa shughuli zao kunaweza kuzingatiwa.

Tawi la IS lililoko Sinai, Misri, lilidai kuwa hakuna mashambulizi yoyote mwaka huu, ikilinganishwa na 102 mwaka jana, ikiwa ni pamoja na operesheni karibu na Mfereji wa Suez mwishoni mwa mwaka, ikionesha kuwa imepata pigo kali na majeshi ya Misri.

Mashambulizi yaliyofanywa na kundi linalojiita tawi la Jimbo la Khorasan (ISKP) nchini Afghanistan pia yalipungua, kwani kundi hilo lilitekeleza mashambulizi 20 mwaka 2023, ikilinganishwa na 145 mwaka jana na 293 mwaka 2021, mwaka ambao Taliban walirejea madarakani.

Ingawa kulikuwa na kupungua kwa idadi ya mashambulizi, yalisababisha idadi kubwa ya majeruhi.

Mnamo Julai, ISKP ilitekeleza shambulio la bomu la kujitoa muhanga katika mkutano wa kisiasa wa chama cha Kiislamu cha Jamiat Ulema-e-Islam-Fazl kaskazini-magharibi mwa Pakistan na kuua takribani watu 60.

Nchini Iraq, IS ilitekeleza jumla ya mashambulizi 141 mwaka 2023, ikilinganishwa na 401 kwa kipindi kama hicho mwaka jana, na kuashiria kushuka kwa 65%.

Kundi hilo lilitekeleza mashambulizi 112 nchini Syria mwaka huu, chini ya 292 mwaka jana.

Je, IS inakua Afrika ?

Tangu kupoteza kwa Baghuz mwaka wa 2019, IS imebadilisha propaganda zake ili kuzingatia "upanuzi" na "ushindi" wake katika Afrika,Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambapo ina matawi matano: Jimbo la Afrika Magharibi (ISWAP) Nigeria, DR Congo. Jimbo la Afrika ya Kati, ambalo mara kwa mara huvamia Uganda, tawi la Sahel, tawi la Msumbiji na tawi la Somalia.

Tawi lililofanya kazi zaidi lilikuwa ISWAP, ambalo linafanya kazi zaidi kaskazini-mashariki mwa Nigeria na eneo jirani la Ziwa Chad, lakini mwaka 2023, shughuli zao pia zimeshuka. Kundi hilo lilidai mashambulizi 470 mwaka 2022, na 266 mwaka 2023.

Matawi ya kundi hilo ya Jimbo la Afrika ya Kati na Msumbiji pia yalitekeleza mashambulizi machache, ingawa yalisalia kuwa tishio.

Wote wameendelea kufanya mashambulizi dhidi ya vikosi vya ndani na vya kikanda na vile vile dhidi ya walengwa wa kawaida, ambao ni wanakijiji wa Kikristo.

Jimbo la IS la Afrika ya Kati pia lilidai mashambulio manne mwaka huu nchini Uganda, moja likiwaua watalii wawili na kiongozi wao, lakini halikutekeleza shambulio baya la Juni katika shule ya sekondari magharibi mwa Uganda, ambayo ililaumiwa kwa kiasi kikubwa.

Kwa ujumla, mashambulizi yanayodaiwa na IS kutoka matawi yake ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara yalipungua hadi 508 mwaka 2023, kutoka jumla ya 847 mwaka uliopita. Hata hivyo, hii bado ilijumuisha 60% ya mashambulizi yote ya IS duniani - idadi kubwa zaidi kwa Afrika hadi sasa.

Shughuli za IS zinakua maeneo yapi?

Kwa mujibu wa data iliyokusanywa na BBC Monitoring, matawi ya IS katika eneo la Sahel na Ufilipino yalifanya kazi zaidi mwaka huu.

IS imeripotiwa kujitanua mashariki mwa Mali karibu na mpaka na Niger tangu Aprili. Ukuaji wa kundi hilo unakuja huku kukiwa na msukosuko wa kisiasa na kiusalama unaoendelea kuathiri nchi za Sahel, ambazo watu wenye itikadi kali wamekuwa wakitaka kuzinyonya.

Kati ya Julai na Oktoba, IS ilitoa ripoti na picha zinazoonesha "kampeni za kijeshi" ambazo kundi hilo lilidaiwa kutekeleza tangu Mei "kupambana na uhalifu".

Nyenzo zao za propaganda zilionekana kukuza sheria za Sharia katika maeneo ya mpaka kati ya Mali na Niger, zikifanya kazi kama mamlaka ya ndani.

Nchini Niger, kufuatia mapinduzi ya Julai nchini humo, IS ilidai mfululizo wa mashambulizi ya vifo vingi dhidi ya jeshi magharibi mwa nchi hiyo.

Shambulio moja la mwanzoni mwa Oktoba liliripotiwa kuwaua takribani wanajeshi 60, na kusababisha serikali ya Niger kutangaza siku tatu za maombolezo.

Tangu 2014, IS imekuwa ikipokea ahadi za utii kutoka kwa vikundi vya wanamgambo huko Kusini-mashariki mwa Asia pia. Washirika wa kundi hilo katika eneo hilo wanafanya kazi zaidi kwenye visiwa vya kusini mwa Ufilipino ambako kuna Waislamu wengi katika nchi hiyo yenye Wakristo wengi.

Tangu Julai, matawi ya kikundi hicho yalitekeleza mashambulizi 20 mwaka huu, ikilinganishwa na saba mnamo 2022.

IS pia ilidai kuhusika na shambulizi wakati wa misa ya Wakatoliki kusini mwa Ufilipino tarehe 3 Desemba, nje ya kipindi ambacho takwimu zetu zinaangalia. na kutoa wito wa ajira katika eneo hilo.

Je, tunajua nini kuhusu viongozi wa IS?

Kundi hilo hivi karibuni limepata hasara kubwa katika safu ya uongozi wake.

IS ilipoteza viongozi watatu tofauti katika muda wa mwaka mmoja, wote waliuawa nchini Syria kati ya Februari 2022 na Aprili 2023.

Kutokana kifo cha Abu Bakr al-Baghdadi katika uvamizi wa Marekani tarehe 27 Oktoba 2019, kundi hilo liliongozwa na Abu Ibrahim al-Hashimi al-Qurashi, kisha Abu al-Hasan al-Qurashi na baadaye Abu al-Hussein al-Qurashi.

Tangu kundi hilo lilipojitangaza kuwa "ukhalifa" mnamo Juni 2014, waliendelea kuwataja viongozi wao kama "makhalifa", wa kwanza akiwa al-Baghdadi.

Mnamo Agosti 2023, IS iliwasilisha kiongozi mpya, Abu Hafs al-Hashimi al-Qurashi, lakini machache yanajulikana kumhusu na bado hajatoa ujumbe wa uongozi.

IS pia ilipoteza baadhi ya makamanda wake wakuu, haswa Syria na Iraq, haswa katika mashambulizi ya vikosi vya muungano unaoongozwa na Marekani.

Mwezi Agosti, jeshi la Msumbiji lilisema limemuua mkuu wa IS katika kaunti hiyo, lakini kundi hilo mara chache hutoa kauli yake kuhusu mauaji hayo, isipokuwa katika kesi ya "khalifa" na msemaji wake.

Wanajeshi wa Iraqi wakiwa wamebeba bendera

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Athari ya vita huko Gaza ni ipi ?

Operesheni za kijeshi dhidi ya IS na ushindani kutoka kwa makundi hasimu katika baadhi ya nchi zikiwemo Somalia, Sahel, eneo la Ziwa Chad, na Syria zinaaminika kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia kuporomoka kwa shughuli za kundi hilo.

Hasara za uongozi na kutokujulikana kwa uongozi wa sasa pia inachukuliwa kuwa sababu kuu.

Lakini bado kuna mamia ya mashambulizi ya IS, hasa barani Afrika, na kundi hilo linaendelea kufanya kazi katika nchi nyingi kwa kutumia udhaifu wa kisiasa, usalama na jumuiya.

Vita vya Gaza vinaweza kuonekana kama moja ya "fursa" ya IS na makundi mengine yenye itikadi kali, ambao wangetafuta njia za kutumia mzozo huo kuelekeza hasira dhidi ya maadui zao.

Takribani watu 20,000 sasa wameripotiwa kuuawa na zaidi ya 52,000 kujeruhiwa huko Gaza tangu kuanza kwa vita, ambavyo vilikuja baada ya uvamizi wa Hamas nchini Israel tarehe 7 Oktoba kuua watu 1,200 (watu wengine 240 walichukuliwa mateka).

Ingawa al-Qaeda ilitoa wito kwa Waislamu kushiriki katika mapigano hayo pamoja na wanamgambo wa Kipalestina, jibu la IS, lililochapishwa katika gazeti la kila wiki la kundi hilo la al-Naba, halikuyasifu makundi ya Wapalestina, wala haikutoa wito kwa Waislamu kuunga mkono Hamas.

Kundi hilo hapo awali lilikuwa likishutumu Hamas kwa kuwakandamiza wafuasi wake katika Ukanda wa Gaza. Badala yake, IS ililenga kuchochea mashambulizi ya kulipiza kisasi duniani kote, ikiwa ni pamoja na dhidi ya serikali za Kiarabu ambazo ilizishutumu kwa "kuilinda" Israeli.

Imetafsiriwa na Lizzy Masinga