Jinsi Wapoland wa kawaida wanavyojiandaa kwa uvamizi wa Urusi

Katika uwanja wa mafunzo ya kijeshi karibu na jiji la Wroclaw, Wapoland wa kawaida wamepanga mstari, wakisubiri kukabidhiwa bunduki na kufundishwa jinsi ya kupiga risasi. "Mara tu duru inapopakiwa, silaha iko tayari kufyatua risasi," anafoka mwalimu, askari wa Poland, uso wake ukiwa umepakwa rangi ili kuficha utambulisho wake.
Vijana na wazee, wanaume na wanawake, wazazi na watoto, wote wamekuja hapa kwasababu moja: kujifunza jinsi ya kunusurika mashambulizi ya silaha.
Pamoja na kuwasha safu ya upigaji risasi, kipindi cha Jumamosi hii asubuhi, kiitwacho "Train with the Army" [Jifunze na Jeshi] , pia hufundisha raia mapigano ya ana kwa ana, huduma ya kwanza na jinsi ya kuvaa barakoa ya gesi.
"Nyakati ni hatari sasa, tunatakiwa kuwa tayari," anasema mratibu wa mradi huo, Kapteni Adam Sielicki. "Tuna tishio la kijeshi kutoka Urusi, na tunajiandaa kwa hili."
Kapteni Sielicki anasema mpango huo umefuatiliwa kupita kiasi, na serikali ya Poland sasa ina mipango ya kuupanua ili kila mtu mzima wa kiume nchini apate mafunzo. Poland, ambayo inashiriki mipaka na Urusi na Ukraine, inasema itatumia karibu 5% ya Pato la Taifa katika ulinzi mwaka huu, kiasi ambacho ni ya juu zaidi katika Nato.

Wiki iliyopita, Waziri Mkuu Donald Tusk alisema Poland inalenga kujenga "jeshi lenye nguvu zaidi katika eneo hilo". Imekuwa ikitumia matumizi makubwa ya fedha, kununua ndege, meli, mifumo ya mizinga na makombora kutoka Marekani, Sweden na Korea Kusini, miongoni mwa mengine.
Dariusz ni mmoja wa wale wanaohudhuria kozi ya Jumamosi huko Wroclaw, na anasema atakuwa "wa kwanza kabisa" kujitolea ikiwa Poland ingeshambuliwa. "Historia imetufundisha kwamba ni lazima tujiandae kujilinda sisi wenyewe. Hatuwezi kumtegemea mtu mwingine yeyote. Leo miungano ipo, na kesho inavunjika."
Anapoondoa barakoa yake ya gesi, Bartek anasema anadhani Wapoland wengi "watachukua silaha" ikiwa watashambuliwa, "na kuwa tayari kulinda nchi."
Agata anahudhuria na rafiki. Anasema kuchaguliwa kwa Donald Trump kumewafanya watu kuwa na wasiwasi zaidi. "Anataka kujiondoa [Ulaya]. Ndiyo maana tunahisi kuwa salama hata kidogo. Kama hatuko tayari na Urusi kutushambulia, tutakuwa wafungwa wao."

Kauli za Donald Trump na wajumbe wa utawala wake zimezua wasiwasi mkubwa miongoni mwa maafisa wa Warsaw. Wakati wa ziara yake katika mji mkuu wa Poland mwezi Februari, waziri wa ulinzi wa Marekani Pete Hegseth alisema Ulaya haipaswi kudhani kuwa uwepo wa wanajeshi wa Marekani katika bara hilo "utadumu milele".
Kwa sasa Marekani ina wanajeshi 10,000 walioko Poland, lakini Washington ilitangaza mwezi uliopita kuwa inajiondoa katika kambi muhimu ya kijeshi katika mji wa Rzeszow mashariki mwa Poland. Maafisa wanasema wanajeshi hao watatumwa tena ndani ya Poland, lakini hatua hiyo imesababisha wasiwasi zaidi nchini humo.
Uadui wa Donald Trump dhidi ya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, na maneno ya joto kwa Vladimir Putin wa Urusi, yameongeza tu wasiwasi.
Poland inatazamiwa kusaini makubaliano ya ulinzi na Ufaransa katika siku zijazo, na mkataba mwingine na Uingereza uko mbioni - hatua zaidi za Warsaw kujiondoa katika uhusiano wake wa kihistoria wa kijeshi na Washington. Pia kuna mazungumzo ya Poland kuletwa chini ya "mwavuli wa nyuklia" wa jeshi la Ufaransa.
"Nadhani [Trump] hakika ametusukuma kufikiria kwa ubunifu zaidi kuhusu usalama wetu," anasema Tomasz Szatkowski, mwakilishi wa kudumu wa Poland katika Nato na mshauri wa rais kuhusu ulinzi. "Nadhani Marekani haiwezi kumudu kuipoteza Poland, kwa sababu hiyo itakuwa ishara ... kwamba huwezi kutegemea Marekani. Hata hivyo, inabidi tufikirie chaguzi nyingine na kukuza uwezo wetu wenyewe."
"Ikiwa Warusi wataendelea na nia yao ya uchokozi kuelekea Ulaya, tutakuwa wa kwanza - mlinda lango," Bw Szatkowski anasema. Anaelezea ujengaji wa haraka wa kijeshi wa Poland kwa "kwanza kabisa, hali ya kijiografia, lakini pia, uzoefu wa historia."

Machungu ya uvamizi wa Urusi yanasikika kila mahali hapa.
Katika nyumba ya matunzo ya wazee wa serikali huko Warsaw, Wanda Traczyk-Stawska mwenye umri wa miaka 98 anakumbuka mara ya mwisho majeshi ya Urusi yalipovamia - mnamo 1939, wakati mapatano kati ya Stalin na Hitler yalisababisha Poland kuwekwa kati ya USSR na Ujerumani ya Nazi.
"Mnamo 1939 nilikuwa na umri wa miaka kumi na miwili. Nakumbuka baba yangu alihangaikia sana [Warusi]," Wanda akumbuka, "Tulijua kwamba Urusi ilikuwa imetushambulia, walichukua fursa ya ukweli kwamba Wajerumani walikuwa wametufichua."
Kwenye ukuta kuna picha ya Wanda kama mpiganaji, akionyesha bunduki wakati wa Machafuko ya Warsaw ya 1944, wakati Wapolishi walipigana chini ya ardhi na Jeshi la Ujerumani katikati ya magofu ya jiji. Baada ya kuwarudisha nyuma Wajerumani katika siku za mwisho za Vita vya Kidunia vya pili, Umoja wa Kisovieti uliweka serikali inayounga mkono Moscow huko Poland, ambayo ilitawala nchi hiyo hadi 1989.
Hivi sasa, karibu wanajeshi wanawake 216,000 wanaunda vikosi vya jeshi la Poland. Serikali inasema inanuia kuongeza hiyo hadi nusu milioni, ikiwa ni pamoja na askari wa akiba - idadi ambayo itaipa jeshi la pili kwa ukubwa katika Nato baada ya Marekani.

Ninamuuliza Wanda kama anafikiri ni jambo zuri kwamba Poland inajenga jeshi lake. "Bila shaka, ndiyo. Urusi ina uchokozi huu ulioandikwa katika historia yake. Sizungumzi juu ya watu, lakini mamlaka huwa hivyo kila wakati, "anavuta pumzi. "Ni bora kuwa nchi yenye silaha kuliko kusubiri kitu kitokee. Kwasababu mimi ni mwanajeshi ninayekumbuka kuwa silaha ndio kitu muhimu zaidi."
Miaka themanini tangu kumalizika kwa Vita vya Kidunia vya pili, Poland kwa mara nyingine tena inawatazama majirani zao kwa woga. Katika ghala moja kusini mwa Poland, kwa mahitaji ya watu wengi, kampuni moja imeunda mfano wa makazi ya bomu.
"Makazi haya yameundwa kimsingi kulinda dhidi ya bomu la nyuklia, lakini pia dhidi ya mashambulizi ya silaha," anasema Janusz Janczy, bosi wa ShelterPro, ambaye ananionyesha kuzunguka chumba cha chuma, kamili na vitanda vya bunk na mfumo wa uingizaji hewa. "Watu wanajenga makazi haya kwa sababu tu hawajui nini cha kutarajia kesho."

Janusz anasema mahitaji ya makazi yake yameongezeka tangu Donald Trump aingie madarakani. "Ilikuwa ni simu chache tu kwa mwezi. Sasa kuna dazeni kwa wiki," anasema, "Wateja wangu wanaiogopa zaidi Urusi. Na wana wasiwasi kuwa Nato isingekuja kutetea Poland."
Lakini je, Poles wako tayari kutetea nchi ikiwa hofu hizo zitatimia? Kura ya maoni ya hivi majuzi iligundua kuwa ni 10.7% tu ya watu wazima walisema watajiunga na jeshi kama watu wa kujitolea katika tukio la vita, na theluthi moja walisema watakimbia.
Mjini Wroclaw, ninawauliza wanafunzi wa Poland kama watakuwa tayari kutetea nchi yao ikiwa itashambuliwa. Wengi wanasema hawataweza. "Vita viko karibu sana lakini vinahisi kuwa mbali," anasema mwanafunzi wa matibabu Marcel, "lakini ikiwa Urusi ingeshambulia, nadhani ningekimbia."
"Pengine ningekuwa wa kwanza kujaribu kutoroka nchini," anasema mwanafunzi mwingine, Szymon. "Sioni chochote cha kufa kwa ajili ya hapa."
Ripoti ya ziada na Aleksandra Stefanowicz
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi