Malalamiko dhidi ya tangazo la pedi linalodaiwa kudhalilisha wanawake lapuuzwa nchini Australia

Chanzo cha picha, ASALEO CARE
Matangazo ya awali yanayoashiria damu ya hedhi kwenye televisheni nchini Australia yanadaiwa kutokwenda kinyume cha kiwango, wasimamizi wamesema.
Matangazo hayo yanayotangaza biashara za pedi, mwezi uliopita yalionyesha madoa ya damu katika nguo ya ndani na damu ikiwa inachirizika kwenye miguu ya mwanamke.
Watazamaji zaidi ya 600 waliandika malalamiko yao na kudai kuwa matangazo hayo ya kibiashara yalikuwa yanaenda kinyume na maadili - idadi ya malalamiko hayo ni kubwa kuliko matangazo yote kwa mwaka 2019.
Lakini mamlaka ya kuthibiti viwanda nchini humo imepuuzia malalamiko hayo na kusifia ujumbe uliotumika katika kuashiria maudhui.
Wasimamizi wa matangazo wanasema kuwa kampeni hiyo inaonesha namna gani usawa unakuwa na uwasilishi wa hedhi umeboreshwa".
Kampuni mama ya pedi hizo za Libra, Asaleo Care, imesema kuwa tangazo hilo limeweza kuachana na mila potofu katika jamii dhidi ya hedhi kwa sababu wanawake wengi wasichana huwa wanaona aibu kuzungumzia masuala ya hedhi hadharani.
Ni tamaduni ambayo wengi wanaona hedhi ni jambo la siri lakini tangazo hilo limeonyesha wazi kuwa mwanamke kupata hedhi ni jambo la kawaida, hivyo ndivyo inapaswa iwe kwa kila mtu.

Chanzo cha picha, Asaleo Care
Watazamaji ambao wametoa malalamiko hayo walidai kuwa matangazo yalikuwa "yanaaibisha na hayakuonyeshwa sehemu sahihi na yalifedhehesha".
Katika majibu yao, mamlaka ya usimamizi wa maudhui ilieleza kuwa baadhi ya watazamaji wasingependa kuona sehemu ya mwili ikititirika damu katika televisheni.
lakini tangazo hilo halikwenda kinyume na maadili .
Wamekataa kufanyia kazi malalamiko hayo ya tangazo kuwa baya katika jamii na liliwekwa katika muda ambao hata watoto wanakuwa wanaangalia.
"Hakuna lugha mbaya au picha mbaya ambayo imeonekana katika tangazo hilo...
Wanapaswa kutojisikia aibu au kuona wamedhalilishwa kwenye matangazo ya hedhi kwa sababu ni kila mwanamke anapitia na hedhi ni jambo la kawaida ," Mamlaka ya maudhui iliandika katika ripoti yake kujibu tuhuma za malalamiko ya wananchi.
Kampeni ya pedi inayoonyesha doa jekundu linaloashiria damu katika pedi badala ya kutumia rangi ya blu ilianza mwaka 2017 nchini Uingereza na kampeni hiyo imeweza kuenea maeneo mengi ya Ulaya, Marekani na Afrika Kusini.
Miaka sita kabla, kampuni ya taulo za wanawake Always ilikuwa ya kwanzakutengeneza tangazo la pedi kwa doti nyekundu badala ya blu katika pedi za maxi.
Wazo hilo lilitolewa mwaka 2011.